LATEST ARTICLES

Spika wa Bunge la Uganda, Jacob Oulanyah afariki Dunia

0

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza kifo cha Spika wa Bunge la Uganda, Jacob Oulanyah leo Jumapili

Kilichosababisha kifo cha Oulanyah hakijabainishwa lakini alikuwa amelazwa Hospitali nchini Marekani kwa zaidi ya mwezi mmoja na ilizua mjadala kwa Waganda ambao walidai iligharimu pesa nyingi sana za walipa kodi kumtibu.

Oulanyah alichukua kiti cha Spika wa Bunge la Uganda mnamo Mei 2021 na kabla ya hapo alikuwa Naibu Spika kuanzia 2011.

Kusafirishwa kwake hadi Marekani kwa matibabu kulizua mjadala miongoni mwa Waganda, ambao walidai kuwa iligharimu pesa nyingi sana za walipa kodi.

Oulanyah alichukua hatamu ya uongozi wa bunge la Uganda mnamo Mei 2021. Alikuwa naibu spika kuanzia 2011.

Alikuwa na sifa ya kuanzisha vikao vya bunge kwa wakati, na kila mara alitoa wito kwa wabunge kuimarisha ubora wa mijadala, kwa kujadili mambo waliyo na ufahamu wa kina.

Alikuwa mwanasheria na mwanasiasa wa muda mrefui. Aliwahi kuwa mbunge wa Eneo Bunge la Kaunti ya Omoro, kaskazini mwa nchi.

Oulanyah alikuwa miongoni mwa wanasiasa kutoka eneo hilo walioshiriki katika mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Uganda na waasi wa Lord’s Resistance Army walioongozwa na Joseph Kony miaka ya 2000.

Nafasi ya ‘diet’ na mazoezi katika kupunguza uzito

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania hivi karibuni imeeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanasababisha vifo kati ya asilimia 40 hadi 45 ya vifo vyote vinavyotokea hospitalini, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 33 miaka mitano iliyopita.

Kutokana na hali hiyo, wizara imeshauri hatua mbalimbali za kuchukuliwa ili kukabiliana na kasi ya ongezeko la vifo hivyo ambapo miongoni mwa hatua hizo ni kupunguza ulaji wa vyakula vya mafuta, chumvi nyingi, unywaji wa pombe na kufanya mazoezi.

Kutokana na msingi huo, tumefanya mahojiano na Dkt. Hussein Ngaillah kutoka Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma kuhusu nafasi ya diet (ulaji chakula) na ufanyaji mazoezi katika kuwezesha watu kupunguza uzito.

Mambo tuliyozungumza ni pamoja na;

Nafasi ya Diet katika kupunguza uzito

Kwa lugha nyepesi Dkt. Ngailllah amesema kuwa diet ni namna fulani ya ulaji wa vyakula ikiwa lengo kuu ni kupunguza uzito. Ameeleza kuwa diet ina nafasi kwenye kupunguza uzito kwa sababu msingi mkubwa ni kupunguza kiwango cha vyakula hasa vya wanga na kuruhusu mwili kutumia mafuta kama chanzo cha nishati. Kwa mantiki hiyo, mafuta ambayo ndiyo yanasababisha uzito mwilini yanapungua.

Je diet inafanya kazi? Jibu ni ndio, inafanya kazi. ndani ya miezi 3-6, unakuwa umepungua uzito.

Kuna mmoja katika wazungumzaji aliwahi kusema kwama “hatuli hadi tuwe na njaa na tukila hatushibi.” Maana yake wanakula kiwango cha chakula kile tu ambacho kinahitajika ili kuupa mwili nguvu. Wajuzi wa mambo wanashauri kuwe na ratiba ya kula, kwa siku isizidi milo mitano, kwa asubuhi, mchana na jioni na inayokuwa ya kutafuna vyakula vyepesi baina ya milo hiyo na hupaswi kula chochote katikati ya hiyo.

Pia hupaswi kuvukisha kifungua kinywa (breakfast) na hupaswi kula usiku sana muda wa mwili kulala. Mlo wako wa asubuhi uwe unaeleweka, wenyewe huita chai nzito, halafu mchana unakula kawaida na jioni chakula chepesi.

Vyakula vya kupunguza uzito

Dkt. Ngailllah ameelekeza kuwa vyakula vinavyopaswa kuliwa na mtu unayetaka kupungua uzito ni, 1). vyakula vya protini, matunda, mboga za majani, vyakula vya jamii ya kunde, karanga na mbegu, 2). Nafaka ambazo hazijakobolewa, kupunguza matumizi ya sukari na soda, 3). Kula mafuta ya mimea na kupunguza mafuta ya wanyama, 4.) Kula vyakula ambavyo huchelewa kumeng’enywa na kukufanya ukae kwa mda mrefu bila kusikia njaa na 5). Maji safi na salama.

Mazoezi ya kupunguza uzito

Wataalamu wanashauri kwa uchache mtu atumie dakika 150 kwa wiki kwa mazoezi mepesi na dakika 75 kwa mazoezi magumu. Na haya yanaweza kuwa kukimbia, kutembea mwendo wa haraka, kucheza muziki, kuruka kamba, kuogelea, kuendesha baiskeli au kuinua vitu vizito. Lengo ni jasho litoke, na mtu afanye mazoezi yale anayoyaweza kila siku kwa dakika 15 hadi dakika 30, afurahie mazoezi na asione kama adhabu.

Diet na mazoezi, ipi njia bora kupunguza uzito?

Kulijibu hili swali, nitakupa mfano, amesema Ngaillah, ukiacha hawa Wamasai waliopo mijini, ukienda kule umasaini hauwezi kukuta Mmasai anakitambi au bwanyenye, au kuna kabila fulani hivi dogo liko Pakistani milimani kule, hutawakuta wamenenepeana.

Siku zote wana miili fulani hivi, tunaiita mti mkavu. Kwanini? Kwa sababu muda mwingi wanatumia kikimbizana na wanyama, kupandisha milima kwa wale wa Pakistani kule, hayo ni mazoezi. Kila siku wanachoma mafuta mwilini na hakuna ziada inayobaki kuwafanya wanenepe kiholela, na hiyo ni kutokana na kuwa hawapati mafuta ya ziada jambo linalochangiwa na vyakula pamoja na ratiba za kula.

Watu hao wanakula vyakula vya kambakamba, vyakula asili na bila mafuta. Kwa hiyo, diet na mazoezi yanaenda bega kwa bega linapokuja suala la kupungua uzito hasa mazoezi.

Aidha, amesema kuwa diet pekee siyo njia bora sana kwa sababu, unaunyima mwili chakula ambacho kinaufanya ufanye kazi, pamoja baadhi ya madini na vitamini na kusababisha baadhi ya seli kuharibika. Ameongeza kuwa diet siyo njia endelevu kwani pindi mtu akisitisha anaweza kurudi kwenye kunenepa tena.

Kutokana na hayo ameshauri kuwa mtu anayetaka kupungua uzito abadili namna ya ulaji wake, ale vyakula asili, apunguze vyakula vya mafuta, afanye mazoezi, apate usingizi bora wa saa zisizopungua saba. Pia ameshauri mhusika aboreshe afya ya akili, aweze kudhibiti hofu na msongo wa mawazo.

Dkt. Ngaillah anapatikana kupitia ukurasa wa Twitter @Ngaillah_ na kwa njia ya simu 0713988457

Chongolo akagua bwawa na Nsenkwa

0

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo @daniel_godfrey_chongolo akisalimiana na Chifu wa kabila la Wakonongo, Michael Kayamba baada ya kuwasili katika jimbo la Katavi.

Chongolo amefika katika jimbo hilo la Katavi kwa lengo la kutembelea na kukagua mradi mkubwa wa bwawa la Nsenkwa linalojengwa kwa ajili ya kuwa chanzo cha maji kwa matumizi ya Wananchi wa vijiji 16 katika halmashauri ya Mlele mkoa wa Katavi.

Mradi huo utakaowahudumia takribani wakazi elfu 68, utagharimu shilingi Bilioni 2.8.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo Chongolo amewapongeza wote waliobuni mrati huo kwa kusema kuwa wamebuni jambo litakalokuwa na matokeo makubwa na chanya kwa Wananchi.

TPA TUNAHITAJI BANDARI MAALUM YA MIFUGO

0

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ameielekeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha inaanzisha bandari maalum kwa ajili ya mifugo katika maeneo ambayo itaona yanafaa.

Akizungumza wakati wa ziara yake alipotembelea bandari ya Lindi Kihenzile amesema, Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi Afrika hivyo ni lazima kuwepo na bandari hiyo.

Amesema sio jambo jema kuchanganya mifugo na mizigo mingine kama vile mazao ya chakula, saruji na makaa ya mawe.

Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kuwa kwa kuzingatia juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya mifugo nchini, upo uhitaji wa kwenda na kasi hiyo kwani kwa sasa nchi jirani wana bandari kubwa maalum kwa ajili ya mifugo.

Aidha, ameielekeza TPA kukamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bandari nyingine mkoani Lindi katika eneo la Mitwele.

Naibu Waziri Kihenzile amekamilisha ziara yake ya siku mbili katika mikoa ya Mtwara na Lindi, iliyokuwa na lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni wakati wa ziara yake katika mikoa hiyo.

Bilioni 70 zatengwa kulipa madeni ya Makandarasi kila mwezi

0

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga shilingi Bilioni 70 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya makandarasi wanaoendelea kutekeleza miradi ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege nchini.

Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo Bilioni 50 zinaenda kulipa makandarasi wa ndani na Bilioni 20 kwa makandarasi wa nje.

Amesema hayo wakati akikagua utekelezaji wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa ambao ujenzi wake umefikia hatua za mwisho na unatarajiwa kukabidhiwa kwa wana Iringa mwishoni mwa mwezi huu.

“Mheshimiwa Rais ameiwezesha Wizara ya Ujenzi kwa kutupa Bilioni 70 kwa ajili ya kulipa makandarasi wa ndani kama kipaumbele cha kwanza kwa madeni ambayo wamekuwa wakidai hadi Juni 30, 2023”, amesema Bashungwa.

Ameongeza kuwa kwa utaratibu huo ndani ya miezi mitatu na nusu Serikali itakuwa imekamilisha madeni ya makandarasi wa ndani ili kazi zote zilizokuwa zikifanywa na makandarasi hao zisiweze kusimama, baada ya hapo fedha hizo (bil 70) zitaendelea kulipa madeni yaliyobaki kwa wakandarasi wa nje.

Bashungwa amesema kuwa mbali na Serikali kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja ya kimkakati juhudi hizo zinaenda sambamba na kujenga anga la Tanzania ili kuimarisha usafiri wa anga kwa kuboresha viwanja vya ndege nchini.

Kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Waziri Bashungwa amesema ni maelekezo ya Rais kukamilisha kiwanja hicho kwa viwango vya juu ili kuruhusu ndege kuruka na kutua saa 24.

“Wana Iringa niwapongeze sana kwa kupata uwanja, uwanja ambao sasa hivi hata wawekezaji wanaotaka kuwekeza Iringa watakuwa na uhakika kuna uwanja ambao umezingatia mambo yote ya kiusalama”, amefafanua Bashungwa.

KOMBE LA DUNIA KUCHEZWA AFRIKA

0

Michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2030 itachezwa kwenye nchi sita katika mabara matatu tofauti.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) imesema nchi tatu za Morocco, Ureno na Hispania watakuwa wenyeji wenza wa michuano hiyo ya Kombe la Dunia mwaka 2030.

Kwa Morocco kupewa nafasi hiyo ya uenyeji wenza wa Kombe la Dunia mwaka 2030 inakuwa nchi ya pili ya Afrika kuandaa michuano hiyo baada ya Afrika Kusini iliyoandaa mwaka 2010.

Lakini mechi tatu za ufunguzi za michuano hiyo ya mwaka 2030 zitachezwa huko Amerika Kusini ikiwa ni sehemu maalum ya maadhimisho ya miaka 100 ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia.

Mechi hizo zitachezwa kwenye nchi za Uruguay, Argentina na Paraguay.

Michuano ya Kombe la Dunia ilianza mwaka 1930 nchini Uruguay na mwaka huu itakuwa imetimia miaka mia moja tangu kuanzishwa, na FIFA imepeleka sherehe hizo kufanyika kwenye nchi hizo ambazo awali nazo zilitangaza nia ya kuomba kuandaa michuano hiyo ya mwaka 2030.

FIFA imetoa nafasi kwa nchi za Bara la Asia na Ocenia kuomba kuandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2034 na tayari Saudia Arabia imeonesha nia hiyo.

Mechi ya ufunguzi kwenye michuano hiyo ya mwaka 2030 itachezwa kwenye jiji la Montevideo nchini Uruguay ambako kulichezwa mechi ya kwanza ya kombe la Dunia la mwaka 1930 na baadae kufuatiwa na michezo mingine miwili itayochezwa kwenye nchi za Argentina na Paraguay.

Baada ya hapo michuano hiyo itakayoshirikisha timu 48 itahamia kuchezwa kwenye Bara la Afrika na Ulaya kwenye nchi za Morocco, Ureno na Hispania.

TPA kujenga Bandari ya Mbamba Bay

0

Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Juma Kajivara amesema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imetangaza zabuni na inakaribia kupata mkandarasi kwa ajili ya kujenga Bandari ya Mbamba Bay iliyopo Ziwa Nyasa.

Mhandisi Kajivara ameyasema hayo mkoani Mtwara alipokuwa akieleza namna TPA imejipanga kuhudumia mizigo kutoka nchi jirani kwa kutumia bandari ya Mtwara wakati ukiendelea na mkutano wa wadau wa kujadili juu ya maandalizi ya usafirishaji wa zao la korosho kupitia bandari ya Mtwara.

Ameongeza, ni matarajio kuwa mizigo kutoka nchi ya Malawi itapita bandari ya Mtwara kisha kuelekea Mbamba Bay ili kufika Malawi, akisisitiza kuwa hiyo ni njia pekee fupi ya kusafirisha mizigo kutoka Tanzania hadi Malawi.

BANDARI NYINGINE KUJENGWA MTWARA

0

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema pamoja na kuwa wizara hiyo ina mipango ya muda mfupi katika usimamizi na matumizi ya bandari ya Mtwara, Serikali inakwenda kujenga bandari nyingine mkoani humo katika eneo linalofahamika kama kisiwa Mgao ambapo kwa sasa hatua za manunuzi zimeanza.

Akizungumza mkoani Mtwara wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa bandari ya Mtwara Naibu Waziri Kihenzile amesema, bandari hiyo mpya itakuwa ni maalumu kwa ajili ya usafirishaji bidhaa zijulikanazo kama ‘bidhaa chafu’ ambazo ni kama makaa ya mawe na saruji.

Amesema wizara ya Uchukuzi inaendelea kuweka mikakati ya namna ya kuimarisha bandari ya Mtwara ili kuhakikisha bidhaa nyingine pia zinasafirishwa kwa wingi.

Katika ziara yake mkoani Mtwara Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ametembelea na kukagua utendaji kazi wa bandari ya Mtwara na uwanja wa ndege wa Mtwara.

TPA YATAKIWA KUSIMAMIA UBORA WA KOROSHO BANDARINI

0

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ameuelekeza uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Mtwara kukaa pamoja na kujadili namna bora ya kufungasha mizigo ya korosho kabla ya kuisafirisha.

Kihenzile ameyasema hayo mkoani Mtwara alipokuwa akizungumza katika mkutano wa wadau kwa ajili ya maandalizi ya usafirishaji wa zao la korosho kupitia bandari ya Mtwara.

Kihenzile pia ameitaka TPA kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelelekzo ya Serikali kuhusu sekta ya uchukuzi na kutoa taarifa za mara kwa mara kwa Wizara ya Uchukuzi.