KOMBE LA DUNIA KUCHEZWA AFRIKA

0
147

Michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2030 itachezwa kwenye nchi sita katika mabara matatu tofauti.

Taarifa ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) imesema nchi tatu za Morocco, Ureno na Hispania watakuwa wenyeji wenza wa michuano hiyo ya Kombe la Dunia mwaka 2030.

Kwa Morocco kupewa nafasi hiyo ya uenyeji wenza wa Kombe la Dunia mwaka 2030 inakuwa nchi ya pili ya Afrika kuandaa michuano hiyo baada ya Afrika Kusini iliyoandaa mwaka 2010.

Lakini mechi tatu za ufunguzi za michuano hiyo ya mwaka 2030 zitachezwa huko Amerika Kusini ikiwa ni sehemu maalum ya maadhimisho ya miaka 100 ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia.

Mechi hizo zitachezwa kwenye nchi za Uruguay, Argentina na Paraguay.

Michuano ya Kombe la Dunia ilianza mwaka 1930 nchini Uruguay na mwaka huu itakuwa imetimia miaka mia moja tangu kuanzishwa, na FIFA imepeleka sherehe hizo kufanyika kwenye nchi hizo ambazo awali nazo zilitangaza nia ya kuomba kuandaa michuano hiyo ya mwaka 2030.

FIFA imetoa nafasi kwa nchi za Bara la Asia na Ocenia kuomba kuandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2034 na tayari Saudia Arabia imeonesha nia hiyo.

Mechi ya ufunguzi kwenye michuano hiyo ya mwaka 2030 itachezwa kwenye jiji la Montevideo nchini Uruguay ambako kulichezwa mechi ya kwanza ya kombe la Dunia la mwaka 1930 na baadae kufuatiwa na michezo mingine miwili itayochezwa kwenye nchi za Argentina na Paraguay.

Baada ya hapo michuano hiyo itakayoshirikisha timu 48 itahamia kuchezwa kwenye Bara la Afrika na Ulaya kwenye nchi za Morocco, Ureno na Hispania.