‘kamchape’ yamsikitisha Chongolo

0
125

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo @daniel_godfrey_chongolo amewataka Wananchi wa mkoa wa Katavi kuachana na imani potofu za kishirikina maarufu kwa jina la ‘kamchape’ kwa kuwa zinafifisha juhudi za kupambana na umaskini.

Chongolo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wanachama wa CCM na Wananchi katika eneo la Ofisi Kuu ya CCM mkoa wa Katavi, Mpanda Mjini.

“Nimeambiwa huku kuna Kamchape, hawa jamaa mnawapa nguvu kubwa, mnawapa kichwa, mnawapa fursa ya kufanya mambo yanayokiuka sheria za nchi”. Amesema Chongolo na kuongeza kuwa

“Imani hizo za kuamini ushirikina ni umaskini na ukitaka kujifunza angalia watu wanaoamini katika ushirikina uone maisha yao. Wanaamini katika ndoto ambazo kutekelezeka kwake ni ngumu.”

Chongolo amesisitiza kuwa maendeleo hayapatikani kwa ndumba, kwa kupuliza, kwa kuagua, kupiga ramli na kutengeneza mambo rahisi bali maendeleo ni mambo yanayotaka kufuata utaratibu.

Katibu Mkuu huyo wa CCM Taifa yupo mkoani Katavi kwa ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, kuhamasisha uhai wa chama mkoani humo na kusikiliza kero za Wananchi.