Mafuta yazidi  kupanda bei

0

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta zilizoanza kutumika leo Jumatano Oktoba 04, 2023.

Petroli itauzwa hadi Tsh 3,281 ikiwa ni tofauti ya Tsh 68 mwezi Septemba, Diseli hadi kikomo cha Tsh 3,448 tofauti ya Tsh 189 mwezi uliopita na mafuta ya taa Tsh 2,943 kwa mkoa wa Dar es Salaam.

Kunguni waitesa Ufaransa, Serikali yatoa tamko

0

Wananchi wa Ufaransa pamoja na watalii wanaoitembelea nchi hiyo wanaugulia maumivu baada ya kungátwa na kunguni ambao wamesambaa katika maeneo mengi hasa ya umma.

Kufuatia kuwepo kwa picha mbalimbali za video mitandaoni zikionesha kuwepo kwa wadudu hao hasa katika jiji la Paris kwenye treni za mwendokasi, hospitali, nyumba za sinema na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Charles-de-Gaulle, Serikali ya Ufaransa imesema inaelekeza juhudi zake katika kupambana na kunguni hao.

“Jimbo linahitaji haraka kuweka mpango wa utekelezaji dhidi ya janga hili wakati Ufaransa inajiandaa kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki na Paralympic 2024,” ameandika Naibu Meya wa Paris, Emmanuel Gregoire katika barua yake kwa Waziri Mkuu Elisabeth Borne

‘kamchape’ yamsikitisha Chongolo

0

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo @daniel_godfrey_chongolo amewataka Wananchi wa mkoa wa Katavi kuachana na imani potofu za kishirikina maarufu kwa jina la ‘kamchape’ kwa kuwa zinafifisha juhudi za kupambana na umaskini.

Chongolo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wanachama wa CCM na Wananchi katika eneo la Ofisi Kuu ya CCM mkoa wa Katavi, Mpanda Mjini.

“Nimeambiwa huku kuna Kamchape, hawa jamaa mnawapa nguvu kubwa, mnawapa kichwa, mnawapa fursa ya kufanya mambo yanayokiuka sheria za nchi”. Amesema Chongolo na kuongeza kuwa

“Imani hizo za kuamini ushirikina ni umaskini na ukitaka kujifunza angalia watu wanaoamini katika ushirikina uone maisha yao. Wanaamini katika ndoto ambazo kutekelezeka kwake ni ngumu.”

Chongolo amesisitiza kuwa maendeleo hayapatikani kwa ndumba, kwa kupuliza, kwa kuagua, kupiga ramli na kutengeneza mambo rahisi bali maendeleo ni mambo yanayotaka kufuata utaratibu.

Katibu Mkuu huyo wa CCM Taifa yupo mkoani Katavi kwa ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, kuhamasisha uhai wa chama mkoani humo na kusikiliza kero za Wananchi.

Adha ya Wanafunzi kutembea umbali mrefu yatatuliwa

0

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga shule katika kila kijiji ili kuwapunguzia watoto adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule.

Dkt. Mollel ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo katika jimbo hilo ambapo pia amewataka Wananchi kumuunga mkono Rais Samia kwa kuhakikisha wanapeleka watoto shule ili kupata elimu.

“Mpaka sasa tumebaki na vijiji vichache sana ambavyo havijapata shule, ila naimani kubwa kwa dhamira ya kiongozi wetu Dkt. Samia kabla ya 2025 atakuwa ameweka mambo safi”. Ameeleza Dkt. Mollel

Aidha ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada zake kuhakikisha inapeleka maendeleo kwa Wananchi kwa kuboresha miundombinu ya barabara, upatikanaji wa maji na umeme.

Katika sekta ya afya Dkt. Mollel amesema kuwa upatikanaji wa dawa umeongezeka ambapo kwa kila watu 10 wanaotakiwa kupata dawa ni watatu tu ndio wanaokosa
tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Rais afanya uteuzi TANAPA

0

Musa Kuji ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habati na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu imeeleza kuwa kabla ya uteuzi huo Kuji alikuwa Naibu Kamishna wa Huduma wa Shirika hilo la TANAPA.

Uteuzi wa DED Korogwe watenguliwa

0

Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Halfan Magani, Mkurugenzi wa halmashauri ya Korogwe na badala yake amemteua Goodluck Mwangomango kushika nafasi hiyo.

Kabla ya uteuzi huo Mwangomango alikuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Singida.

Said Majaliwa yeye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tanga Mjini ambapo kabla alikuwa Mkurugenzi wa wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.

Faraja Msigwa ameteuliwa na Rais kuwa Mkurugenzi wa Kilindi mkoani Tanga ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Amemteua Naima Bakari Chondo kuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Singida Mjini kuchukua nafasi ya Goodluck Mwangomango ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa wilaya ya Korogwe.

Rais pia amemteua Shamim Adam Sadiq kuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Ruangwa na
Hamza Hussein Hamza kuwa Katibu Tawala wa wilaya ya Ngorongoro kuchukua nafasi ya Nyakia Chirukile ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga.

Kabla ya uteuzi huo Hamza alikuwa Afisa Tarafa wa Ndudu, wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Amemteua Lameck Ng’ang’a kuwa Katibu Tawala wilaya ya Karatu mkoani Arusha ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Tarafa Karatu na anachukua nafasi ya Msigwa aliyeteuliwa kuwa Mkurugenzi wa wilaya ya Kilindi.