Leseni 2411 za uchimbaji madini zimetolewa Geita

0

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema Mkoa huo umetoa leseni 2411 za uchimbaji madini ili kuongeza chachu katika uchimbaji madini na huku kipaumbele chao katika utoaji wa leseni hizo ni wachimbaji wadogo na wanawake.

Shigella ameyasema hayo wakati wa ufungaji wa maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita ambapo amesema bado wanaendelea kutoa leseni za uchimbaji madini na katika leseni hizo zilizotolewa, kuna kundi la wachimbaji wadogo wanawake 300 ambao wamepewa leseni.

Pia Shigella amesema wanaendelea kuandaa maonesho ya madini mkoani humo ili kuongeza juhudi za kuufanya Mkoa huo kuongoza kwa uchangiaji wa mapato Serikalini baada ya mkoa huo kushika nafasi ya 7 katika kuingiza mapato serikalini kwa mikoa yote Tanzania.

Ameongeza kuwa washiriki katika maonesho ya mwaka huu wameongezeka kutoka 250 kwa mwaka 2022 na kufikia 350 kwa mwaka 2023 kutoka mataifa 7 (Mwenyeji Tanzania, Kenya, Malawi, Burundi, China, India na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo).

Mitambo ya Madini yajengwa Dodoma, Mwanza, Geita

0

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema mitambo mitatu ya usafishaji wa madini ya dhahabu na fedha imejengwa katika Mikoa ya Dodoma, Mwanza na Geita. Ikiwa na uwezo wa kusafisha kilo 965 kwa siku.

Abdulla ameyasema hayo wakati wa ufungaji wa maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita.

“Mitambo hiyo itawezesha madini ya dhahabu na fedha kusafishwa kwa asilimia 99.99 na kupata thamani halisi ya madini. Jambo hili litawezesha nchi yetu kupitia Benki Kuu kuendelea kununua madini na kuyahifadhi ili kuimarisha shilingi yetu na uchumi wa Tanzania.” – amesema Abdulla.

Abdulla amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ufungaji wa maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita yaliyoanza Septemba 20, 2023 na kufungwa rasmi leo Septemba 30, 2023.

Wachimbaji madini wasisitizwa kutunza mazingira

0

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito kwa wachimbaji madini nchini kutunza mazingira wakiwa kwenye shughuli zao ili kutoathiri viumbe hai.

Abdulla ameyasema hayo wakati wa ufungaji wa maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita.

“Kama tunavyofahamu shughuli za madini ikiwemo uchimbaji na uchenjuaji zinaweza kuathiri mazingira. Natoa wito kwa wachimbaji wa madini hasa wachimbaji wadogo kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa na Serikali katika kuhakikisha shughuli za madini zinakwenda sambamba na utunzaji wa mazingira (miti, wanyama na vyanzo vya maji) ili kuwa na uchimbaji endelevu na salama kwa kizazi cha sasa na baadae.”‘-
Amesema Abdulla.

Hemed Abdulla : BOT endeleeni kununua dhahabu

0

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), kuendelea kununua dhahabu kwa lengo la kuiwezesha nchi kuwa na akiba ya dhahabu ya kutosha.

Abdulla ameyasema hayo wakati wa ufungaji wa maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita.

Mpaka sasa BoT imenunua kiasi cha kilogram 418 za dhahabu yenye kiwango cha asilimia 99.9. Na taarifa ya BOT iliyitolewa na Gavana wake ilieleza kuwa Benki Kuu itanunua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wa ndani na wafanyabiashara wa dhahabu kwa fedha za Kitanzania.

WATAALAMU WA TEHAMA JESHI LA POLISI WATHAMINIWE

0

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Jumanne Sagini amelishauri Jeshi la Polisi Tanzania kutambua ujuzi, weledi na uzalendo wa wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika jeshi hilo kwa kuwapandisha vyeo mara kwa mara bila ya kuwaondoa kwenye fani zao.

Amesema ipo haja ya Jeshi hilo kuonesha kuwathamini kwakuwa wamekubali kuendelea kulitumikia jeshi hilo bila ya kutamani kwenda kufanya kazi kwingine licha ya kuwa na ujuzi walionao.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa kifedha wa Jeshi la Polisi Tanzania ’URA Mobile’ iliyofanyika katika viwanja vya chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam kilichopo Kurasini Dar es Salaam, Sagini ameongeza kuwa kwa taaluma waliyoionesha wataalamu hao wanastahili kuthaminiwa.

“Ndio maana nikamuambia IGP kwenye zile promotion promotion zile hawa wawapeleke harakaharaka ili maslahi ambayo angayatafuta kule ayapate huku.

Tabu yenu mkimpandisha akapanda sana mtamtoa IT mnamwambia simamia kamisheni, huyu mpandisheni alafu abaki palepale ilitaaluma yake na uwezo wake tuendelee kunufaika nao. Kuna dhambi gani mtu anafanya wonders mnampandisha anakuwa na licheo likubwa limshahara likubwa alfu anafanya kazi yake ileile ya taaluma maana huko nako tunawahitaji” Amesema Sagini

Bashungwa amvaa Mkandarasi Barabara ya Mzunguko

0

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mkandarasi Avic anayejenga barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma, yenye urefu wa Kilometa 112.3 sehemu ya Ihumwa Dry Port – Matumbulu – Nala (km 60), kuhakikisha anakamilisha barabara hiyo ifikapo mwezi Desemba, 2024.

Bashungwa ametoa agizo hilo Septemba 29, 2023, jijini Dodoma wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amemsisitiza mkandarasi huyo kuongeza kasi kwenye ujenzi wa madaraja mawili ambayo yanaonekana kuchelewa ujenzi wake.

“Sipepesi macho kwenye usimamizi wa mikataba, kufanya kazi kwa ubora na kasi ndio kipimo chako, ukizembea kwenye kazi hii usahau kupewa kazi nyingine za ujenzi kwenye Sekta hii nchini”, -amesema Bashungwa.

Ameahidi kutembelea tena mradi huo ifikapo Desemba mwaka huu ili kuona uetekelezaji wa maagizo yake na kumsisitiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana ili uweze kukamilika kwa wakati kulingana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Bashungwa ameuagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kushirikiana na Shirika la Reli (TRC), kurudisha haraka mawasiliano ya barabara ya lami eneo la Mkonze na Nala ambalo lilibomolewa kwa ajili ya ujenzi wa reli ya SGR kwani wananchi wamekuwa wakipata kero kutokana na changamoto katika maeneo hayo.

Bashungwa amewataka wakandarasi nchini wanaotekeleza miradi ya ujenzi kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo kwa mujibu wa Mkataba na kusisitiza kutokuwa na huruma kwa yeyote atakayekiuka mikataba hiyo.

Bashungwa amemuagiza Mhandisi Mshauri Mzawa wa kampuni ya Inter-Consult kumsimamia mkandarasi wa kampuni ya China Civil Engineering Corporation (CCEC) anayetekeleza sehemu ya Nala – Veyula – Mtumba (km 52.3), kutoa vifaa vya usalama kwa wafanyakazi wake ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea maeneo ya kazi.

Katika hatua nyingine, Bashungwa amewaagiza Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini kuhakikisha wanazibua mifereji ya barabara zilizo chini ya Wakala huyo kabla ya mvua hazijaanza ili zisiwe chanzo cha kuleta mafuriko, sambamba na hilo Waziri huyo amempongeza Meneja wa TANRODS Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanya matengenezo na kuzibua barabara na mifereji katika mkoa huo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta ameeleza kuwa mpaka sasa sehemu ya mradi kutoka Nala – Veyula – Mtumba (km 52.3) umefikia asilimia 54.3 na sehemu inayoanzia Ihumwa Dry Port – Matumbulu – Nala umefika asilimia 50 na sasa wakandarasi wanaendelea na kazi mbalimbali za ujenzi wa makalavati na madaraja makubwa mawili.

Mradi wa Barabara ya Mzunguko wa nje ya Dodoma (Km 112.3), unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi Bilioni 221 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2024.

Waziri Mkuu : Tushirikiane kupambana na dawa za kulevya

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imekuwa ikifanikiwa katika kampeni zake mbalimbali za hamasa kwa jamii kutokana na nguvu pamoja na sauti ya Viongozi wa dini.

Waziri Mkuu amesema hayo katika Baraza la Maulid lililofanyika kitaifa mkoani Dodoma ambapo amesema hiyo ni kutokana na Viongozi wa dini kutimiza majukumu yao katika mafundisho ya kiroho kwa Waumini wao na hivyo imewarahishia Viongozi wa Serikali kutimizia majukumu yao kwa weledi katika kuleta maendeleo.

“Suala ambalo ningependa kusisitiza ni ushiriki wa madhehebu ya dini katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwani kwa sasa limekuwa tatizo kubwa na hasa matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya Duniani limekuwa kubwa, na Taifa letu pia linapitiwa na wimbi hili”. amesema Waziri Mkuu.

Amesema zamani ilizoeleka matumizi ya dawa za kulevya ni mijini lakini kwa sasa matumizi ya dawa za kulevya yanawafikia hadi Wananchi wa vijijini hasa vijana ambao ndio nguvu kazi kubwa ya Taifa.

“Lakini pia hata baadhi ya watoto wetu wapo hatarini zaidi katika kutumbukia kwenye janga hili kutokana na ushawishi wa rika na uwezo mdogo katika maamuzi yao”. ameongeza Waziri Mkuu.

Amewasihi Viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kukabiliana na matatizo ya kupoteza nguvu kazi.

Bakwata : Tunamuunga Mkono Rais Samia

0

Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) limesema linamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake yote na kuwaombea Dua ili waweze kuwa na ufanisi zaidi.

Akisoma Salamu za BAKWATA katika Baraza la Maulid Kitaifa mkoani Dodoma
Katibu Mkuu wa BAKWATA Alhaj Nuhu Mruma amesema, sababu za wao kuiunga mkono Serikali ni kutokana na juhudi kubwa inazofanya katika kuwaletea Wananchi maendeleo kwenye sekta za kiuchumi, kisiasa na kijamii pamoja na kuboresha mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

“Mheshimiwa mgeni rasmi ni hivi karibuni katika kujenga demokrasia nchini, aliunda kikosi kazi maalum kilichoshughulikia masuala ya demokrasia nchini na hatimaye kuyakubali maoni mengi yaliyopendekezwa na kikosi kazi hicho na mengine yameanza kufanyiwa kazi ikiwemo ruhusa ya vyama vya siasa kufanya mikutano yao ya hadhara”. amesema Mruma

Amesema jukumu lao Viongozi wa dini ni kuendelea kuishauri Serikali, kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mambo mbalimbali na kuiombea amani nchi pamoja na kuwaombea viongozi wake.