Rais Samia Suluhu Hassan ameteua na kufanya mabadiliko ya uteuzi kwa wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala na Kaimu Kamishna Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Kwa Wakuu wa wilaya amemhamisha kituo cha kazi Sixtus Mapunda kutoka wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa kuwa mkuu wa wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Mapunda anachukua nafasi ya Mobhare Matinyi ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Amemhamisha kituo cha kazi mkuu wa wilaya ya Urambo mkoani Tabora Kenan Kihongosi kwenda kuwa mkuu wa wilaya ya Momba mkoani Songwe.
Kihongosi anachukua nafasi ya Fakii Raphael Lulandala ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Elibariki Bajuta, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Urambo mkoani Tabora kuchukua nafasi ya Kenan Kihongosi aliyehamishiwa Momba.
Rais Samia pia amemteua William Mwakilema, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuwa mkuu wa wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga kuchukua nafasi ya Jokate Mwegelo ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Nyakia Ally Chirukile ameteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Sumbawanga ambapo anachukua nafasi ya Sixtus Mapunda aliyehamishiwa Temeke.
Kabla ya uteuzi huo Nyakia alikuwa Katibu Tawala wa Ngorongoro.