VIONGOZI AFRIKA WAWEZESHANE, WASISHINDANE

0

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema
kwa sasa dunia inazungumza lugha moja kuhusu usalama wa Chakula ambapo inakadiriwa siku zijazo idadi ya watu duniani itafikia Bilioni 9 japo inakabiliwa na changamoto za kimazingira.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 Waziri Bashe amesema Afrika ni Bara dogo lenye watu wenye umri wa wastani wa miaka 28 huku likiwa na zaidi ya ardhi asilimia 65 ambayo bado haijatumika, hivyo ipo haja ya viongozi wa Afrika kuwezeshana ili kuyakabili mambo yote hayo.

Amesema hatma ya maendeleo stahimilivu duniani itapatikana ikiwa tu Bara la Afrika na viongozi wake wataweka jitihada kubwa katika kutambua jitihada za wenzao na kuwezeshana badala ya kushindana ili kufikia lengo la kuzitumia kikamilifu rasilimali zilizopo katika maeneo yao.

Tuhuma zamtupa Antony nje ya kikosi cha Brazil

0

Mshambuliaji wa Manchester United, Anthony amekanusha tuhuma zinazomkabili za kumshambulia aliyekuwa mpenzi wake, Gabriela Cavallin, baada ya habari mpya kuchapishwa na vyombo vya habari nchini Brazil.

“Ninaweza kuthibitisha pasi na shaka kuwa tuhuma hizi ni za uongo,” amesema Antony ambaye ameachwa nje ya kikosi cha Brazil kufuatia tuhuma hizo.

Amesema kuwa anaamini uchunguzi wa polisi unaoendelea utaweka bayana ukweli utakaothibitisha kuwa hana hatia.

Antony ameachwa nje ya kikosi hicho kinachoshiriki michezo ya kuwania kufuzu kombe la dunia mwaka 2026 dhidi ya Bolivia na Peru, ambapo nafasi yake imechukuliwa na Gabriel Jesus.

Jeshi la Polisi nchini Uingereza limesema kuwa lina taarifa za tuhuma hizo na kwamba kwa sasa uchunguzi unaendelea kubaini ukweli wote.

Biteko : Nataka umeme uwafikie wote

0

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishat Dkt. Doto Biteko pamoja na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga wamepokelewa rasmi na Menejimenti na Watumishi wa wizara ya Nishati katika Ofisi za wizara hiyo zilizopo jijini Dodoma, baada ya kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa hizo.

Dkt. Biteko amesema kazi iliyo mbele ni kuhakikisha huduma ya nishati inawafikia Wananchi wote na kwamba pamoja kazi nzuri iliyofanyika ya kuimarisha sekta ya Nishati, bado kuna nafasi ya kufanya kazi hiyo vizuri zaidi ili nishati ya uhakika ipatikane.

“Kama watu hawapati umeme, kama watu hawapati nishati wanayoihitaji, hata tukivaa suti za namna gani tunakuwa hatuna maana na tutakuwa tunasemwa kila siku, kiu yangu ni kuona tunafanya kazi kwa viwango ili huduma ya nishati iwafikie wananchi wote.”amesisitiza Dkt. Biteko

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyompatia ili kuweza kuhudumia sekta ya nishati kama Mbunge aliyetoka katika kundi la vijana na ameahidi uchapakazi, weledi na ufanisi katika kazi zake.

JITIHADA ZA TANZANIA KUBORESHA MIFUMO YA CHAKULA

0

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametaja namna Tanzania imedhamiria kufikia lengo namba mbili la umoja wa mataifa (SDG2) linalohusu kuufikia ulimwengu usio na njaa mwaka 2030.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika unaofanyika mkoani Dar es Salaam Dkt. Mpango amesema mkutano huo utainufaisha Tanzania kuimarifa mifumo ya chakula kwa kuwekeza zaidi kwenye rasilimali ardhi na nguvu kazi ya Wanawake barani Afrika.

Amesema Tanzania inajivunia jitihada za maboresho ya mifumo ya chakula na imejitoa kushirikiana na wengine ambapo lengo kuu ni kuwa na ulimwengu usio na njaa ifikapo mwaka 2030.

Akitoa mifano ya namna Tanzania imeweka jitihada kwenye suala hilo Dkt. Mpango amesema, hivi sasa kilimo hapa nchini kinatambulika kama chanzo kikuu cha ukuaji wa uchumi ambapo kimetoa ajira kwa zaidi ya asilimia 65 ya Wananchi huku kikichangia katika pato la Taifa kwa asilimia 27 Tanzania Bara na asilimia 21 kwa Zanzibar.

Amesema sekta ya kilimo inachangia katika usafirishaji wa bidhaa zake nje ya nchi [export] kwa zaidi ya asilimia 30 na kuzalisha asilimia 65 za malighafi kwa ajili ya viwanda vya Tanzania.

Naibu Spika “Mmejiongezea mzigo ‘for nothing’”

0

Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu ameishauri wizara ya Maji kuboresha mchakato wa umiliki wa visima kwa kuwarudishia Wananchi visima walivyovichukua, ili huduma ya maji iendelee kupatikana.

“Hivi visima toka mchukue mmefanya tathimini ya ufanisi wake?. Visima vyote vya Wananchi ambavyo DAWASA mmevichukua vimekufa… mnawapa tabu Wananchi, mmejiongezea mzigo for nothing. Tunaomba mfikirie upya namna ya kurudisha visima kwa Wananchi vifanye kazi.” Ameshauri Naibu Spika Zungu

Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma baada ya Mbunge wa jimbo la Temeke mkoani Dar es Salaam, Dorothy Kilave kuhoji kwanini Serikali isiwarudishie Wananchi visima maana tangu vimechukuliwa hakuna marekebisho na Wananchi wanaendelea kukosa maji.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema, visima hivyo vilichukuliwa kwa sababu za kiufundi na havitarudishwa kwa Wananchi.

“Visima vimechukuliwa kwa sababu za kiufundi, sasa hivi kwa mfano wizara ya Afya inaweza kumiliki hosipitali zake na sisi wizara ya Maji tunahitaji kumiliki vyanzo hivi vya maji vyote ili viwe chini ya uangalizi wa watalaam wetu, hatutavirudisha kwa Wananchi bali tutaongeza nguvu ili kuhakikisha vinakwenda kutumika na kuongeza usambazaji wa maji kwa Wananchi.” Amesema Naibu Waziri Maryprisca Mahundi

BAJETI BIL 125, NITAWAWEZESHA MSIMAMIE UCHAGUZI

0

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imepeleka fedha nyingi Jeshi la Polisi ili kulisaidia liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo hasa wakati wa uchaguzi.

Amesema kwa mwaka 2024 kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo amelitaka Jeshi hilo liwe makini zaidi katika maeneo yote ya nchi likisimamia haki itendeke na usalama uwepo katika uchaguzi huo pamoja na ule wa mwaka 2025.

Rais Samia ameongeza kuwa amekwishazungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Camillus Wambura kuwa atashughulikia changamoto za Jeshi hilo na amekwishapokea bajeti ya shilingi Bilioni 125.

Ameongeza kuwa atahakikisha anaipata bajeti kamili ili changamoto zote za Jeshi hilo zitatuliwe na liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.

“Kwa hiyo bajeti nitaenda kuihangaikia niipate ili niwawezeshe msimame vema na mkasimamie vema chaguzi zetu.” Amesema Rais Samia

Alikuwa akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi.

IGP KAZA BUTI JESHI LINYOOKE

0

Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Camillus Wambura kusaidia Jeshi hilo kubadilika kwa kuwa na maadili yanayotakiwa, na kuongeza kuwa amefarijika kuona mabadiliko yameanza kuonekana.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa Maafisa wa Jeshi la Polisi unaofanyika mkoani Dar es Salaam Rais Samia amesema, zipo dalili njema kuwa jeshi hilo limeanza kubadilika kwa kuwa mabadiliko hayo yameanza kuonekana kuanzia juu kwa viongozi wa jeshi hilo.

Amesema iwapo Makamishna na Wakuu wa majeshi wamebadilika, hivyo hivyo walio chini yao watabadilika, japokuwa motisha za kupandisha vyeo na mambo mengine ya kuinua ari ya kufanya kazi yamechangia kuleta maboresho hayo.

“Bado wapo wanaokiuka maadili….bado. Kuna cases [kesi] tunazipokea kuna nyingine clips mtu akipotoka huko unarushiwa muone polisi wako huyo,” amesema Rais Samia na kuongeza kuwa

“Kwa hiyo bado kazi ipo nataka nikiri kwamba mabadiliko hayafanyiki kwa ghafla, tutaanza hatua kwa hatua.
Hatua imeonekana na kidogo kidogo mabadiliko yataendelea kuwepo jinsi ambavyo wanapelekwa kwenye mafunzo ya maadili na kujua wajibu wao ndivyo watakavyoweza kubadilika.” Amesema Rais Samia