Waajiri watakiwa kuzingatia usalama na afya mahali pa kazi

0

Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) imetakiwa kuhakikisha inaendelea kusimamia usalama na afya sehemu za kazi ili kuimarisha utendaji na afya kwa Wafanyakazi

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti leo mkoani Arusha.

Prof. Ndalichako amesema masuala ya usalama na afya ni mtambuka na yanagusa sekta zote za uchumi, hivyo ni vyema kushirikiana ili kuimarisha mifumo ya usimamizi wa usalama na afya kwa wafanyakazi nchini.

Akizungumza awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru kamati hiyo kwa kuishauri vyema serikali kuhusu masuala ya usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi na amewahakikishia ofisi hiyo itaendelea kusimamia kwa ufanisi masuala hayo.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda amesema taasisi hiyo itahakikisha ustawi wafanyakazi unaimarika sambamba na kulinda uwekezaji kupitia mifumo ya usalama na afya sehemu za kazi

Lissu na wenzake mbaroni

0

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kukamatwa kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu na wenzake watatu kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko isiyo halali na kuzuia askari kutekeleza majukumu yao.

Kamanda Masejo amesema baada ya mahojiano hayo na ukamilishwaji wa taratibu zingine, hatua nyingine za kisheria zitafuata.

FAO yaahidi kuendeleza sekta za mifugo, uvuvi

0

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza sekta za Mifugo, Uvuvi na Kilimo hususani kuwawezesha Wanawake kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali katika sekta hizo.

Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi na Mwakilishi wa FAO upande wa Afrika, Abebe Haule-Gabriel wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

“Naomba kutumia fursa hii kukueleza kuwa FAO tumekuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania na tutaendelea kushirikiana katika kuendeleza sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuendelea kuwainua Wanawake na Vijana wanaoshiriki katika sekta hizo,” amesema Abebe.

Kwa upande wake Waziri Ulega ameishukuru FAO kwa ushirikiano wa kifedha na kitaalam inaoutoa kwaTanzania katika miradi mbalimbali inayolenga kusimamia na kuendeleza rasilimali ya uvuvi hususani utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa Uvuvi Mdogo, Mpango Kabambe wa sekta ya Uvuvi na kuwawezesha Wanawake katika sekta ya uvuvi.

Mabadiliko ya tabianchi kuathiri zaidi vichanga

0

Wawakilishi kutoka Jumuiya ya Upumuaji ya Ulaya wametoa wito kwa Umoja wa Ulaya (EU) kupunguza viwango vya uchafuzi wa hewa, kwani vilivyopo vinahatarisha maisha ya watoto wachanga, wenye pumu na wenye magonjwa sugu ya mapafu.

Vichanga huathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa hali ya hewa kwa kuwa mapafu yao yako kwenye hatua ya ukuaji na wao hupumua haraka na kuvuta hewa hadi mara tatu zaidi kuliko watu wazima wawapo nje.

Makundi mengine yaliyo hatarini ni pamoja na wagonjwa wa magonjwa sugu, wazee, Wajawazito na watu wanaofanya kazi za nje mfano za ujenzi.

Ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha kuwa hatua nyingi za kupunguza utoaji wa gesi chafuzi zinaweza kuwa chanzo cha hewa safi na kupunguza hatari za kiafya kwa makundi mbalimbali.

Waliofariki kwenye tetemeko ni zaidi ya 2000

0

Zaidi ya watu 2,000 wamethibitika kufariki dunia na maelfu kujeruhiwa nchini Morocco kufuatia tetemeko kubwa la ardhi kuyakumba maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Habari zaidi kutoka nchini Morocco zinaeleza kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwa kuwa bado kuna idadi kubwa ya watu wamenasa kwenye vifusi huku zoezi la uokoaji likiendelea.

Kufuatia tetemeko hilo, Mfalme Mohammed VI wa Morocco ameagiza Jeshi la nchi hiyo kufanya kazi ya kuwaokoa watu waliokumbwa na tetemeko hilo na ametaka kazi hiyo ifanyike kwa kutumia helikopta pamoja na ndege zisizo na rubani.

Tetemeko hilo kubwa la ardhi lililoikumba Morocco limeharibu makazi ya maelfu ya raia wa nchi hiyo na miundombinu huku ikielezwa kuwa jiji maarufu la kibiashara la Marrakesh nalo limeharibiwa vibaya.

Uvuvi wa Bahari Kuu kuipatia Tanzania Dola milioni 2.1

0

Tanzania Bara na Zanzibar zinatarajia kukusanya takribani Dola Milioni 2.1 kupitia mauzo ya leseni 45 za uvuvi wa bahari kuu zilizonunuliwa na wawekezaji kutoka China na Hispania.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mikataba ya mauzo ya leseni hizo iliyofanyika jijini Dar-es-Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema eneo la bahari kuu upande wa Tanzania Bara na Zanzibar lina ukubwa wa takribani kilomita za mraba 220,000, ambazo kwa muda mrefu hazijatumika ipasavyo.

Waziri Ulega amebainisha kuwa eneo la bahari linalomilikiwa na Tanzania bara na Zanzibar lina uwezo wa kuhimili meli za uvuvi mpaka 100, na hivyo amewaomba wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu kufanya hivyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi kutoka Zanzibar, Suleiman Makame, amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Wizara yake, kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA), itasimamia na kutekeleza vipengele vyote vilivyopo kwenye leseni hizo.

Prof. Jay Amtembelea Mzee Kikwete

0

Mwanamuziki nguli nchini, Joseph Haule (Prof. Jay), amemtembelea Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, nyumbani kwake mkoani Dar es Salaam.

Kwenye ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Mzee Kikwete ameandika, “Leo nimetembelewa na Profesa J nyumbani kwangu Kawe. Ni furaha kubwa kuona afya yake imeimarika. Hakika Mwenyezi Mungu ni mkuu.”