Idadi ya vifo yazidi kuongezeka nchini Morocco

0

Kufuatia tetemeko la ardhi nchini Morocco, idadi ya watu wanaokadiriwa kufariki dunia katika tetemeko hilo inakadiriwa kufika watu 2,900.

Wale walionusurika wamejiunga na timu ya uokozi ili kuendeleza juhudi za kuwatafuta manusura wengine. Vikosi vya uokoaji vimeendelea kufanya kazi ya uokozi bila kuchoka, hata usiku kucha.

Ni muhimu kukumbuka kwamba hili ni tukio baya zaidi kuwahi kuikumba nchi ya Morocco, Kaskazini mwa Afrika, tangu tetemeko la ardhi la mwaka 1960 lililoharibu mji wa Agadir na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Tanzania na Indonesia kukuza ushirikiano wa kibiashara

0

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji, amekutana na kufanya mazungumzo kuhusu kuendeleza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Indonesia na Balozi wa Indonesia nchini, Tri Yogo Jatmiko, katika Ofisi ndogo za Wizara hiyo jijini Dar es Salaam.

Waziri Kijaji amemhakikishia Balozi huyo kuwa Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo na iko tayari kuwezesha miradi ya uwekezaji hususani katika sekta ya kilimo, hasa katika uongezaji wa thamani katika mazao ambayo nchi hiyo imepanga kuyaendeleza, kama vile karafuu, ili kuongeza ajira na kipato kwa Watanzania.

Rais Samia asema katiba mpya si mali ya wanasiasa

0

Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa mchakato wa katiba mpya ni wa Watanzania wote na sio wa wanasiasa kama ambavyo baadhi ya watu wanadhani, na kwamba uandaaji wake unahitaji muda wa kutosha na ushiriki wa makundi yote.

Rais Samia ametoa rai hiyo wakati akifungua mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa na Wadau wa Demokrasia Kutathmini Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Hali ya Siasa Nchini unaofanyika kwa siku tatu kuanzia leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Katiba si mali ya vyama vya siasa. Katiba ni mali ya Watanzania, awe na chama au hana. Hivyo, matengenezo yake yanahitaji tafakuri sana,” amesema Rais Samia.

Ameeleza kuwa bado Watanzania wengi hawaifahamu katiba ya sasa, wengine wakidhani ilani ya CCM ndio katiba, na kwamba Serikali inatekeleza mchakato wa kutoa elimu kwa umma ili waifahamu katiba ya sasa, waweze kutoa maoni sahihi pindi watakapotakiwa kufanya hivyo.

Wakati huo huo, amesisitiza kwamba ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa iliyotolewa sio tiketi ya kuvunja sheria za nchi kama ambavyo inafanyika sasa na baadhi ya vyama.

Hata hivyo Rais Samia ameongeza kuwa hashangazwi na hilo kutokea kwa sababu baadhi ya vyama havina ajenda ya kueleza Wananchi.

“Tulianza, ooh na katiba, tukaenda ikakatika katikati, bandari, sasa imekatika tumerudi tena katiba,” ameeleza Rais Samia akitolea mfano namna baadhi ya vyama vinavyoruka kutoka ajenda moja kwenda nyingine.

Ametahadharisha kuwa, hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria, na kwamba yeyote atakayekiuka sheria atachukuliwa hatua bila muhali, huku akiongeza kuwa Watanzania wote ni sawa, na kwamba hakuna Mtanzania bora zaidi ya mwingine.

Awali akizungumza kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) Profesa Ibrahim Lipumba alimpongeza Rais Samia kwa hatua za kuimarisha demokrasia anazochukua huku akipendekeza maeneo manne kufanyiwa maboresho kwenye katiba ya sasa kabla ya chaguzi za mwaka 2024 na mwaka 2025.

Ni kweli Jumatatu ni siku isiyopendwa?

0

Kumekua na mtazamo tofauti tofauti kuwa siku ya Jumatatu sio siku ya furaha kwa wengi hasa muda wa asubuhi.

Na hii ni kutokana na watu wengi kutoka kwenye siku za mwisho wa Juma na kutakiwa kwenda kwenye majukumu yao mengine ya siku ya Jumatatu asubuhi.

Jumatatu ni siku ya kwanza ya wiki na ni ishara ya mwanzo wa kazi kwa wiki nzima na hii sio kwa Wafanyakazi tu bali pia hata Wanafunzi Jumatatu kwao ni siku isiyofurahiwa kwani masomo pia huanza siku hiyo.

Zipo sababu mbalimbali zinazoelezwa kusababisha watu kutoipenda siku ya Jumatatu, kama vile;

  1. Kurudi kazini baada ya siku mbili za mapumziko na kufurahi
  2. Mahusiano kazini baina ya Wafanyakazi kama hayako sawa
  3. Kutokuwa tayari kwa ajili ya Jumatatu kutokana na uchovu wa mwisho wa wiki
  4. Kichwa kujawa bado na fikra za vitu vilivyofanyika mwisho wa Juma.
  5. Kuwepo kwa kazi ngumu katikati ya wiki.

Je,, Una mtazamo gani kuhusu siku ya Jumatatu?.

Lipumba : Uchaguzi wa Rais upingwe mahakamani

0

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Profesa Ibrahim Lipumba amewasilisha mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan maeneo manne ya kipaumbele ambayo ni muhimu yakafanyiwa maboresho kwenye Katiba ya sasa kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) amesema ni muhimu maeneo hayo yakafanyiwa maboresho kwa sababu ni wazi kuwa katiba mpya haiwezi kupatikana kabla ya mwaka 2025.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni moja, kuwezesha upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi kwa kurekebisha ibara ya 74 na kwamba tume hiyo isimamie chaguzi zote, tofauti na sasa ambapo uchaguzi wa Serikali ya Mitaa unasimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala.za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Eneo la pili ni katiba iruhusu mgombea binafsi kwa kufanyia maboresho ibara ya 39(2) na 67(1).

Aidha, eneo la tatu ni kufanyia maboresho ibara ya 41(6) ili itamke kuwa mshindi wa nafasi ya Urais atatangazwa endapo tu atapata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali.

Matokeo ya uchaguzi wa Rais kupingwa mahakamani ni eneo la nne ambalo TCD inapendekeza liwepo kwa kurekebisha ibara 41(7) ya katiba ya sasa.

Profesa Lipumba amesema kuwa maboresho hayo yakifanyika yatawezesha kuondoa kasoro nyingi ambazo hulalamikiwa wakati wa uchaguzi.

Waajiri watakiwa kuzingatia usalama na afya mahali pa kazi

0

Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), wametakiwa kuhahakisha wanasimamia usalama na afya sehemu za kazi ili kuimarisha utendaji na afya kwa Wafanyakazi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti yaliyofanyika mkoani Arusha.

Prof. Ndalichako amesema masuala ya usalama na afya ni mtambuka na yanagusa sekta zote za uchumi, hivyo ni vyema kushirikiana ili kuimarisha mifumo ya usimamizi wa usalama na afya kwa wafanyakazi nchini.

Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja ameishukuru kamati hiyo kwa kuishauri vyema serikali kuhusu masuala ya usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi na amewahakikishia ofisi hiyo itaendelea kusimamia kwa ufanisi masuala hayo.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda amesema taasisi hiyo itahakikisha ustawi wafanyakazi unaimarika sambamba na kulinda uwekezaji kupitia mifumo ya usalama na afya sehemu za kazi.