Nyongo: Toeni taarifa mkikutana na dawa ambazo si salama

0

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Stanslaus Nyongo, ametoa wito kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) kuendeleza ufanisi wao katika kuchunguza ubora na usalama wa dawa na vifaa tiba ili kulinda afya za Watanzania.

Nyongo alitoa wito huo wakati wa ziara ya kamati yake kwenye Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba kwa lengo la kutathmini shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo katika kulinda afya za Watanzania.

Aidha, Nyongo aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo husika, ikiwa ni pamoja na TMDA kupitia 15200# na kuchagua namba 2, wanapokutana na dawa ambazo si salama na zinaweza kuleta madhara katika jamii. Hii ni ili kushughulikia changamoto hiyo kwa haraka.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, aliwapongeza watumishi wa TMDA kwa juhudi zao kubwa katika utendaji wao unaosaidia kuhakikisha usalama wa wananchi kupitia dawa, vifaa tiba, na vitendanishi.

Mtoto wa Tembo aokolewa kutoka shimoni

0

Askari wa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) wamefanikiwa kuokoa mtoto wa tembo mwenye umri wa takribani wiki nne aliyekuwa amezama katika shimo lenye matope katika Kijiji cha Kwamsanja, kilichopo kata ya Kibindu, Halmashauri ya Chalinze, karibu na Pori la Akiba la Wamimbiki.

Taarifa za mtoto huyo wa tembo aliyetelekezwa na kundi lake na kuangukia shimoni zilitolewa na raia mwema aitwaye Manase Thomas Baha, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kwamsanja. Taarifa hizo zilimfanya Kamanda wa Pori la Akiba la Wamimbiki, Emmanuel Lalashe, kutuma timu ya askari wanne (4) kushirikiana na askari wa Jeshi la Akiba (migambo) sita (6) kwa ajili ya zoezi zima la kuokoa mtoto huyo wa tembo.

Akizungumza baada ya zoezi la uokoaji, Kamanda Lalashe aliwashukuru wananchi wanaoishi karibu na Hifadhi ya Wamimbiki kwa ushirikiano wao katika kulinda rasilimali za nchi, hasa rasilimali za wanyamapori katika hifadhi hiyo. Rasilimali hizi za wanyamapori ni muhimu kwa shughuli za utalii na pato la taifa.

Tumieni mkutano wa dunia wa ufugaji nyuki 2027 kuvutia wawekezaji

0

Wadau wa ufugaji nyuki nchini wametakiwa kutumia fursa ya mkutano wa Dunia wa Ufugaji Nyuki (APIMONDIA) utakaofanyika nchini 2027, kuvutia wawekezaji na kuongeza tija katika ufugaji na biashara nzima ya mazao ya nyuki na utalii.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki katika mkutano na vyombo vya habari uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam .

“Tumieni mkutano huu vizuri kwa kuongeza tija katika ufugaji na biashara nzima ya mazao ya nyuki, kuongeza wigo wa mashirikiano na taasisi mbalimbali duniani katika kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo pamoja na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za ufugaji nyuki hususani teknolojia na mbinu mbalimbali za kuboresha na kuendeleza sekta hii “- amesema Kairuki.

Ametoa wito kwa watanzania na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta hiyo kwa kuwa kwa sasa uzalishaji wa asali ni tani takribani elfu 32 tu wakati kama taifa kuna uwezo wa laki 138.

APIMONDIA ni Shirikisho la Umoja wa Vyama vya Wafugaji nyuki Duniani lililoanzishwa mwaka 1895 nchini Italia. Tanzania ilijiunga katika shirikisho hilo mwaka 1984 ambapo Tanzania kwa mwaka huu iliibuka kuwa mshindi wa kinyanganyiro cha kuandaa Mkutano wa 50 mwaka 2027.

Umoja wa Mataifa wataka kuimarishwa demokrasia Afrika

0

Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk ametoa wito wa kurejeshwa haraka utawala wa kirai kwenye mataifa ya Afrika yalioshuhudia mapinduzi ya kijeshi.

Volker Turk amesema mwenendo wa kuchukua madaraka kwa nguvu sio suluhu kwa matatizo yaliyopo.

Pia, amesema njia pekee ya kuyashughulikia matatizo ni kuwa na utawala wa kiraia unaotoa nafasi kwa umma kuwa huru kuikosoa serikali na kushinikiza mageuzi.

Aidha, amezungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa huduma muhimu, ndiyo yanachangia hali ya kukata tamaa miongoni mwa raia duniani na kuchochea hisia za itikadi kali.

Pia, Volker Turk aliongezea baadhi ya changamoto zinazoikumba dunia ni kama vile ukosefu wa usalama nchini Haiti na ukandamizaji wa makundi ya walio wachache ulimwenguni.

Darasa la saba kuanza mitihani kesho

0

Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza kuanza kwa mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi itakayofanyika Septemba 13 na 14 mwaka huu, ambapo wanafunzi 1,397,370 wanatarajiwa kufanya mitihani hiyo, ikiwa na ongezeko la watahiniwa 13,000, sawa na asilimia 0.93 ikilinganishwa na mwaka jana.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Said Mohammed, amewataka watahiniwa kuwa waadilifu na kuacha vitendo vya ulaghai. Pia, ametoa wito kwa Watanzania kutoa taarifa pindi wanapobaini vitendo vyovyote vya ulaghai juu ya mitihani hiyo.

Katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, jumla ya masomo sita yatatahiniwa, ambayo ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, pamoja na Uraia na Maadili.

Rais Samia ateuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya GCA

0

Rais Samia Suluhu Hassan ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (Advisory Board of the Global Centre on Adaptation – GCA).

Taarifa ya uteuzi huo iliyowasilishwa na Ban Ki-moon, Mwenyekiti wa Bodi ya GCA na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, ilitangazwa wakati wa mkutano kando ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Nairobi, Kenya.

Uteuzi huo ni utambuzi wa wazi wa uongozi imara wa Rais Samia katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi siyo tu katika eneo la Afrika bali pia kimataifa. Tanzania imekuwa ikiongoza katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi barani Afrika.

Mbali na Rais Samia, wajumbe wengine wa Bodi hiyo ni Rais wa Senegal, Macky Sall, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinumwi Adesina, na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva.

Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCA) ni taasisi kubwa kabisa duniani inayojikita katika kusimamia masuala ya uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi. Mpaka sasa, GCA imeweza kufanikisha upatikanaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 50, na Tanzania iko mstari wa mbele kupokea faida za fedha hizo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Bodaboda afariki kwa kugongwa na mwendokasi

0

Dereva wa bodaboda amefariki dunia baada ya kugongwa na basi la Mwendokasi kwenye mataa ya kuelekea Lumumba, katikati ya kituo cha Fire na DIT jijini Dar es Salaam.

Polisi wamethibitisha kifo cha dereva huyo ambaye imeelezwa aliingia kwenye barabara maalum ya mabasi hayo ya bila kuwa na tahadhari.

Watoto 400,000 kupewa chanjo ya Polio Songwe

0

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amebainisha kuwa zaidi ya watoto laki nne wanatarajiwa kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio katika Mkoa wa Songwe.

Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akianza ziara yake ya kukagua huduma zinazotolewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ambapo ameanza kutembelea Hospitali ya Wilaya hiyo, Zahanati ya Mbala, pamoja na Kituo cha Afya Mbuyuni kilichopo katika Wilaya hiyo.

“Baada ya kupatikana kwa mtoto mmoja mwenye ugonjwa wa Polio, tumeamua kutoa chanjo ya ugonjwa huo ambapo kwa Mkoa wa Songwe tunatarajia kuchanja watoto takribani laki nne ambao wana umri chini ya miaka nane,” amesema Waziri Ummy.

Amesisitiza kuwa, mwaka 2015 Shirika la Afya Duniani (WHO) liliitangaza Tanzania kuwa ni nchi ambayo imetokomeza ugonjwa wa Polio. Hata hivyo, mwaka huu 2023, Tanzania imepata mtoto mwingine mwenye ugonjwa huo katika Manispaa ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa.

Amefafanua kuwa chanjo hiyo itatolewa katika mikoa sita iliyopo mipakani, ambayo ni Mkoa wa Songwe, Kigoma, Rukwa, Katavi, Mbeya, pamoja na Kagera.