Bilioni 70 zatengwa kulipa madeni ya Makandarasi kila mwezi

0
108

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga shilingi Bilioni 70 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya makandarasi wanaoendelea kutekeleza miradi ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege nchini.

Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo Bilioni 50 zinaenda kulipa makandarasi wa ndani na Bilioni 20 kwa makandarasi wa nje.

Amesema hayo wakati akikagua utekelezaji wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa ambao ujenzi wake umefikia hatua za mwisho na unatarajiwa kukabidhiwa kwa wana Iringa mwishoni mwa mwezi huu.

“Mheshimiwa Rais ameiwezesha Wizara ya Ujenzi kwa kutupa Bilioni 70 kwa ajili ya kulipa makandarasi wa ndani kama kipaumbele cha kwanza kwa madeni ambayo wamekuwa wakidai hadi Juni 30, 2023”, amesema Bashungwa.

Ameongeza kuwa kwa utaratibu huo ndani ya miezi mitatu na nusu Serikali itakuwa imekamilisha madeni ya makandarasi wa ndani ili kazi zote zilizokuwa zikifanywa na makandarasi hao zisiweze kusimama, baada ya hapo fedha hizo (bil 70) zitaendelea kulipa madeni yaliyobaki kwa wakandarasi wa nje.

Bashungwa amesema kuwa mbali na Serikali kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja ya kimkakati juhudi hizo zinaenda sambamba na kujenga anga la Tanzania ili kuimarisha usafiri wa anga kwa kuboresha viwanja vya ndege nchini.

Kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Waziri Bashungwa amesema ni maelekezo ya Rais kukamilisha kiwanja hicho kwa viwango vya juu ili kuruhusu ndege kuruka na kutua saa 24.

“Wana Iringa niwapongeze sana kwa kupata uwanja, uwanja ambao sasa hivi hata wawekezaji wanaotaka kuwekeza Iringa watakuwa na uhakika kuna uwanja ambao umezingatia mambo yote ya kiusalama”, amefafanua Bashungwa.