Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishat Dkt. Doto Biteko pamoja na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga wamepokelewa rasmi na Menejimenti na Watumishi wa wizara ya Nishati katika Ofisi za wizara hiyo zilizopo jijini Dodoma, baada ya kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa hizo.
Dkt. Biteko amesema kazi iliyo mbele ni kuhakikisha huduma ya nishati inawafikia Wananchi wote na kwamba pamoja kazi nzuri iliyofanyika ya kuimarisha sekta ya Nishati, bado kuna nafasi ya kufanya kazi hiyo vizuri zaidi ili nishati ya uhakika ipatikane.
“Kama watu hawapati umeme, kama watu hawapati nishati wanayoihitaji, hata tukivaa suti za namna gani tunakuwa hatuna maana na tutakuwa tunasemwa kila siku, kiu yangu ni kuona tunafanya kazi kwa viwango ili huduma ya nishati iwafikie wananchi wote.”amesisitiza Dkt. Biteko
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyompatia ili kuweza kuhudumia sekta ya nishati kama Mbunge aliyetoka katika kundi la vijana na ameahidi uchapakazi, weledi na ufanisi katika kazi zake.