Zitto: Sensa ni zoezi muhimu

0
129

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amewataka wananchi kujitokeza kuhesabiwa kwenye sensa ya watu na makazi hapo kesho, ili kuiwezesha serikali kuwa na takwimu zitakazoisaidia kujua namna ya kuwahudumia wananchi.

Zitto ametoa wito huo wakati akizungumza katika Kipindi cha Jambo Tanzania kinachotangazwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Amesema matokeo ya sensa ya watu na makazi yatasaidia kufahamu sekta zipi zimeajiri vijana pamoja na kujua takwimu za kiwango cha umasikini wa watanzania.

Zitto amesema kutokana na umuhimu wa sensa, ndio maana chama cha ACT Wazalendo kimeendelea kuwahamsisha wanachama wake na Watanzania wote kushiriki zoezi hilo kikamilifu.

“Kutokana na zoezi la sensa kuna faida kubwa sana, maana sensa itatoa uhalisia wa mahitaji ya Watanzania na namna ya kujipanga kuwahudumia watu kulingana na uhitaji wa makundi halisi.” ameongeza Zitto Kabwe