Wizara ya Ulinzi yasema anayehitaji ujuzi milango ipo wazi

0
135

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax amesema, milango ipo wazi kwa yeyote anayehitaji kupata ujuzi wa namna ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Dkt. Stergomena ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Sabasaba yanapofanyika maonesho ya 46 ya biashara ya kimataifa ambapo leo Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) linatimiza miaka 41 tangu kuanzishwa kwake.

Amesema SUMA JKT ipo tayari kutoa ujuzi kwa yeyote aliye tayari kutoa ushirikiano katika suala la uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, na kuongeza kuwa kikubwa wanachosisitiza ni ubora.

Amesema ikiwa imetimia miaka 41 ni wakati muafaka kwa SUMA JKT kuchagua eneo ambalo litajipambanua zaidi na kuwekeza, hususani katika miradi mikubwa ya kitaifa ili kuchangia uchumi wa Taifa na kutaja moja ya miradi hiyo kuwa ni kilimo cha alizeti.

Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa Julai Mosi mwaka 1981 kwa amri ya aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa wakati huo Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa lengo la kufanya biashara na kuzalisha faida ili kusaidia gharama za uendeshaji wa shughuli za JKT pamoja na kujenga uchumi wa Taifa.