Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameagiza kuondolewa kazini kwa Wakandarasi wawili wanaotekeleza miradi ya maji ya Buhigwe na Kaseke mkoani Kigoma, kwa madai ya kushindwa kufanya kazi kulingana na matakwa ya mikataba yao.
Waziri Aweso ametoa agizo hilo mkoani Kigoma na kuwataja Wakandarasi hao kuwa ni Fabec investment anayetekeleza mradi wa maji wa Kaseke uliopo katika halmashauri ya Kigoma DC na Mbesso Construction Company Ltd anayetekeleza mradi wa maji wa Buhigwe uliopo wilayani Buhigwe.
Waziri Aweso amesema kuwa mradi wa maji wa Kaseke ambao ujenzi wake unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.1 ulitakiwa ukamilike mwezi agosti mwaka 2020 lakini mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 65, huku mradi wa maji wa Buhigwe unaogharimu shilingi bilioni 1.8 uliotakiwa kukamilika mwezi machi mwaka 2019 mpaka sasa umefikia asilimia 45.