Walioomba mikopo HESLB watakiwa kufanya marekebisho

0
167

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa muda wa siku nne kwa Wanafunzi takribani elfu tatu walioomba mikopo kwa mwaka wa masomo wa 2021/2022 kufanya marekebisho, ili kukamilisha taratibu za maombi yao.

Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronica Nyahende amesema mara baada ya kukamilika kwa hatua hiyo ya marekebisho, bodi itaanza kuwapangia mikopo Wanafunzi wahitaji.

Dkt. Nyahende alikuwa
akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

“Katika uhakiki wa maombi tumebaini waombaji 2,982  fomu zao zina kasoro, tumetoa muda wa siku nne na baada ya hatua hiyo kukamilika tutaanza mchakato wa kupanga mikopo kwa wanafunzi wenye sifa na uhitaji.” amesema Dkt. Nyahende

Kwa mujibu wa Dkt. Nyahende, hadi kufikia Septemba 30 mwaka huu HESLB ilikuwa imepokea maombi 88,688 na kati ya maombi hayo 85,706 yalikuwa kamilifu na 2,982 yalitakiwa kufanyiwa marekebisho.

Amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha fedha za mikopo ya Wanafunzi zinalipwa kabla ya vyuo vya elimu ya juu kuanza kufunguliwa kuanzia Oktoba 25 mwaka huu.

Katika mwaka wa masomo wa 2021/2022, Serikali imetenga shilingi bilioni 570 kwa ajili ya bajeti ya mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya juu 162,000 wakiwemo wale wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.