Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameitaka Bodi ya Maziwa kwenda katika halmashairi na vikundi vya vijana na wakina mama wanaojihisisha na maziwa kuhamsisha ukusanyaji wa maziwa ili kuongeza mnyororo wa thamani ya maziwa.
Hayo ameyasema wakati wa kikao na bodi ya maziwa na bodi ya nyama ili kupanga namna ya kutumia fursa zilizopo kwenye soko la kimataifa la bidhaa hizo kutokana na unafuu utakaokuwepo kwenye uzalisha wa bidhaa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022
Aidha, Ulega amewaambia wajumbe wa bodi za maziwa na nyama kufika katika maeneo ya wafugaji na wajasiriamali kujua changamoto zinazowakabili na kuzitatua mara moja
“Nendeni mkatoe elimu kwa wafugaji kila halmashauri juu ya kunenepesha mifugo ili kuleta mnyororo wa thamani katika sekta ya mifugo kwa wafugaji walioko vijiji ili kuanza kuuza nyama kwa wingi ndani na nje ya nchi,” amesisitiza Ulega
Awali Msajili Bodi ya Maziwa, Dkt. George Msaya na John Chassama Meneja Masoko Bodi ya Nyama wameeleza namna watavyowafikia wauzaji wa maziwa na wafugaji kupitia halmashauri kutoa elimu ya namna ya kuuza bidhaa zao kwa faida na kujipatia kipato na kuleta manufaa kwa Taifa kwa ujumla.
Tanzania ni moja ya nchi barani Afrika zenye idadi kubwa ya mifugo ikiwepo ngo’mbe, mbuzi na kondoo wanaoweza kutumika kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa Taifa na maendeleo ya watu.
Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza na Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi juu ya kupeleka wataalamu Botswana kujifunza namna ya uzalishaji wa nyama kwa wingi ili kuja kusaidia wafugaji kufunga kitaalamu na tija.