Karibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amezuru kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais, Marehemu Dkt. Omari Ali Juma, Chake chake Pemba na kutaka aenziwe kwa mazuri aliyoyapigania.
Akizungumza akiwa kaburini hapo kabla ya kushiriki dua ya kumwombea marehemu Dkt. Omari, Shaka amesema mwaka huu Dkt. Omari ametimiza miaka 21 tangu kutokea kifo chake mwaka 2001, huku nchi ikitimiza miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi.
“Hapa sio sehemu ya kutoa hotuba, ujumbe wangu ni kwamba mwaka huu tunatimiza miaka 21 tangu Dkt. Omari alipotutoka. Alikuwa nguzo muhimu kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, wakati wote na kwa nafasi zote alizoaminiwa alitimiza majukumu yake kwa uzalendo mkubwa.
“Wakati tukimkumbuka Dkt. Omari Ali Juma nchi yetu inatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, huwezi kuzungumzia mafanikio ya demokrasia bila kumkumbuka Dkt. Omari kutokana na jitihada alizozichukua. Tuyaenzi yale aliyoyasimia kwa maendeleo ya taifa,” amesema.
Aidha, amesema wakati Watanzania wakimwombea Dkt. Omari pia wamwombee Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameendeleza ndoto na za viongozi waliotangulia akiwemo Dkt. Omari.
Awali akizungumza kabla ya Dua hiyo, mwakilishi wa familia ya Dkt. Omari, Zubeir Ali Juma alishukuru na kukupongeza kwa uamuzi wa Shaka pamoja na viongozi mbalimbali kwa kuendelea kudhuru kaburi hilo mara kwa mara.