TCRA yaagizwa kuongeza utoaji elimu kwa umma

0
196

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa umma kuhusu matumizi ya mtandao ‘digital literacy’ kwa kuwa mpaka sasa kiwango cha kuelimisha umma kinachotolewa na Mamlaka hiyo hakitoshelezi.

“TCRA bado sijaridhishwa na kiwango cha elimu ya matumizi ya mtandao mnayoitoa kwa umma na katika utoaji wa elimu kwa umma mkumbuke kuelimisha jamii kuhusu wajibu na haki zao ili wanapopata shida mitandaoni wajue wapite katika njia zipi”, Dkt. Ndugulile

Aidha, Dkt. Ndugulile ametoa maelekezo kwa TCRA kuimarisha mfumo wa ukaguzi wa vifaa vya kielektroniki vinavyouzwa na wafanyabiashara ili kuthibitisha ubora na uhalali wa vifaa hivyo ikiwezekana viwekewe alama kuwa vimekaguliwa ili kuhakikisha usalama wa vifaa hivyo kwa matumizi ya wananchi.

Katika hatua nyingine Dkt. Ndugulile ameielekeza TCRA kuhakikisha Shirika la Posta Tanzania linafanya kazi yake ya kusafirisha vipeto na vifurushi kwa kufuata sheria ya EPOCA inayosema kuanzia uzito wa 0 hadi 0.5 gms haruhusiwi msafirishaji yeyote kusafirisha isipokuwa Shirika hilo na kuitaka TCRA kusimamia vema suala hilo.

Kwa upande wa Mkuu wa TCRA wa ofisi ya Zanzibar, Esuvatie Masinga amesema kuwa Mamlaka hiyo inaendelea kujipanga vizuri katika utoaji wa elimu kwa umma na wiki hii tayari wameshatoa mafunzo ya matumizi ya TEHAMA kwa masheha 120 kwa Unguja na Pemba.