Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amefungua mkutano wa viongozi wa juu unaohusu kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwa kuunga mkono maendeleo endelevu ya uchumi wa buluu kwa nchi zinazoendelea, nchi zinazoendelea zisizo na bahari pamoja na nchi za visiwa vidogo.
Mkutano huo ni sehemu ya mikutano ya viongozi wa juu ya uhifadhi wa bahari na rasilimali zake inayoendelea jijini Lisbon nchini Ureno.
Katika mkutano huo Makamu wa Rais ametoa wito kwa mataifa kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa manufaa ya kiuchumi kwa nchi zote ikiwa ni pamoja na kuunganisha nguvu za pamoja ,kuwekeza katika teknolojia za kibunifu pamoja na tafiti.
Amesema ni muhimu kuyashirikisha moja kwa moja makundi ya kijamii ikiwemo wanawake, vijana na jamii inayotumia bahari, ili kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya bahari na rasilimali zake.
Dkt. Mpango amesema ili kufikia maendeleo endelevu ya uchumi wa Buluu inapaswa kuzingatia hali ya kijamii, kiuchumi na kimazingira wakati wa matumizi ya rasimali za bahari kama vile ongezeko la idadi ya watu, kuongezeka kwa matumizi na hitaji la vyanzo vipya vya chakula, nishati na madini.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yupo nchini Ureno kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhifadhi wa bahari na rasilimali zake wenye lengo la kuhamasisha juhudi za mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa lengo la 14 la maendeleo endelevu.