Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Tanzania inakwenda kufufua mpango wa miaka mitatu wa maendeleo ya Sekta za utamaduni, sanaa na michezo ulioingiwa na Serikali ya China.
Akizungumza Februari 4, 2022 jijini Dar es Salaam na Balozi wa China nchini Chen Mingjian katika kikao maalum kwenye sherehe za uzinduzi wa michezo ya msimu wa baridi ya Olympic 2022 amesema tayari wizara yake imeandaa andiko kwa ajili ya mpango huo litakalowasilishwa hivi karibuni.
Katika kikao hicho Waziri aliambatana na Katibu Mkuu wake, Dkt. Hassan Abbasi
“Tunatarajia kuwasilisha mpango wetu ambao tutaingia makubaliano ili utekelezaji wake uanze mara moja” amefafanua Mchengerwa
Kwa upande wake Balozi Chen amesema ni wakati mwafaka wa kufufua na kuendeleza sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuinua uchumi wa nchi zote baada ya kushuka kutokana na ugonjwa wa Uviko 19.
Amesema Serikali yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu kupitia mafunzo mbalimbali.