Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ijumaa wiki hii linatarajiwa kupitisha Sheria ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa ikitoa Mamlaka kwa mtu kujipima Virusi vinavyosababisha Ukimwi.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa ufunguzi wa semina elekezi kwa Wasanii mbalimbali, semina iliyoandaliwa na Wizara hiyo ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa pamoja na Baraza la watu wanaoishi na Virusi vinavyosababisha Ukimwi(NACP).
“Changamoto kubwa inayoikabili Wizara ya Afya katika suala zima la VVU na UKIMWI ni wanaume kutojitokeza kwa wingi kupima, na hapa ninavyoongea leo hadi Ijumaa sheria ya watu kujipima wenyewe Virusi vya UKIMWI majumbani kwao itapitishwa rasmi, lakini hata hivyo itampasa mtu kwenda hospitali kupima tena ili ajiridhishe hata kama atakuwa ameshajipima mwenyewe,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepeleka Bungeni mapendekezo ya Sheria itakayoruhusu umri wa mtu kupima virusi vinavyosababisha Ukimwi uanzie miaka 15.