Serikali yaipatia TBC shilingi bilioni 5

0
256

Serikali imelipatia  Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) shilingi bilioni tano, ambazo pamoja na mambo mengine zitatumika katika kuboresha usikivu redio ya TBC Taifa hasa kwenye maeneo ya pembezoni.

Akizungumza mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kutembelea ofisi za TBC Kanda ya Kati jijini Dodoma, Mwenyekiti wa kamati hiyo Stanslaus Nyongo amelitaka shirika hilo kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema, Serikali itaendelea kuisaidia TBC ili itekeleze majukumu yake ipasavyo.

Amesema katika mapendekezo ya mpango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, TBC ni miongoni mwa taasisi zilizopewa kipaumbele.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt Ayub Rioba Chacha amesema kuwa, pamoja na maboresho ya usikivu wa matangazo maeneo ya pembezoni, maboresho mengine yatakayofanywa na shirika hilo ni kuongeza ubunifu kwenye vipindi vinavyorushwa kupitia vituo vya redio na televisheni vya TBC.