Kamati ya Kudhibiti Magonjwa katika wilaya ya Jimei huko Xiamen nchini China, imeanza kutekeleza mpango wake wa kuwapima samaki pamoja na wavuvi pindi wanapotoka kuvua, ili kufahamu kama wana UVIKO – 19 au la.
Mpango huo ulitangazwa kuanza kutumika katika wilaya hiyo ya Jimei mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, kwa hofu kwamba wavuvi wa kigeni wanaweza kuingiza nchini humo ugonjwa wa UVIKO -19.
Mpango huo unahusisha kupima wavuvi wenyewe, samaki pamoja na vifaa ambavyo watakuwa wamevitumia katika shughuli zao za uvuvi.
Picha mbalimbali za video zimeonekana kwenye mitandao ya kijamii zikionesha samaki wakipimwa vipimo vya UVIKO -19, hali ambayo imeonekana kuwashangaza watu wengi.
https://twitter.com/manyapan/status/1523245989250883586?s=20&t=dKL45UrnwdD_pkY_5r5IGA
Hii si mara ya kwanza kwa samaki walio hai kupimwa UVIKO -19 huko Xiamen.
Mmoja wa wafanyakazi katika ofisi ya Maendeleo ya Bahari huko Xiamen ameliambia gazeti la South China Morning Post la nchini China kuwa “tumejifunza kutoka sehemu ya Hainan, ambayo inashuhudia mlipuko mbaya wa UVIKO – 19.”
Uongozi wa mji wa Xiamen umeagiza zaidi ya watu milioni tano wa mji huo wapimwe ili kujua kama wana UVIKO – 19 au la, na hiyo ni baada ya kugundulika kwa watu 40 wanaougua ugonjwa huo.