Love transfusion – filamu ya kitazania yenye viwango vya kimataifa.

0
172

Ubora wa filamu za kitanzania umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2023 filamu ya Kitanzania inayokwenda kwa jina la LOVE TRANSFUSION imekuwa gumzo mitandaoni baada ya trailer lake kuachiwa hivi karibuni.

Imezoeleka kwenye filamu nyingi kuongozwa na wanaume, lakini mambo ni tofauti katika filamu hii ambayo wanawake wamechukua nafasi kubwa kuifanikisha. Hii ikijumuisha Muongozaji (Director), Meneja uzalishaji (Production Manager), Muongozaji wa ubunifu (Art Director), Mapambo, Msimamizi wa mswada na Maleba, wote hawa ni wanawake lengo ni kuonesha ubunifu na uwezo wa wanawake katika kutengeneza filamu zenye ubora wa kimataifa.
Filamu hiyo ambayo imetayarishwa na Kefa Igilo na Jerryson Onasaa na kuongozwa na Winnie Nzunda, inahusu simulizi ya matokeo ya kiapo cha yamini ya mahusiano kilichochukuliwa na wanandoa watarajiwa kwa lengo la kuimarisha uhusiano wao.

Mambo yanakwenda kinyume na matarajio yao baada ya masharti kukosewa na kupelekea mfululizo wa visa na mikasa ya kusisimua na kufanya penzi lihamie kwa muhusika mwengine.

Filamu hii inalenga kuchunguza utata wa mahusiano ya kibinadamu na matokeo ya matendo na maamuzi yetu, pamoja na nguvu ya upendo na utayari wa watu kufanya jambo lolote kwa wale wanaowapenda bila ya kupima madhara yake.

Filamu hii imechezwa na waigizaji mahiri ambao walishinda tuzo kadhaa katika Tuzo za Filamu Tanzania mwaka 2022 akiwemo Tunu Mbegu ambaye alishinda Tuzo ya Muigizaji bora wa kike na Collins Frank ambaye alishinda Tuzo ya Muigizaji bora chipukizi wa Kiume. Waigizaji wengine ambao ni sura mpya kwenye tasnia ya filamu na wameonesha uwezo wa hali ya juu ni pamoja Prisca Lyimo ambaye ni Miss Tanzania Mshindi wa tatu mwaka 2020, Ally Kashmiry ambaye ni mtangazaji na msoma habari kutoka Clouds TV, Christian Mandingo pamoja na Glory Baltazary.

Kwa mujibu wa watayarishaji, ujio wa filamu hii ni matokeo ya mafanikio ya kazi yao ya kwanza ‘STILL OKAY TO DATE’ambayo ilifanya vizuri ndani ya nchi na nje ya nchi kwa kushinda tuzo ya filamu bora ya kimataifa katika tuzo za kalasha mwaka 2022 ambazo huandaliwa na bodi ya filamu ya Kenya.

Kwa taarifa zaidi kuhusu namna gani unaweza kutazama filamu hiyo ambayo itaoneshwa kwa mara ya kwanza tarehe 18/03/2023, fuatilia kurasa zao binafsi za mitandao ya kijamii. Au ukurasa rasmi wa instagram wa filamu hiyo unafahamika kwa @ltmovie2023.