Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amezindua Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii nchini na kuitaka kurekebisha kasoro zilizojitokeza siku za nyuma na pia ugawaji ufanyike kwa uwazi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Arusha, Mchengerwa amesema ameunda kamati hiyo kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa kifungu cha 38 (1) na (2) ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori sura ya 283 huku akisisitiza kwamba Kamati hiyo inatakiwa kuboresha changamoto zote ili tasnia ijiendeshe kibiashara.
“Ni imani yangu kwamba kwa kuzingatia ushauri utakaotolewa na Kamati hii tasnia ya Uwindaji wa Kitalii itazidi kuimarika na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi”. Amesema Mchengerwa na kuongeza kuwa
“Pia Kamati itasaidia kuhakikisha vitalu vyote vinapata wawekezaji ili kuongezea mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na vitalu 43 ambavyo kwa sasa vipo wazi.”
Mchengerwa
amefafanua kuwa uwindaji wa kitalii unachangia katika pato la Taifa hususani fedha za kigeni na kwamba kwa wastani, Serikali inakusanya takribani shilingi Bilioni 30 kwa mwaka kutokana na uwindaji.
Naye Katibu wa Kamati hiyo ambaye pia ni Kamishna wa Mamlaka ya Wanyamapori nchini (TAWA) Mabula Nyanda amemshukuru Waziri Mchengerwa kwa kuunda Kamati hiyo na kusema itasaidia kuboresha tasnia hiyo ya uwindaji wa kitalii.