Hukumu ya akina Aveva yaahirishwa tena

0
144

 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo mkoani Dar es Salaam imeshindwa kutoa hukumu ya kesi inayomkabili Rais wa zamani wa klabu ya Simba, Evans Aveva na mwenzake Godfrey Nyange hadi tarehe 28 mwezi huu.
 
Hukumu hiyo ambayo ilitarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Thomas Simba imeshindwa kutolewa kwa kile alichoeleza Hakimu huyo kuwa ni sababu zilizo nje ya uwezo wake.
 
Katika shtaka la kughushi, washtakiwa wote wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na klabu ya Simba zina thamani ya dola 40,577 za Kimarekani sawa na zaidi ya shilingi milioni 90, huku wakijua kwamba sio kweli kosa ambalo wanadaiwa kulitenda Mei 28 mwaka 2016.
 
Pia katika mashtaka mengine inadaiwa Aveva na Nyange kati ya Machi 10 na Septemba 30 mwaka 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo wakionyesha kwamba klabu ya Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya dola 40,577 za Kimarekani wakati wakijua sio kweli.
 
Hii ni mara ya pili hukumu ya kesi hiyo ikiahirishwa ambapo tarehe 6 mwezi huu Eveva hakutokea kwa kile kilichoelezwa kwamba alikwenda kwenye matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili mkoani Dar es Salaam.