CCM Kilimanjaro yabatilisha maamuzi ya Mkurugenzi

0
123

Chama cha Mapinduzi Mkoani Kilimanjaro, kimesema maamuzi yaliyofanywa na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mwanga Zefrin Lubuva ya kuzuia magari mawili ya mkandarasi kutoka kampuni ya Bona and Hubert Engineering (T) LTD anayejenga kipande cha barabara ya Mwanga-Kikweni-Vuchama, kilometa 4.2 kwa kiwango cha lami, ni batili.

Akitoa tamko la kikao cha Halmashauri kuu ya CCM Mkoa, kilichokaa leo mjini Moshi,Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa Patrick Boisafi, amesema maamuzi yaliyochukuliwa na mkurugenzi huyo, ni yake binafsi na sio mambo ya kiutumishi na chama hakitakubaliana na mamauzi hayo.

Boisafi amesema kitendo hicho kimeisababishia serikali kupata hasara na kwamba Ccm haikotayari kuona serikali inaingiziwa hasara kwa mambo ambayo hayana tija kwa wananchi.

Kufuatia hali hiyo, wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM mkoa wamepitisha kwa kauli moja, magari yaliyokamatwa ya mkandarasi huyo kuachiwa na ujenzi wa barabara hiyo uendelee na ukamilike kwa wakati, ili kunufaisha wananchi.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai, amesema alishatoa maelekezo magari hayo yaachiliwe bila kutekelezwa na kumuagiza katibu tawala wa Mkoa huo Dkt. Seif Shekalaghe, kufuatilia na iwapo kutakuwa na hasara yoyote iliyopatikana kutokana na kukamatwa kwa magari hayo, Mkurugenzi huyo awajibike.