90% ya vifo vya uzazi vinatokea hospitalini

0
245

Wanawake 556 kati ya Laki Moja hufariki dunia kila mwaka kutokana na uzazi, huku asilimia 90 ya vifo hivyo vikiripotiwa kutokea hospitalini na katika vituo vya afya.

Sababu za vifo hivyo zinatajwa kuwa ni mimba za utotoni na kukosa ujuzi kwa baadhi ya watoa huduma.

Takwimu hizo zimetolewa mkoani Dar es Salaam na Meneja wa programu ya afya ya uzazi wa mama na mtoto kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya afya ya uzazi na idadi ya watu (UNFPA) Felister Bwana, wakati wa semina iliyoshirikisha waandishi wa habari.

Amesema moja ya ajenda za UNFPA ni kuhakikisha vifo vinavyotokana na uzazi vinakomeshwa hasa katika nchi zinazoendelea.

Kwa upande wa vyombo vya habari Felister amesema bado vina jukumu la kusaidia kutoa elimu ya masuala ya uzazi katika jamii.

Mchambuzi wa masuala ya idadi ya watu na maendeleo kutoka UNFPA Ramadhani Hangwa amesema kufuatia maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano uliofanyika Nairobi, Kenya mwaka 2019, shirika hilo limeandaa mkutano maalum utakaofanyika tarehe 9 na 10 mwezi huu.

Amesema lengo la mkutano huo ni kupokea taarifa ya utekelezaji wa mambo mbalimbali ikiwemo usawa wa kijinsia na vifo vya wanawake kipindi cha ujauzito.