HOSPITALI YA RUFAA KANDA YA KUSINI MTWARA YAZINDULIWA

0

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, ambayo itahudumia wagonjwa wa rufaa kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, na nchi jirani kama Msumbiji, Zambia, Malawi, na visiwa vya Comoro.

Hospitali hiyo yenye sakafu tano, ujenzi wake umegharimu takribani bilioni 15 hadi kukamilika, na inakadiriwa kutoa huduma kwa wagonjwa 800-1,000 na kuwa na vitanda 1000 vya kulaza wagonjwa.

Huduma zitakazotolewa hospitalini hapo ni pamoja na upasuaji wa Jumla, tiba (Internal Medicine), matibabu ya moyo, matibabu ya watoto, tiba ya uzazi na via vya uzazi (Obstetrics and Gynaecology).

RAIS SAMIA: KUOKOA MAISHA YA WATU HAKUHITAJI STAREHE

0

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kinachofanyika katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini Mtwara ni kuokoa maisha ya watu jambo ambalo haliihitaji starehe.

Amemwelekeza waziri wa afya kutafuta fedha za kununua vifaa kama vishikwambi na kompyuta kwa ajili ya kuwasaidia wakuu wa idara na watumishi wengine wa afya kupata taarifa kwa wakati kutoka kwenye mitandao na maeneo mbalimbali kwa lengo la kuongeza ujuzi.

Sambamba na hilo amesema amewataka watumishi wa sekta ya afya kutunza jengo na vifaa watakavyonunuliwa na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha ameongeza kuwa kila mmoja anapaswa kufanya kazi ili kumridhisha Mungu kwa nafasi walizochaguliwa kwazo.

“Kila mtu alipo Mungu kamchagulia hiyo ndio destiny yake na kama Mungu kakuchagulia mridhishe Mungu kwa huduma unayotoa,” amesema Rais Samia

BANDARI YA MTWARA KUWA KAMA BANDARI YA DAR

0

Akikagua shughuli za uboreshaji wa Bandari ya Mtwara, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mkoa wa Mtwara ni kituo cha biashara kwa Kanda ya Kusini. Amesisitiza kuwa Bandari ya Mtwara haikujengwa kwa ajili ya kujenga Mtwara pekee, bali ilijengwa kwa lengo la kufungua mikoa ya Kusini na kuwa Bandari hiyo inategemewa kutoa huduma kwa nchi jirani.

Vilevile, Rais Samia amesema kuwa kwa sasa Bandari ya Mtwara ni ya pili kwa ukubwa nchini, ikitanguliwa tu na Bandari ya Dar es Salaam. Amewataka watumishi wa Bandari kufanya kazi kwa bidii na weledi ili Bandari ya Mtwara ifikie kiwango cha Bandari ya Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa Serikali imejizatiti kuongeza bajeti ya kuboresha miundombinu ya Bandari ili kuvutia zaidi wafanyabiashara. Serikali pia imejiandaa kusafirisha korosho kupitia Bandari ya Mtwara, hivyo amewaomba wananchi wajiandae kuiunga mkono Serikali kwa kuongeza mapato yanayotokana na shughuli za Bandari.

Miradi iliyotekelezwa kama sehemu ya maboresho ya utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara ni pamoja na ujenzi wa Gati moja la Nyongeza lenye urefu wa mita 300, ujenzi wa mita ya kupima mafuta ili kuhakikisha mafuta yanayoshushwa katika Bandari yanapimwa, ujenzi wa sehemu ya kuhifadhi makasha, pamoja na ukarabati wa ghala na vifaa vya kuhudumia mizigo bandarini.

Maboresho Bandari ya Tanga yakamilika

0

Meneja wa Bandari mkoa wa Tanga Masoud Mrisha amesema maboresho ya bandari yaliokuwa yakifanyika kwa takribani miaka miwili sasa yamekamilika na mkandarasi anatarajia kukabidhi rasmi September 15 mwaka huu.

Mrisha ametoa kauli hiyo wakati wa mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kueleza kuwa ukarabati huo umetumia zaidi ya shilingi bilioni 429, ambazo zimetumika kuongeza kina kutoka mita 3 mpaka kufikia mita 13 na ujenzi wa magati mawili.

Aidha maboresho hayo yamesaidia kuongezeka kwa uchukuzi wa shehena kutoka tani 750,000 za awali na matarajio ni kufikia tani milioni 3.

Ummy: Watumishi wa Afya wanapaswa kulipwa stahiki zao kwa wakati

0

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael, kuwahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuwalipa watumishi wa Afya stahiki zao kwa wakati.

Waziri Ummy ameyasema hayo wakati akiongea na wajumbe wa Timu za Usimamizi na Uendeshaji wa huduma za Afya ngazi ya Mkoa (RHMT) na Halmashauri zote za Mkoa (CHMT) na Wajumbe wa Timu ya Uendeshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (RRHMT) wakati akihitimisha ziara yake katika Mkoa wa Songwe.

“Naomba sana Mkuu wa Mkoa kupitia kwako kuwahimiza Wakurugenzi kuwalipa watumishi wa Afya stahiki zao kwa wakati ili wapate moyo wa kuendelea kutoa huduma katika vituo vyetu vya Afya,” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema Wakurugenzi wengine waige mfano wa Mkurugenzi wa Momba ambaye amewagawia viwanja watumishi wa Afya. Hivyo, lazima kuwajengea motisha na kuwavutia watumishi hao wa Afya ili waendelee kufanya kazi katika Halmashauri za Mikoa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael, amemuomba Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kupeleka watumishi wa Afya hasa madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo.

TBC na UNCDF kutoa elimu ya nishati mbadala

0

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji ya Maendeleo (UNCDF) kupitia mradi wa Cookfund yanalenga kushirikiana kuelemisha jamii kuhusu matumizi ya nishati mbadala ili kuendana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo utanzaji wa mazingira na kuondokana na madhara yatokanayo na nishati isiyo safi.

Mazungumzo ya kulenga ushirikiano huo yamefanyika katika ofisi za TBC Mikocheni, Dar es Salaam wakati viongozi wa UNCDF wakiongozwa na Mkuu wa UNCDF Tanzania, Peter Malika walipotembelea TBC na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha.

Malika amesema kupitia mradi wao wanalenga kuiunga mkono Serikali katika jitihada za kuendana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na mpango wa Serikali kuelekea matumizi ya nishati mbadala kufikia mwaka 2024 kwa taasisi zenye chini ya watu 100 na mwaka 2025 kwa taasisi zenye watu chini ya watu 200.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema TBC imekuwa mstari wa mbele kusimamia, kutunza na kuelemisha jamii kuhusu utanzaji wa mazingira kupitia vipindi mbalimbali vinavyorushwa na TBC.

Puuzeni uzushi kuhusu Msomera

0

Mkuu wa wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema wakazi wa Kijiji cha Msomera hawana tatizo lolote na serikali wala wizara ya mifugo na uvuvi, hivyo kuiomba jamii kupuuza yanayosemwa na baadhi ya watu wasioitakia mema serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.

Msando ametoa kauli hiyo mbele ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega aliyefika kijijini hapo kuzungumza na wakazi wa Msomera.

Amesema kijiji cha Msomera ni kijiji kilichopangwa kwa kufuata mpango wa matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo ya malisho na josho kwa ajili ya mifugo.

Katika awamu ya kwanza mpaka sasa tayari kaya 500 zimeshaanza makazi mapya kijijini Msomera zikitokea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na awamu ya pili ya kuwapokea wengine inatarajia kuanza Septemba 25 mwaka huu.