







Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Serikali imedhamiria kuwa mzalishaji mkubwa na nishati.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akifungua Kongamano la Tano na Maonesho ya Nishati Tanzania.
“Tunaendelea na utafutaji wa gesi, tunataka tuwe wazalishaji wakubwa wa nishati, tuwe na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na nafuu na ziada tutauza nje ya nchi.“ amesema Waziri Mkuu
Amesema Tanzania haitegemei kuzalisha umeme kwa kutumia maji pekee bali inaendelea kuweka mkazo katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati nyingine kama gesi na jua.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema kongamano hilo la kimataifa la nishati ambalo limehusisha viongozi na wadau kutoka mataifa mbalimbali Duniani litajadili namna bora ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nishati.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa ya kongamano hilo kuzisisitiza nchi zote Wanachama kuhakikisha taasisi za mafunzo zinatoa programu maalum za mafunzo katika sekta za nishati ili kuongeza idadi ya watu walio na ujuzi na maarifa kwenye sekta hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mkoa huo una hifadhi ya kutosha ya mafuta kutokana na wawekezaji kupewa kipaumbele katika kuwekeza mkoani humo.
Chalamila amesema hayo alipofanya ziara katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) zilizopo Mikocheni, Dar es Salaam na kuongeza kuwa mkoa wa Dar es Salaam hautakutana na
changamoto ya uhaba wa mafuta kwa kuwa kuna uwekezaji mkubwa uliofanywa na Wafanyabiashara wa mafuta.
Chalamila amewahakikishia Wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa mkoa huo ni salama na vyombo vya ulinzi viko imara kuhakikisha mkoa huo upo shwari wakati wote.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Wananchi wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kuongeza nguvu katika kilimo, ili kuchochea maendeleo.
Rais Samia amesema pamoja na jitihada zingine, Serikali imejidhatiti kupandisha bei ya zao la korosho ili wakulima wa zao hilo wanufaike nalo.
Akiwasalimia wananchi wa Ruangwa baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Nanganga – Ruangwa – Nachingwea mkoani Lindi Rais Samia amesema, azma ya Serikali ni kuboresha miundombinu ya barabara zitakazouunganisha mkoa wa Lindi kwa lami.
Rais Samia Suluhu Hassan pia amewataka Wakandarasi wilayani Ruangwa kukamilisha miradi kwa haraka.
Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la Msingi la ujenzi wa barabara ya Nachingwea – Ruangwa – Nanganga, sehemu ya Ruangwa – Nanganga yenye urefu wa kilomita 53.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo hadi kukamilika kwake itagharimu shilingi Bilioni 50.3.
Akizindua ujenzi wa barabara hiyo Rais Samia amesema Serikali imejipanga kujenga miundombinu ya mikoa ya Kusini ili kurahisisha usafirshaji wa mazao na kukuza uchumi wa mikoa hiyo na hivyo kuwataka Wakandarasi wakamilishe ujenzi wa barabara hiyo kwa wakati.
“Niwaombe wakandarasi na wasimamizi waende kwa kasi sana, lakini nipongeze TANROADS mkandarasi na wengine kwa hatua ambayo imeshafikia na kwetu sisi Serikali mafedha yapo tunasubiri certificate [cheti] ziletwe tulipe kazi ziendelee”. amesema Rais Samia
Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuunganisha mkoa wote wa Lindi kwa barabara za kiwango cha lami pamoja na wilaya kwa wilaya ziunganike kwa barabara za lami.
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imesema itahakikisha inatenga bajeti ya kutosha ya kuweka taa katika barabara zote zinazopita katika miji ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi katika maeneo hayo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa , mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Sabasaba uliopo Wilaya ya Newala mkoani Mtwara ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Rais Samia katika mikoa ya Kusini.
Aidha, Waziri Bashungwa amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wanaoendelea kutekeleza mradi wa barabara kuanzia Mnivata hadi Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami ili kazi iweze kukamilika na kwa viwango vya juu.
“Niwaombe wananchi wa Mtwara mtoe ushirikiano kwa wakandarasi na muwe sehemu ya miradi hii kwa upendo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameleta mabilioni ili tuweze kujenga lami kwa viwango vya juu”, – amesisitiza Bashungwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, amewaeleza wananchi wa Kijiji cha Nanguruwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, kuwa hadi ifikapo mwezi Machi 2024, vitambulisho vya Nida vitapatikana nchi nzima.
Akijibu moja ya kero na changamoto za wananchi zilizowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, Shamsia Mtamba, wakati wa Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan Mkoani Mtwara, Masauni amesema kuwa hadi sasa vitambulisho milioni 2 tayari vimepokelewa.
Ameongeza kuwa kwa wakati huu, namba za utambulisho zinaendelea kutumiwa kutoa huduma zote na kuwataka wananchi kutambua kuwa kutopata vitambulisho hakutawazuia kupata huduma.
Aidha, ameziagiza taasisi za umma nchini zinazotoa huduma kwa wananchi kutokumnyima mwananchi huduma kwa makosa yasiyo yake.