TRILIONI 1 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MIJI

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, ameshuhudia utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC), mradi utakaoziendeleza halmashauri 45 nchini.

Mradi huo utagharimu dola Milioni 410 za Kimarekani ambazo ni zaidi ya shilingi Trilioni Moja, fedha kutoka Benki ya Dunia.

Mradi huo utakaotekelezwa kwa muda wa miaka sita unalenga kuboresha miundombinu kwa kujenga barabara za lami, masoko, vituo vya mabasi, bustani za kupumzikia, mitaro ya maji ya mvua na vivuko.

KATIBU MKUU FUATILIA MTANDAO WA WEZI FEDHA ZA MIRADI

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kufuatilia mtandao wa wizi wa fedha za miradi.

Mchengerwa ametoa agizo hilo wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTICS) iliyofanyika mkoani Dar es Salaam.

Amesema eneo la fedha za miradi lina changamoto, hivyo amemtaka Katibu Mkuu TAMISEMI kufuatilia mtandao huo wa wizi ili kubaini watumishi wa TAMISEMI wanaohusika.

Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, kwa
sasa ana ushahidi wa halmashauri tano ambazo baadhi ya viongozi wa halmashauri hizo na Watumishi wanadaiwa kugawana fedha za miradi.

MASHIMO BARABARANI KUGHARIMU NAFASI ZA MABOSI TARURA

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa
amewataka watendaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuacha utaratibu wa kuchimba barabara na kuziacha na mashimo kwa muda mrefu bila kuyafukia.

Ametoa maelekezo hayo alipokuwa akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) iliyofanyika mkoani Dar es Salaam.

Kwa upande wa Mameneja wa TARURA amewataka kuhakikisha bajeti ya kufukia mashimo inakuwepo pale ambapo wanakwenda kuchimba mashimo katika barabara.

Ameonya kuwaondoa katika nafasi zao watendaji wa TARURA pamoja na Mameneja wa TARURA wa mikoa na wilaya pale ambapo mashimo hayo yataachwa wazi hadi wiki mbili bila kuchukuliwa hatua zozote.

Waziri Mchengerwa amesema yapo mashimo yamechimbwa na kuachwa wazi mwezi mzima, hali inayosababisha adha kwa watumiaji wa barabara.

Msigwa Katibu Mkuu wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo

0

Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Gerson Msigwa kuwa Katibu Mkuu wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Kabla ya uteuzi huo Msigwa alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Nafasi iliyoachwa wazi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali itatangazwa baadae.

Mkurugenzi Busega asimamishwa kazi

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busega mkoani Simiyu, Veronica Vicent Sayore, kuanzia leo 22 Septemba, 2023 ili kupisha uchunguzi.

Mchengerwa amechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kuhusu utendaji kazi usioridhisha, kutokuwa na ushirikiano na viongozi wenzake pamoja na kutowashirikisha watendaji katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kutokana na tuhuma hizo, Mchengerwa amemwelekeza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuunda timu ya uchunguzi wa mwenendo wa utendaji kazi wa Mkurugenzi huyo pamoja na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega.

Aidha, amewataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, kusimamia dhana ya ushirikishwaji wa viongozi, watendaji na wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuimarisha uhusiano mzuri baina ya viongozi na watendaji ili kujenga timu yenye umoja katika kutekeleza jukumu la kuwahudumia wananchi.

Mfumo mpya wa manunuzi serikalini kudhibiti rushwa

0

Mfumo wa kielektroniki unaowezesha kufanya usajili, kuchakata zabuni, kusimamia mikataba, malipo na kununua kupitia katalogi na minada kimtandao (NeST) uliotengenezwa na Watanzania unatarajiwa kudhibiti vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa kughubika michakato wa ununuzi Serikalini.

Uhakika huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Eliakim Maswi akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania na kuongeza kuwa mfumo huo wa kisasa utarahisisha zaidi michakato ya manunuzi.

Akieleza ufanisi wa mfumo huo, amesema awali katika mfumo wa TANePS walilazimika kufanyia michakato yote pembeni kisha kuipakia (upload) taarifa kwenye mfumo, lakini kupitia NeST, michakato itafanyika kwenye mtandao na hivyo kutoa uwazi kwa wazabuni na umma kuona mwenendo mzima.

Aidha, mfumo huo utaondoa malalamiko ya watu kukosa tenda kwa sababu utaonesha sababu za mwombaji kukosa, pia utaongeza ushindani kwa kuonesha idadi ya tenda zilizopo, tenda zilizoombwa, tenda zilizo wazi, utaonesha ni nani anayechelewesha mchakato kukamilika pamoja na taarifa nyingine muhimu katika manunuzi.

“Ule mfumo tunaoachana nao, kampuni moja ya Kigiriki ilituuzia. Lakini kama Taifa, mkitengeneza mfumo wenu, maana yake taarifa zote na takwimu zote mnazo nyie wenyewe. Lakini ule mwingine, hata Mgiriki yule alikuwa anaona tunachofanya. Sasa hivi tunaona sisi wenyewe,” amesema Maswi akieleza namna mfumo mpya unavyotekeleza sera ya usiri wa taarifa.

Amesema mfumo huo utaanza kutumika rasmi Septemba 30 mwaka huu ambapo NeST utatumika kwenye taasisi zote na kwamba kwa mujibu wa sheria mpya Afisa Masuuli asipotumia mfumo ataweza kutozwa faini isiyopungua milioni 10, kifungu kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Polisi Tanga yawanasa watuhumiwa wa wizi

0

Jeshi la polisi mkoani Tanga linawashikilia raia wawili kutoka Kenya kwa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaibia watu wanaopaki magari nje ya benki na wanaopaki magari nje ya ofisi.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amewataja raia hao kuwa ni Idrisa Musa Kasimu (24) na Samweli Kimath (25), waliokuwa wakitumia gari lenye namba za usajili T 931 CVS aina ya IST.

Amesema baada ya mahojiano na jeshi la polisi kukamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.

Wanahabari watakiwa kuepuka upotoshaji

0

Mkuu wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Erasto Sima amewashauri waandishi wa habari kuzingatia misingi ya kiuandishi na weledi katika kuhabarisha jamii juu ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali. Sima ameyasema hayo mkoani Kagera wakati akifungua semina ya waandishi wa habari mkoani Kagera iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhusu miradi inayotekelezwa na Serikali ukiwemo ule wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima – Uganda hadi Chongoleani Tanga – Tanzania. Amesema Wananchi wanategemea kujua yanayoendelea nchini kupitia vyombo vya habari na endapo waandishi wa habari watapotosha habari zao watajenga chuki na taharuki kwa Wananchi dhidi ya Serikali. “Rais Samia Suluhu Hassan anaujua vizuri huu mradi na anaufuatilia kwa karibu hivyo nashukuru kwa kuandaliwa hii semina, naamini wanahabari mtauongelea vizuri mradi huu baada kujua mengi mazuri yatakayotokana na kukamilika kwa mradi huu ikiwemo kukuza uchumi na pato la Taifa”. ameongeza Sima