Sherehe za Maulid

0

Baadhi ya Waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, kushiriki sherehe za Maulid zinazofanyika Kitaifa mkoani humo

Sherehe hizo zinaongozwa na Kaimu Mufti Sheikh Ali Ngeruko, na zitakujia Mbashara kupitia TBC1 na Youtube Channel ya TBConline.

Dkt. Mollel : Huduma za Maabara ni msingi wa Hospitali

0

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema Huduma za maabara ndiyo msingi mkuu wa Hospitali katika kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha.

Dkt. Mollel amebainisha hayo mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro wakati akifungua mkutano wa mwaka wa 36 wa Chama cha wataalamu wa maabara nchini ambapo amesema kuwa kiasi cha Shilingi trilioni 6.7 kilichowekezwa kwenye sekta ya afya nchini asilimia kubwa imelenga kwenda kuboresha Huduma za maabara.

Dkt. Mollel amesema jiwe la msingi katika sekta ya afya ni maabara hivyo serikali itaendelea kuboresha Huduma za maabara katika hospitali zote nchini ili wananchi waweze kupata Huduma bora.

“Hospitali yoyote msingi wake ni maabara ndiyo maana mtaona hivi sasa serikali yetu ya awamu ya sita chini ya uongozi imara wa Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kuwekeza kwenye Huduma za maabara kwa kufunga mashine za MRI, CT Scan na mashine nyine za kupima vimelea vya magonjwa mbalimbali katika hospitali zote nchini”- ameeleza Dkt. Mollel

Amesema maabara ni muhimu sana kwani zimekuwa msaada wakati inapotekea mlipuko wa magonjwa mbalimbali na kusaidia kutambua sambuli kwa wakati.

“Tulipambana na UVIKO-19 watu wa maabara ndiyo walikuwa msaada lakini pia tulipambana na homa ya mgunda watu waliokuwa mstari wa mbele ni wataalam wa Huduma za maabara”- amesisitiza Dkt. Mollel

Aidha amesema lengo la kongamano hilo ni wataalam wa Huduma za maabara nchini kukaa na kujadili kwa namna gani wataboresha huduma hizo ngazi ya taifa hadi ngazi ya msingi.

KIHENZILE AFANYA ZIARA BANDARINI

0

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amefanya ziara yake ya kwanza toka ateuliwe kushika wadhifa huo kwa kutembelea na kukagua baadhi ya bandari zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ambapo amejionea namna shughuli mbalimbali zinavyoendeshwa.

Akiwa katika ziara hiyo Kihenzile amebainisha mambo kadhaa ambayo ni mikakati ya Serikali katika kuchochea kasi ya maendeleo nchini, kupitia bandari.

Mikakati hiyo ni pamoja na kujenga matenki makubwa yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta hadi tani laki tatu na elfu sitini na usimikaji mtambo mkubwa wa kisasa Kigamboni, Dar es Salaam kwa ajili ya kupima kiwango cha mafuta kinachoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Wakati wa ziara hiyo Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile pia amekagua eneo maalum linalotumika
kushusha magari kutoka kwenye meli ambapo kwa siku yanashushwa takribani magari laki tatu na eneo lenye uwezo wa kuhifandi magari elfu sita kwa wakati mmoja.

TPA: NDEGE ZA KITALII ZITATUA BAHARINI

0

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Juma Kijavara amesema, mamlaka hiyo ina mpango wa kutekeleza mradi unaojulikana kama Dynamic Water Front katika bandari ya Dar es Salaam.

Mradi huo utakuwa na gati maalumu la utalii litakaloruhusu ndege kutua au kuanzia safari kwenye maji.

Akiwasilisha taarifa za kuanza kwa mradi huo kwa Naibu Waziri Uchukuzi David Kihenzile, Kijavara amesema moja ya maeneo muhimu katika mradi huo ni pamoja na eneo zitakapotua ndege za kitalii zinazoelekea Zanzibar, Mafia na maeneo mengine nchini.

Ameongesa kuwa pamoja na kuwa na gati maalumu la utalii, mradi huo pia utakuwa na eneo la hoteli kubwa za kisasa, maeneo ya kupumzika na eneo la kuhudumia meli kubwa.

Mradi huo wa Dynamic Water Front utagawanyika katika maeneo makubwa matano ambayo yote yatapatiwa majina ya wanyama wakubwa ambao ni tembo, chui, faru, simba na nyati.

Kijavara amesema mradi huo unaweza kuwa ni mkubwa pekee wenye huduma kama hizo kwa Afrika Mashariki na unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa sasa mradi huo upo katika hatua ya mazungumzo na mwekezaji ambaye watasirikiana kuutekeleza.

TOZO ZA HALMASHAURI KIKWAZO KWA BANDARI KAVU DSM

0

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho ameiomba Serikali kuingilia kati changamoto inayotokana na kutoza ushuru wa maegesho ya magari katika maeneo yanayosimamiwa na bandari ya Dar es Salaam.

Mrisho ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akilitambulisha kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile eneo maalumu litakalojengwa mitambo ya kuhifadhia bidhaa za vyakula zinazoharibika kwa haraka.

Amesema kwa sasa changamoto kubwa inayowakabili madereva wa malori katika bandari kavu za Dar es Salaam ni tozo hizo kutoka halmashauri huku akiitaja halmashauri ya Temeke kuwa ni mojawapo.

Amesema Bandari ya Dar es Salaam tayari inalipa ushuru wa huduma (Service Levy) kwa halmashauri, hivyo ingeendelea kutumia tozo hizo na kuwaacha madereva wa malori kupaki katika bandari hizo bila ya kuongezewa tozo zingine kwani kinachoendelea hivi sasa ni madereva hao kutafuta njia zingine za kukwepa tozo hiyo na kwenda kupaki malori barabarani.

Hivi sasa madereva wa malori wanaoegesha malori katika bandari Kavu Dar es Salaam wanatozwa na halmashauri gharama za kuegesha magari hayo, jambo walilodai kuwa ni kero kwao.

Dkt. Biteko asisitiza upendo na umoja kwa Watanzania

0

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewasisitiza wananchi kushikamana kuwa na umoja pamoja na upendo ili kuweza kuleta maendeleo ya pamoja kwenye jamii na kuacha kufanyiana chuki na kugawanyika kutokana na tofauti mbalimbali zikiwemo za itikadi za vyama, dini, kabila na majimbo.

Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi wa jimbo lake la Bukombe mkoani Geita katika ziara yake mkoani humo.

“Nataka niwaombe tupendane, tuthaminiane. Tofauti tulizonazo zisitufanye tukagawanyika, tuonane sisi ni  Watanzania wa daraja moja. Niwaombe viongozi wa chama cha CCM na madiwani mliopo hapa twendeni tukawaunganishe Watanzania,” amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amefanya ziara wilayani Bukombe mkoani Geita akitokea Geita Mjini alipofungua rasmi Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani humo mpaka Septemba 30, 2023 yatakapofungwa na Rais Samia Suluhu Hassan

Mavunde: Tutafanya utafiti wa madini nchi nzima

0

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Rais Samia Suluhu Hassan amewapa maelekezo wizara hiyo kufanya utafiti wa madini nchi nzima ili kupata taarifa sahihi za upatikanaji wa rasilimali za madini kwa maeneo husika hapa nchini ili kuwarahisishia wachimbaji kufanya shughuli zao katika maeneo sahihi yenye madini.

“Mheshimiwa Rais amenipa maelekezo ya kwamba ni hakikishe tunaendelea na kufanya utafiti [wa madini] Ili wachimbaji wasichimbe madini kwa kubahatisha. Wananchi hawa wanapoteza mitaji yao na nguvu zao kwa sababu hawana taarifa ya madini wanayoyachimba kwa sababu hatujafanya utafiti wa mkubwa kuifikia nchi nzima kubaini rasilimali za madini zilizopo,” amesema.

Aidha, Mavunde ameongeza kuwa, mwaka 2004 ulifanyika utafiti wa madini kwa kurusha ndege kwenye maeneo ya Kahama, Biharamulo, Mpanda na Nachingwea, maeneo ambayo ni sawa na ekari milioni 7 tu kati ya ekari milioni 233 za nchi nzima.

Mavunde ameyasema hayo wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wilayani Bukombe mkoani Geita.