DKT. MWINYI : TUTAENDELEA KUTIMIZA TULIYOYAAHIDI

0

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar,
Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi amesema ataendelea kutimiza ahadi alizowaahidi Wananchi na kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Wenyeviti wa Chama cha Mapinduzi wa mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar waliofika Ikulu Zanzibar leo Agosti 30, 2023.

Aidha, Dkt. Mwinyi amempongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mialiko kwa Wenyeviti hao kuhudhuria Tamasha la Kizimkazi mwaka huu.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi akizungumza kwa niaba ya Wenyeviti hao wa CCM wa mikoa amempongeza Rais Mwinyi kwa mabadiliko ya maendeleo yaliyofanyika Zanzibar chini ya uongozi wake na kuendelea kutekeleza vema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Muhimbili yamnasa Daktari ‘Feki’

0

Mussa Mawa,
Mkazi wa Dar es Salaam amekamatwa katika maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili akituhumiwa kutapeli Wananchi wanaopata huduma kwa kujifanya daktari.

Taarifa iliyotolewa na Hospitali hiyo imeeleza kuwa watendaji wa Idara ya Ulinzi ya hospitali hiyo walimbaini daktari huyo ‘Feki’ akiwa kwenye harakati za kuwatapeli Wananchi wanaouguza ndugu yao aliyelazwa jengo la Mwaisela.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha ametoa rai kwa watu wote wanaojihusisha na kutapeli Wananchi katika eneo la Hospitali hiyo kuacha kufanya hivyo.

Muhimbili yamnasa Daktari ‘Feki’

ELIMU YA KIKOKOTOO KUENDELEA KUTOLEWA

0

Serikali imesema itaendelea kutoa elimu ya kanuni mpya ya mafao ya Pensheni (Kikokotoo) na hadi kufikia Juni 30, 2023 Wanachama wa mifuko ya Pensheni 131,497 na waajiri 5,580 wamefikiwa na elimu hiyo.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Patrobas Katambi amesema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Priscus Tarimo aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuhusu malalamiko ya wastaafu juu ya Kikokotoo kinachotumika kupiga mahesabu na kulipa mafao.

Aidha, amesema elimu hiyo itaendelea kutolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kushirikiana na Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Naibu Waziri Katambi amesema mpango wa Serikali ni kuendelea kuwaelimisha Wananchi hususani waajiri na wanachama wa mifuko hiyo wakiwemo wastaafu kuhusu faida ya kanuni hizo.

Serikali yataka kuharakishwa ujenzi barabara ya Tanga – Pangani

0

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali ipo tayari kukamilisha malipo ya Mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani yenye urefu wa kilomita 50.

Waziri Mbarawa ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami, ambapo ujenzi wake ulianza mwaka 2019 na kutakiwa kukamilika mwaka 2022.

Amesema fedha za kukamilisha ujenzi huo zipo tayari, kinachotakiwa ni kuongezeka kwa kasi ya ujenzi ili ikamilike na kuruhusu Wananchi kuitumia.

Katika hatua nyingine Serikali imetoa shilingi Bilioni nne kwa ajili ya kulipa fidia Wananchi 358 waliopitiwa na mradi huo wa barabara ya Tanga -:Pangani.

Hadi sasa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Tanga umelipa shilingi Bilioni 3.8, huku wengine wakiwa hawajalipwa kutokana na migogoro ya kifamilia.

Pluijm ajiuzulu ukocha Singida BS

0

Kocha Mkuu wa Singida BS, Hans Van der Pluijm amejiuzulu nafasi hiyo baada ya kuitumikia tangu mwaka 2022.

Kufuatia uamuzi huo walima alizeti hao wa Singida watakuwa chini ya Kocha Msaidizi, Mathias Lule mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Singida BS, kocha huyo amejiuzulu kwa kile alichoeleza kuwa anahitaji muda zaidi kwa ajili ya masuala yake binafsi.

Kocha huyo amekuwa na mafanikio makubwa ambapo aliiwezesha timu kumaliza nafasi ya nne katika ligi, kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika na hivi karibuni amewezesha kusonge mbele kwenye mashindano hayo ya Afrika baada ya kuvuka mzunguko wa kwanza.

Dugange arejea Bungeni

0

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange, Leo ameonekana Bungeni jijini Dodoma kwa mara ya kwanza baada kutoonekana kwa kipindi kirefu tangu alipopata ajali ya gari jijini Dodoma Aprili 27, 2023.

Dkt. Dugange leo amejibu maswali bungeni yaliyoelekezwa TAMISEMI katika Bunge la 12 kikao cha kwanza.

Kusajili kushiriki mkutano AGRF mwisho leo

0

Katibu Mkuu wa wizara ya Kilimo Gerald Mweli amesema hadi sasa Marais kadhaa wamethibitisha kushiriki mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) utaofanyika hivi karibuni mkoani Dar es Salaam.

Amesema kwa upande wa Mawaziri zaidi ya asilimia 80 ya matarajio wamethibitisha kushiriki kwenye mkutano huo.mkubwa na usajili unaendelea mpaka baadae hii leo.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati maandalizi ya mkutano huo yakiendelea Mweli
amesema, mpaka sasa nchi imeshavuka lengo la washiriki ambapo lengo lilikuwa ni kufikisha washiriki elfu tatu lakini hadi sasa waliojiandikisha wamezidi na kufikia elfu 4 hivyo wanatarajia kufunga dirisha la usajili leo Agosti 29, 2023.

“Idadi hii ya washiriki inaonesha imani yao kwa nchi yetu, lakini kufikia jitihada hizo ni juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuitangaza nchi kimataifa. Hivyo nitoe rai kwa watu wote wakiwemo wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mkutano huu wa AGRF kwani watapata manufaa makubwa.” Ameeleza Mweli

Amesema Serikali imealika kampuni kubwa zinazojihusisha na kilimo ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara nchini watakaotangaza biashara zao kimataifa.

Aidha, Mweli ameeleza kuwa Tanzania inatarajia kufungua kiwanda cha kuchakata mbolea kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya nchi, ambapo kupitia mkutano huo wa Mifumo ya Chakula 2023 kiwanda hicho kitatangazwa ili kupata soko la Kimataifa.