Rais Samia: Lengo la Tamasha la Kizimkazi ni kurithisha utamaduni

0

Rais Samia Suluhu Hassan amesema lengo la Tamasha la Kizimkazi ni kurithisha utamaduni wa Kusini Unguja kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akihutubia wakati wa hafla ya kilele cha Tamasha la Kizimkazi, Rais Samia amesema mbali na kurithisha utamaduni lakini pia lina lengo kuwaweka pamoja wananchi wa Kusini Unguja na kufurahi kwa pamoja.

“Wajukuu zetu hawajui hata vyakula vyetu wala tamaduni za huku. Tamasha hili lengo lake ni kuwakumbusha na kuwarithisha watoto na vizazi vyetu utamaduni wa watu wa Unguja Kusini,” amesema Rais Samia

Ameongeza kuwa mbali na mambo ya utamaduni lakini pia tamasha hilo limetumika kuzindua na kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuvutia uwekezaji kwenye maeneo ya mkoa wa Kusini na Zanzibar kwa ujumla.

Miradi 12 imezinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika tamasha la mwaka huu ambapo Rais Samia ameshiriki.

Tutawapeleka vijana jando la kisasa, ndoa si mchezo

0

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali inatambua kuwa mtoto wa kiume yupo katika hatari ya kutopata malezi bora, hivyo ipo katika mchakato wa kuandaa mpango wa malezi na makuzi ya watoto kwenye umri wa awali na mpango wa pili wa kuwawezesha na kuwaendeleza vijana balee kuanzia umri wa miaka 10 hadi 19.

“Tutajikita zaidi katika kuongezea nguvu zaidi tuje na programu za kimkakati zinazojikita zaidi kwenye masuala ya watoto wa kiume, zamani watoto wa kiume walikuwa wanapelekwa jando lakini sasa tutakuwa tunawapeleka jando la kisasa na miongozo yao mizuri mizuri inayosema namna ya kuwa baba wazuri ili watakapo balee wajue changamoto watakazokutana nazo kwenye ndoa kwamba ndoa si mchezo.” Amesema Dkt. Dorothy Gwajima na kuongeza kuwa

“Ni kweli kabisa tunatambua kuwa mtoto wa kiume tofauti na awali anakumbwa na changamoto nyingi sana zitokanazo na mmonyoka wa maadili, anakosa malezi na makuzi bora kiasi kwamba sasa hata akijakuwa baba atashindwa kuwa baba mzuri wa kupambana na changamoto za familia.”

Dkt. Gwajima ameyasema hayo Bungeni, Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe ambaye amehoji mpango wa Serikali katika kulinda na kumjengea mtoto wa kiume uwezo.

“Hivi karibuni kumeibuka utamaduni wa kumtetetea mtoto wa kike lakini tunao utamaduni wetu ambao mtoto wa kiume ni baba au kiongozi wa familia. Je, serikali ina mpango gani wa kumjengea uwezo mtoto wa kiume.” amehoji Mbunge Saashisha

Dkt. Gwajima : Ni ukatili kuwekeza mke akiwa tumboni kwa mama yake

0

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali inatambua kuna mila zenye faida ambazo zinapaswa kuendelezwa na mila zenye kuleta madhara ikiwemo mila ya kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama.

“Mila hii ina madhara kwa kuwa inachochea ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni na inamnyima mhusika haki yake ya msingi ya kumchagua mwenza wa kuishi naye umri utakapofika.” amesema Dkt. Gwajima

Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mary Mwinyi aliyehoji Serikali ina mpango gani wa kufuatilia mila potofu za kuwekeza mke akiwa tumboni mwa Mama hasa katika mikoa ya Manyara na Arusha.

Msitume nyaraka ‘WhatsApp’ ni marufuku

0

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete amesema sheria inayosimamia nyaraka za Serikali inaelekeza kuwa mawasiliano ya Serikali yafanyike kwa njia ya barua na si vinginevyo.

Kufuatia kuwepo kwa sheria hiyo, Naibu Waziri Kikwete amewaonya watendaji wa Serikali ambao wanatumia njia ambazo sio rasmi kutuma nyaraka.

“Haitokuwa sawa na ni marufuku ya Serikali kuwasilisha au kutumiiana ‘Documents’ za Serikali kupitia njia ya WhatsApps na njia nyingine zisizo rasmi, isipokuwa kwa maelekezo ambayo yatakuwa yametolewa vinginevyo katika mamlaka,” amesema Naibu Waziri Ridhiwani Kikwete.

Ameyasema hayo Bungeji jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Janejelly Ntate James ambaye amehoji uhalali wa matumizi ya makundi ya WhatsApp kutumiana nyaraka.

Aidha, Naibu Waziri Kikwete amelihakikishia Bunge kuwa Serikali bado inaendelea kutengeneza mifumo mbalimbali ambayo itaileta Serikali yote katika adabu ya utendaji.

JKT Queens yatwaa ubingwa wa CECAFA

0

Timu ya JKT Queens kutoka Tanzania imeshinda ubingwa Ligi ya Mabingwa ya CECAFA kwa Wanawake baada ya kuifunga CBE Women ya Ethiopia kwa mikwaju ya penati.

Miamba hiyo ilikwenda dakika 120 bila kufungana na hivyo mikwaju ya penati ikaamuliwa kama njia ya kumpata bingwa ambapo JKT Queens imeshinda kwa penati 5-4.

Kufuatia ushindi huo, JKT Queens ndio itakayouwakilisha ukanda wa CECAFA kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ya CAF kwa Wanawake.

Mashindano hayo yatafanyika Novemba 2023 nchini Ivory Coast.

Kigezo cha Tanzania kuwa mwenyeji Mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika AGRF chatajwa

0

Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Gerald Mweli amesema kigezo cha Tanzania kuwa na sifa ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) ni utayari wake katika kuendesha agenda ya chakula kwa ajili ya dunia.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari mkoani Dar es Salaam Mweli amesema pamoja na nchi kuonekana kuwa na utayari huo ulioipa sifa ya kuwa mwenyeji wa AGRF, Serikali imeongeza bajeti katika Sekta ya kilimo kutoka shilingi Bilioni 298 kwa mwaka wa fedha uliopita hadi shilingi Bilioni 970 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Amesema bajeti iliyoongezwa imepangwa kutumika katika maeneo muhimu akiyataja kuwa ni umwagiliaji, utafiti, mbegu na ushiriki katika kilimo kwa vijana na wanawake.

Kwa upande mwingine Mweli amesema Serikali itaweka miondombinu ya muda mrefu kwa ajili ya kutoa huduma ya umwagiliaji na kuwajengea uwezo maafisa ugani na wakulima.

Tanzania yaifuata Algeria na matumaini ya kufuzu AFCON

0

Timu ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanaume, Taifa Stars, imeondoka nchini leo kuelekea Tunis, Tunisia kwa Kambi ya kujiandaa na mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu AFCON dhidi ya Algeria.

Mchezo huo utakaochezwa Septemba 7, 2023 nchini Algeria ikikumbukwa kuwa mchezo wa kwanza Tanzania ilipoteza 2-0.

Tanzania ipo kundi F pamoja na Uganda na Niger ambapo (Tanzania) inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 7 baada ya michezo mitano.

Tanzania inahitaji walau alama moja kwenye mchezo huo ili kujihakikishia nafasi kwenye mashindano hayo Afrika ambapo itafikisha alama nane ambazo haziwezi kufikiwa na Uganda yenye alama nne.

Endapo Tanzania itafungwa kwenye mchezo huo, matumaini yake ya kufuzu yatabaki kwa kuiombea Niger iifunge Uganda, au hata Uganda ikishinda, isishinde kwa tofauti ya magoli zaidi ya mawili.