Jengo la PAPU kuzinduliwa Arusha

0

Rais Samia.Suluhu Hassan, Kesho Septemba 02, 2023 anatarajiwa kuzindua jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Aftika (PAPU), lililopo mkoani Arusha.

Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela amesema jengo hilo ambalo ni la kisasa litatoa huduma za kiushindani wa kisayansi na kiteknolojia.

Amewataka wakazi wa jiji la Arusha kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo.

Doto Cup yaleta msisimko Geita

0

Timu ya soka ya Butizya FC ya mkoani Geita imeingia hatua ya fainali baada ya kuifunga timu ya Runzewe Academy magoli 4 bila, katika michuano ya Doto Cup iliyofanyika katika uwanja wa mpira wa shule ya sekondari ya Ushirombo.

Mwemyekiti wa kamati ya mashindano ya Doto Cup Nelvin Salabaga amesema, ligi hiyo inayodhaminiwa na Mbunge wa jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko imekuwa na msisimko mkubwa na vijana wengi wamejitokeza kwa ajili ya kushiriki.

Baadhi ya wachezaji wamesema kucheza katika michuano ya Doto Cup kunaibua vipaji vyao na kwamba
watu wengi wanajitokeza kuwaangalia na wanatarajia kuchukuliwa kwenda kucheza sehemu zingine ambapo watapata ajira.

Tangu ilipoanzishwa mwaka.2016, Michuano ya Doto Cup imekuwa ikifanyika kila mwaka.

Rapa Kontawa asalimisha sare JWTZ

0

Rapa wa muziki wa Tanzania @kontawaa amejisalimisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kurudisha mavazi ya Jeshi aliyokuwa akiyatumia.

@kontawaa amerejeshe mavazi hayo zikiwa zimepita siku chache baada ya JWTZ kuwataka Wasanii wanaotaka kutumia sare za Jeshi hilo kwenye kazi zao kufuata utaratibu wa kuomba kibali ili waruhusiwe kutumia mavazi hayo, huku likitoa siku saba kuanzia Agosti 24,2023 kwa Wananchi kusalimisha mavazi ya Jeshi au yanayofanana na sare za Jeshi.

Tangazo hilo la JWTZ lilitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu Luteni Kanali Gaudentius llonda.

“Tunatoa siku saba kuanzia leo iwe mwisho wa kuyavaa, kuyatumia au kuyauza, kwa wale Wasanii wao watafuata utaratibu wa kuomba kibali ili waruhusiwe kutumia mavazi hayo, baada ya siku saba atakayekutwa na mavazi hayo atachukuliwa hatua kali ambayo itakuwa fundisho kwa wengine,” Alionya Luteni Kanali llonda.

Yafahamu majukumu ya msingi ya JWTZ

0

• Kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

• Ulinzi wa Mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

• Kufanya Mafunzo na Mazoezi ili kujiweka tayari Kivita wakati wote.

• Kufundisha umma shughuli za Ulinzi wa Taifa.

• Kushirikiana na Mamlaka za Kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa maafa.

• Kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

• Kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani Kimataifa.

Chanzo: Tovuti ya JWTZ

Je!, Wajua sifa za kujiunga na JWTZ?

0

Utaratibu wa kujiunga na JWTZ

Uandikishaji

Mtu yeyote ataandikishwa kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa sifa zifuatazo:

Awe raia wa Tanzania

Awe na Elimu ya kidato cha nne na kuendelea na awe amefaulu

Awe hajaoa/hajaolewa

Awe na umri kuanzia miaka 18 hadi 25

Awe na tabia na mwenendo mzuri

Awe na akili timamu na afya nzuri

Masharti ya Utumishi

Askari atapewa nambari ya utumishi baada ya kufaulu mafunzo ya awali.

Atalitumikia Jeshi kwa kipindi cha mwanzo cha miaka sita, baada ya hapo atafanya kazi kwa mkataba wa miaka miwili miwili kwa kibali cha Mkuu wa Majeshi.

Maafisa

Bodi ya Uteuzi wa Maafisa (Officers Selection Board)
huwafanyia usaili Askari wenye elimu ya kidato cha sita na kuendelea toka Vikosini na Shule za Askari wapya (Recruitment Schools).

Watakaofaulu masailiano hayo hupewa hadhi ya Afisa Mwanafunzi (Officer Cadet), na hupelekwa Chuoni (Tanzania Military Academy) kwa mafunzo ya Uafisa kwa muda wa mwaka mmoja.

Chanzo: Tovuti ya JWTZ

Wafahamu wakuu wa majeshi Tanzania 1964 – 2023

0

Wakuu wa Majeshi waliopita
mwaka 1964 hadi 1974 ni Jenerali Mirisho Sarakikya

Mwaka 1974 hadi 1980 ni Jenerali Abdalah Twalipo.

Mwaka 1980 hadi 1988 ni Jenerali David Musuguri.

Mwaka 1988 hadi 1994 ni Jenerali Mwita Kiaro.

Mwaka 1994 hadi 2001 ni Jenerali Robert Mboma.

Mwaka 2001 hadi 2007 ni Jenerali George Waitara.

Mwaka 2007 hadi 2017 ni Jenerali Davis Mwamunyange.

Mwaka 2017 hadi 2022 ni Jenerali Venance Mabeyo.

Mwaka 2022 hadi sasa ni Jenerali Jacob Mkunda.

Chanzo: Tovuti ya JWTZ

Mkurugenzi Arusha ahukumiwa miaka 20 jela

0

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewahukumu aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dkt. John Pima na wenzake wawili kifungo cha miaka 20 jela baada ya kukutwa na makosa ya uhujumu uchumi.

Hukumu hiyo imetolewa leo Agost 31, 2023 na Hakimu Seraphin Nsana, katika kesi namba 5/2023 ya uhujumu uchumi, iliyokuwa inawakabili Dkt. Pima, aliyekuwa Mweka Hazina wa jiji la Arusha, Mariam Mshana na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji, Innocent Maduhu.

Akisoma hukumu hiyo mbele ya mahakama hiyo, Hakima Nsana amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imewatia hatiani washtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa inawakabili.

“Kwa kuzingatia maombi ya mawakili wa upande wa washtakiwa, ikiwemo kutokuwa na rekodi ya makosa ya nyuma, utegemezi wa familia na ushirikiano mlioutoa katika kipindi chote cha uendeshaji wa kesi hii, mahakama inawapa adhabu ya kutumikia miaka 20 jela huku miezi 14 mliokuwa kizuizini ikizingatiwa.”
Amesema Hakimu Nsana.

Mbali na hilo, washtakiwa wana haki na nafasi ya kukata rufaa katika Mahakama Kuu endapo hawajaridhika na hukumu hiyo.

UWAMATA : Kamchape ni matapeli

0

Umoja wa Waganga wa Tiba Asilia, Tiba Mbadala na Wakunga wa Jadi nchini (UWAMATA) umesema kikundi cha watu wanaojiita Kamchape kwa madai ya kuwachapa wachawi mkoani Kigoma ni cha Matapeli waliyojivika kofia ya uganga.

Akizungumza katika uzinduzi wa ofisi ya chama hicho mkoani Kigoma,
Mwenyekiti wa
UWAMATA Taifa Mohamed Fundikila amesema, vitendo vinavyofanywa na watu hao havipaswi kufumbiwa macho, kwani ni udanganyifu na uchonganishi ambao unaweza kusababusha uvunjifu wa amani kwa jamii.

Aidha, Fundikila ameliomba Jeshi la Polisi kuendelea kuwasaka watu hao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, huku akiwasisitiza Wananchi kutokubali kudanganyika.

Kwa upande wake Katibu wa Umoja huo mkoa wa Kigoma, Haruna Shaban na baadhi ya Waganga wamesema wanashangazwa na vitendo hivyo kwani hata namna vinavyofanyika ni tofauti kabisa na taratibu za matibabu ya tiba za asili.

Kauli ya UWAMATA
inakuja zikiwa zimepita siku chache baada ya kuibuka kwa kikundi cha watu ambao wanajiita kamchape na wengine Lambalamba ambao wanapita katika maeneo ya vijijini mkoani Kigoma wakichapa watu kwa tuhuma za ushirikina.