Afrika tutumie tafiti kwenye kilimo

0

Nchi za Afrika zimetaikiwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Ili kuepuka uhaba wa mazao kwa wananchi wake.

Hayo yamesemwa na Rais Mstaafu wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete wakati akichangia mada kwenye Mkutano wa mifumo ya Chakula barani afrika unaoendelea mkoani Dar es salama ambapo wadau mbalimbali wameshiriki.

Dkt. Kikwete amesema kutokana na mabadiliko ya tabianchi hali sio nzuri na kuzitaka Serikali za matafita ya Afrika kuweka mkazo kwenye tafiti ili kujua mazao yanayoweza kustahimili eneo husika na kuleta tija.

“Mimi ni mkulima mdogo nimewahi kulima hekari 40 mvua ikagoma, nikalima hekari 20 zikagoma nikalima Tena hekari 5 mvua haikutosha pia, lakini naipongeza Serikali ya sasa imekuja na utafiti ambao unasaidia mkulima kujua sehemu sahihi ya kulima zao linaloendana na eneo husika” – amesema Kikwete.

Serikali yaandaa mpango wa Kilimo Biashara 2024 – 2030

0

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe
amesema Wanawake Milioni 1.6 watafikiwa na Mpango wa Kilimo Biashara na kuwezeshwa kwa miaka sita kuanzia 2024 – 2030,, na hivyo kuwa na uwezo wa kufanya uzalishaji mkubwa.

Waziri Bashe ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika na kuhudhuriwa na wadau.mbalimbali wa chakula.

Amesema kwa kuwa Tanzania imekusudia kulisha Dunia, hivyo imejiwekea mipango thabiti ya kuwezesha vijana na Wanawake kwa kuwapatia mikopo.

Waziri Bashe amesema Kilimo Biashara kitasaidia kuzalisha ajira kwa vijana wengi ambao watakuwa wamejiunga kwenye makundi mbalimbali.

IFIKAPO 2025 ROBO TATU YA MBEGU ZIZALISWE NCHINI

0

Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kwamba kufikia mwaka 2025 Serikali ya Tanzania imejidhatiti kuhakikisha kuwa robo tatu ya mbegu zinazotumika nchini zinazalishwa ndani ya nchi.

Rais amesema hayo alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa washiriki, hususan vijana, katika Mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa wa Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Rais Samia ameeleza kuwa mbegu hizo zimethibitishwa na zinajulikana kwa uwezo wake wa kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa na pia kuzingatia mahitaji ya udongo wa wakulima. Hii inalenga kuboresha uzalishaji wa kilimo nchini Tanzania na kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima.

Pamoja na hayo, Rais amegusia jinsi teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) inavyotumika kuboresha sekta ya kilimo. Amebainisha kuwa TEHAMA inatumika kwa ufanisi katika masuala ya umwagiliaji, ikisaidia kuhakikisha mmea unapata maji sahihi kwa wakati unaofaa.

Rais Samia pia amefafanua kuwa TEHAMA itaingia katika mchakato wa uhifadhi wa mazao ya wakulima. Serikali itajenga miundombinu ya kisasa kwa ajili ya kuhifadhi mazao haya, na kutumia teknolojia kuweka uwiano wa unyevu katika nafaka. Hatua hii itasaidia kuzuia tatizo la sumu kuvu katika nafaka na kuhakikisha ubora wa mazao.

Kwa kuongezea, Rais Samia ametaja matumizi ya TEHAMA katika kufuatilia masoko ya mazao. Pia, amebainisha kwamba mashamba yataandaliwa kwa kutumia teknolojia ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji. Hii itawawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika kilimo na kutumia vifaa vya kisasa, ikiwa ni pamoja na zana za kiotomatiki, kufanya kazi kwa ufanisi.

Aidha, Rais ameongeza kuwa maafisa wa kilimo (maafisa Ugani) wamewezeshwa kwa vifaa maalumu kwa ajili ya kupima afya ya udongo. Huduma hii ya upimaji itatolewa kwa kila mkulima mara kwa mara ili kusaidia wakulima kuchagua aina sahihi za mbolea na mbegu za kutumia, na hivyo kuboresha uzalishaji katika sekta ya kilimo.

JITIHADA ZA SERIKALI KUTAFUTA SOKO LA MAZAO YA TANZANIA

0

Rais Samia Suluhu Hassan amekiri kuwepo kwa changamoto ya masoko ya bidhaa zinazozalishwa, lakini Serikali imefanya tafiti na kugundua kuwa kinachopelekea changamoto hizo ni kutofahamu mahitaji halisi ya soko la ndani na nje ya nchi, muunganiko wa soko la bidhaa pamoja na mkulima.

Amesema hayo alipokuwa akijibu swali kutoka kwa kijana aliyehudhuria Mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano Julius Nyerere (JNICC) swali lililohitaji kufahamu ni kwa namna gani Serikali ya Tanzania inatatua changamoto na kuhamasisha upatikanaji wa masoko na uongezaji thamani kwa bidhaa zinazozalishwa na vijana.

Rais Samia amesema katika suala la muunganiko wa soko na mkulima, Serikali imeanza kuweka jitihada hizo kwa baadhi ya mazao kama korosho ambapo imekuwa na matokeo chanya kwa kusaidia kupandisha bei ya korosho kwa kumjengea mkulima ushirika wa moja kwa moja wa soko la bidhaa hiyo kwa kumuondoa mtu wa kati [dalali].

Amesema kwa sasa wanunuzi wananunua korosho kutoka kwenye vyama vya ushirika vya wakulima hivyo wakulima wanapata fursa ya kushindanisha bei, jambo ambalo limepelekea bidhaa hiyo kupanda bei. Rais Samia ameitaja bidhaa ya mbaazi pia ikiwa moja ya bidhaa ambazo zimefanikiwa kupata soko zuri kutokana na jitihada hizo.

Vilevile Rais Samia amesema jitihada zingine Serikali inazochukua ni kuboresha miundombinu ya usafirishaji kwa kujenga barabara zinazounganisha mikoa-mikoa, mikoa -wilaya zake na barabara kuu na nchi za Jirani ili kuyafikia masoko ya nchi jirani kwa kusaidia mazao kutolewa shambani.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zinakwenda sambamba na kuboresha bandari zilizopo nchini akiitaja bandari ya Dar es Salaam, Zanzibar, Tanga na Mtwara.

Amesema Serikali inajenga eneo maalumu la kuhifadhi mazao yanayoharibika kwa haraka ili wakati yanasubiri usafiri yaweze kupata hifadhi.

Sambamba na hilo, amesema Serikali imenunua ndege ya mizigo iweze kusafirisha mazao yanayoharibika kwa haraka [Hotculture] kwani ndege hiyo itasafiriaha mazao na kuyapeleka nje jambo ambalo litaepusha kutumia usafiri wa jirani ambao unaweza kuwa na changamoto nyingi ikiwemo za kubadilisha umilika wa bidhaa hizo.

Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa Serikali inasaidia kutafuta waongeza thamani kwa mazao ambayo yamepatikana ili yanapoingia sokoni yawe yamekwisha chakatwa.

Tanzania yafanya vizuri kwenye kilimo biashara

0

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amesema Tanzania imeanza kufanya vizuri katika sekta ya Kilimo Biashara, hasa baada ya kuwa na mpango wa kuwawezesha Wanawake na Vijana katika kufanya shughuli hizo.

Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo mkoani Dar es Salaam ambapo mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika unaoendelea na kujumuisha wadau wa chakula kutoka Afrika na nje ya Bara hilo.

Amesema kumekuwa na ongezeko la Wanawake na Vijana kushiriki katika shughuli za Kilimo Biashara, jambo ambalo ni ishara ya mafanikio ya Tanzania katika kufikia malengo ya kuilisha Dunia.

Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa pamoja na mafanikio yaliyoanza kuonekana bado kuna changamoto katika upatikanaji wa mitaji na teknolojia ya kisasa katika kufanya Kilimo Biashara.

“Mkutano huu unalenga kuhamasisha Mpango wa BBT ambao unalenga kuzalisha mazao ya chakula na mifugo na upatikanaji wa soko ya uhakika nje ya Tanzania ili Wanawake na Vijana wawe na taswira chanya kwenye Kilimo Biashara” Amesema Dkt. Mwinyi

RAIS SAMIA KUZUNGUMZA NA VIJANA WA AFRIKA

0

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwahutubia vijana wa Afrika kupitia mkutano utakaofanyika mkoani Dar es Salaam ambapo pia atapokea taarifa ya namna vijana wa bara hilo wanavyojihusisha na kilimo na wanavyotumia fursa mbalimbali za kilimo.

Pia atazungumzia mwelekeo sahihi wa Bara la Afrika katika kusaidia eneo la vijana kupata ajira kupitia sekta ya kilimo.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam kunapofanyika mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema mkutano huo utafanyika hapo kesho.

Ameongeza kuwa hadi sasa Marais saba wa Afrika wamethibitisha kushiriki katika mkutano huo wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF).

BENKI YA DUNIA YAISHIKA BEGA TANZANIA

0

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema Tanzania imepata mkopo wa Dola Milioni miatatu za Kimarekani sawa na zaidi ya shilingi Bilioni miasaba kutoka Benki ya Dunia, fedha zitakazotumika kwa ajili ya kuboresha sekta ya Kilimo nchini.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Programu ya Uvumilivu wa Mifumo ya Chakula Tanzania Waziri Bashe amesema, Programu hiyo imepangwa kutekelezwa kwa muda wa miaka mitano, hivyo ataweka jitihada zaidi ikamilike ndani ya miaka mitatu.

Ameongeza kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye maeneo walipo Wakulima wadogo.

Aidha, Waziri Bashe amesema moja ya matokeo ya programu hiyo ni kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwa zaidi ya hekta elfu 37 na hivi sasa wizara hiyo imekwishaanza upembuzi yakinifu kwa ajili ya programu hiyo.