Vifaa vya kujipima ukimwi mil 1.6 vyasambazwa

0

Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI hadi sasa imeweza kusambaza vifaa vya mtu kujipima mwenyewe maambukizi ya Virusi vya UKIMWI zaidi ya Milioni 1.6 kuanzia Mwaka 2021 nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwenye kilele cha Mdahalo wa Kitaifa wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ambapo Mgeni rasmi alikua ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.

Waziri Ummy amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI itaendelea kuongeza nguvu za kusambaza vifaa hivyo vya watu kujipima wenyewe Virusi vya UKIMWI ili kuweza kutambua hali zao wenyewe na kwa haraka kuhusu ugonjwa huo.

Waziri Ummy amebainisha kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kupanua wigo wa vituo vya kupima na kutoa huduma za matunzo (CTC) kwa watu wenye UKIMWI ambapo hadi sasa kuna vituo 8,529.

“Nitoe rai kwa watu wote wanaoishi na VVU kuzingatia matumizi sahihi na endelevu ya dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI ili kuweza kujilinda wao wenyewe lakini pia kuwalinda wengine”- amesisitiza Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa huduma za kupima, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU hapa nchini ili vituo vyote vinavyotoa huduma za Afya viwe pia na vituo vya kupima na kutoa matunzo (CTC) kwa 95% ifikapo Mwaka 2025.

Wadaiwa sugu TBA kikaangoni

0

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameagiza Wakala wa Majengo (TBA), kuhakikisha inakusanya deni la Shilingi Bilioni 81.5 wanazodai kwa wapangaji wao sambamba na kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba hizo  ili upatikanaji wa fedha hizo uweze kusaidia utekelezaji wa miradi mingine nchini.

“TBA simamieni sheria kwa yeyote asiyelipa kodi hata kama ni kiongozi, waandikieni notisi ya kulipa madeni yao na wasipolipa waondoeni, wapo wengine nje wanasubiri wapewe nyumba ili waweze kulipa kodi kwa wakati na tutatumia makusanyo hayo kujenga nyumba nyingine”,- amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameyasema mkoani Dodoma wakati alipofanya ziara yake kwa mara ya kwanza katika ofisi hizo na kuzungumza na menejimenti ya TBA ambapo amesisitiza uwekezaji wenye tija kwa watumishi na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Bashungwa ameagiza TBA kuhakikisha wanakuja na mikakati itakayosaidia kujenga nyumba za bei nafuu hasa kwa vijana wanaoajiriwa katika utumishi wa umma hususan Dodoma ili kuweza kumudu gharama za maisha.

AGIZO LA WAZIRI MKUU KUHUSU UHABA WA MAFUTA ‘WIKI MOJA’

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko kuendelea kufuatilia, kutatua na kupata ufumbuzi wa tatizo la mafuta nchini.

“Nikiri kwamba ni kweli tunayo changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini kwa sababu kuna vituo katika maeneo mbalimbali vinakosa mafuta na Watanzania wanalalamika. Zipo jitihada zinafanywa na Serikali kupitia mifumo yetu ya mafuta, wizara ….. na sisi tunajua umuhimu wa nishati hii…..Tumeanza kumuona Naibu Waziri Mkuu (Dkt. Biteko) akifanya vikao kadhaa, kwa kuwa ameshaanza hii kazi niendelee kumuagiza aendelee na hili, muhimu nishati hii ipatikane nchini, ndani ya wiki moja tutakuwa tumeshapata majibu .” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Ametoa agizo hilo Bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, alipokuwa akijubu swali la Mbunge wa jimbo la Mlalo, Tanga, Rashid Shangazi aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya bei pamoja na upatikanaji wa mafuta nchini.

VIONGOZI WA AFRIKA KUFANYA TATHMINI YA VIPAUMBELE

0

Akihutubia mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) mkoani Dar es Salaam, Rais Samia Suluhu Hassan amependekeza Viongozi wa Afrika kufanya tathmini ya vipaumbele vilivyopo katika nchi zao ili kuleta suluhisho la changamoto zinazohusu mifumo na usalama wa chakula.

Rais Samia amesema ili kufikia lengo la kujadili kadhia za mifumo ya chakula na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuendeleza minyororo ya thamani za bidhaa za kilimo na kujadili mipango ya kuimarisha usalama wa chakula barani Afrika, viongozi wa Afrika hawana budi kufanya tathmini ya vipaumbele vyao na kuvinasibisha na mahitaji ya sasa katika muktadha mpana wa kidunia.

Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo kutawezesha kuyafikia mageuzi yanayohitajika katika mifumo ya chakula na kuifanya sekta ya kilimo kuifikia Afrika inayotazamiwa.

Mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) ulioanza Septemba 05, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) utahitimishwa Septemba 08, 2023.

HII NI AIBU NA HAIKUBALIKI

0

Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyeji wa mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) amesema, ni aibu na ni hali isiyokubalika kuelezwa kuwa katika Bara la Afrika wapo watu wanaofariki dunia kwa kukosa chakula.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) unaohudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi za Afrika na wadau wa mifumo ya chakula Barani Afrika Rais Samia amesema, inakadiriwa kuwa zaidi ya Waafrika Milioni 283 wanalala na njaa kila siku na wengine wanapata utapiamlo na magonjwa yanayohusiana na lishe huku wengine wakifariki dunia kwa kukosa chakula.

Amesema kutokana na utajiri wa maliasili na fursa zilizopo Barani Afrika, bara hilo lilipaswa kutoa suluhisho kwa changamoto ya mifumo ya chakula duniani kwani Afrika imebarikiwa kwa kuwa na asilimia 65 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani na watu wake asilimia 60 ni vijana ambao ni nguvu kazi kubwa.

Rais Samia ameongeza kuwa Afrika imebarikiwa kwa kuwa na maji mengi katika mito na maziwa makubwa, pamoja na madini yanayoweza kutoa fedha za kutosha kuwekeza katika sekta ya kilimo.

Amesema licha ya nchi za Afrika kuwa na yote hayo, zimebaki kuwa walalamikaji badala ya kutafuta suluhisho la kuelekea njia ya kuleta Mapinduzi ya uchumi wa kijani.

KIKWETE AMTANGAZA MSHINDI WA TUZO YA CHAKULA AFRIKA

0

Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Chakula Afrika Dkt. Jakaya Kikwete ameitangaza Taasisi ya Kutafiti Mbegu za Maharage ya kutoka nchini Kenya ya PABRA kuwa mshindi wa Tuzo ya Chakula Afrika kwa mwaka 2023.

Dkt. Kikwete ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Tanzania
amemtangaza mshindi huyo mkoani Dar es Salaam, kando ya mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika.

PABR imefanikiwa kuvumbua mbegu za maharage aina 650 ambapo kati yake zipo zenye sifa ya kuzaa mazao mengi, zinazohimili mabadiliko ya tabianchi hasa katika mazingira ya joto na zipo zenye lishe ya kutosha.

Tuzo hiyo ya Chakula Afrika kwa mwaka 2023
ina thamani ya Dola Laki Moja za Kimarekani ambazo ni sawa na shilingi Milioni 250 na mshindi huyo atakabidhiwa tuzo hiyo baadaye hii leo na Rais Samia Suluhu Hassan

Dola Mil 10 za USAID kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi

0

Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) limetangaza uwekezaji mpya katika miradi miwili wenye thamani ya Dola Milioni 10 za Kimarekani, ili kulinda ikolojia muhimu na kupunguza gesi ukaa nchini.

Uwekezaji huo umetangazwa na Naibu Kiongozi Mkuu wa USAID, Isobel Coleman.

Fedha hizo zinajumuisha kiwango cha awali cha Dola Milioni 8 za Kimarekani za uzinduzi wa mradi wa USAID Tumaini kupitia vitendo, ambao ni wa miaka mitano unaoendeshwa kwa ubia na Taasisi ya Jane, na Dola Milioni 2.1 za Kimarekani kwa ajili ya kuboresha uwezo wa jamii za Pwani na wavuvi wa Tanzania katika kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi kama sehemu ya mradi unaoendelea wa USAID Heshimu Bahari.

Agizo la  Waziri Mkuu  kuhusu uhaba wa mafuta ‘wiki moja’

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko kuendelea kufuatilia, kutatua na kupata ufumbuzi wa tatizo la mafuta nchini.

“Nikiri kwamba ni kweli tunayo changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini kwa sababu kuna vituo katika maeneo mbalimbali vinakosa mafuta na Watanzania wanalalamika. Zipo jitihada zinafanywa na Serikali kupitia mifumo yetu ya mafuta, wizara ….. na sisi tunajua umuhimu wa nishati hii…..Tumeanza kumuona Naibu Waziri Mkuu (Dkt. Biteko) akifanya vikao kadhaa, kwa kuwa ameshaanza hii kazi niendelee kumuagiza aendelee na hili, muhimu nishati hii ipatikane nchini, ndani ya wiki moja tutakuwa tumeshapata majibu .” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Ametoa agizo hilo Bungeni jijini Dodoma wakati wa kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, alipokuwa akijubu swali la Mbunge wa jimbo la Mlalo, Tanga, Rashid Shangazi aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya bei pamoja na upatikanaji wa mafuta nchini.