Waziri Nape: Huduma za mawasiliano zibadilishe maisha ya watu

0

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametaka huduma za mawasiliano zinazotolewa kwa jamii ziwe zenye kutoa matokeo chanya na kubadili maisha ya watu.

Waziri Nape ameyasema hayo wakati akifunga Kongamano la Connect 2 Connect (C2C) lililofanyika Zanzibar.

“Tunataka tuondoke kwenye kuweza kumuunganisha mtu na huduma za mawasiliano tu, na kufanya huduma hizo ziwe na matokeo chanya kwenye maisha ya watu”.- amesema Waziri Nape.

Pia, ameipongeza kampuni ya Extensia Limited kwa kuandaa kongamano hilo kubwa lililokutanisha wadau mbalimbali wa TEHAMA kutoka barani Afrika.

Chanjo ya Polio kutolewa kwenye mikoa sita

0

Wizara ya Afya kwa kushirikiana Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inatarajia kuendesha kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio kwa watoto zaidi ya Milioni tatu nchini, walio na umri wa chini ya miaka 8.

Watoto watakaopatiwa chanjo hiyo ni wa mikoa ya Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya.
 
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kampeni hiyo itaanza Septemba 21 hadi 24, 2023.
 
Tanzania inaendesha kampeni hiyo ya chanjo kutokana na wizara ya Afya kupokea taarifa Mei 26, 2023 za uwepo wa mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi na moja ambaye alionesha dalili za kupooza kwa ghafla katika manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Uchunguzi wa Maabara ulithibitisha kuwa mtoto huyo ana maambukizi ya virusi cha Polio. 

Waziri Ummy amesema maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Polio yametolewa taarifa pia katika nchi zinazopakana na Tanzania.

Mifumo ya chakula na mazingira

0

Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kikao kilichohusisha wadau wa mazingira kando ya mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika unaofanyika mkoani Dar es Salaam, ambao wamejadili mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya Tabianchi na namna ya kukabiliana na changamoto zake.

Kikao hicho pia kimepokea maoni, mapendekezo na mchango kutoka Tanzania ambayo imewakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo.

Miongoni mwa mapendekezo ya Tanzania ni kuyataka mataifa ya Afrika kuachana na kilimo cha mazoea na kuwekeza zaidi kwenye utafiti Ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Mwigulu: Changamoto ya upatikanaji wa dola inatatuliwa

0

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mipango ya Serikali katika kupunguza athari na changamoto za upatikanaji wa fedha za kigeni ni pamoja na kuimarisha sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi na kuongeza kiwango cha kuuza fedha za kigeni katika soko la pesa za kigeni.

Amesema kati ya Machi 2022 na Agosti 2023 Benki Kuu ya Tanzania iliuza zaidi a Dola Milioni 500 za Kimarekani.

“Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za muda mfupi na mrefu katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa pesa za kigeni hasa dola za Kimarekani hapa nchini”. amesema
Waziri Nchemba

Ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Era Chiwelesa aliyeuliza kuhusu mpango wa Serikali katika kunusuru uchumi wa nchi kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni hususani Dola za Kimarekani.

Wajawazito wanaokunywa pombe washtakiwe

0

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii wa Afrika Kusini, Hendrietta Bogopane-Zulu amesema,
Wajawazito wanaokunywa pombe wanapaswa kushtakiwa kwa uhalifu, kutokana na pombe kuathiri ubongo wa mtoto aliye tumboni.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuongeza uelewa juu ya athari za unywaji wa pombe kwa Wajawazito, Naibu Waziri Hendrietta amesema ni vema hatua hiyo ikachukuliwa kutokana na matumizi ya pombe kwa Wajawazito kuongezeka nchini Afrika Kusini.

Madhara mbalimbali yanaweza kumpata mjamzito na mtoto aliye tumboni endapo mama huyo anakunywa pombe.

Madhara hayo ni kama;

-Kuwa na kumbukumbu hafifu

-Kupata matatizo ya kuona na kusikia

-Kupata matatizo ya moyo, figo na mifupa

-Kuwa na uwezo mdogo wa kuelewa

Je! Una ushauri gani kwa wajawazito kuhusu matumizi ya pombe?

WASHINDANE KWA PROPOSAL TUWAPE TREKTA

0

Akipokea trekta lililokabidhiwa kwa Serikali kutoka kampuni ya Kimataifa ya wauzaji wa matrekta ya JOHN DEERE, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema ili kuwakabidhi vijana trekta hilo umeandaliwa utaratibu wa kutangaza mashindano ili kumpata mshindi.

Bashe ameeleza kuwa utaratibu huo wa kumpata mshindi utahusisha mashindano ya vikundi vya vijana ambavyo vitatakiwa kuwasilisha andiko la wazo la biashara wanayotaka kufanya katika sekta ya Kilimo kuendana na matumizi na uhitaji wa trekta hilo.

“Mchakato huo utakuwa transparent tutashirikiana na John Deere, wizara ya Kilimo na AGRA kwa ajili ya kuendesha hayo…..Kikundi cha vijana kitakachoshinda kitakabidhiwa trekta”. Amesema Waziri Bashe

Makabidhiano ya trekta hilo yamefanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Dar es Salaam unapofanyika mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF).

Rais Samia awatunuku Taifa Stars kitita cha Milioni 500

0

Kufuatia timu ya Taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars) kufuzu kuingia fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika hapo jana wakitoka sare na Algeria, Rais Samia Suluhu Hassan ameizawadia timu hiyo donge nono la shilingi Milioni 500.

Zawadi hiyo ilikuwa ni ahadi ya Rais kwa timu hiyo wakiwa kwenye maandalizi ya kuchuana nchini Uganda.

Akizungumza akiwa Algeria, Saidi Yakubu, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema tayari fedha hizo zimekwisha tolewa.

“Nafurahi kuwaambia kwamba hizo fedha sio tu kwamba zitatolewa, zimekwisha letwa wizarani kwa ajili yenu.”