Teknolojia ya VAR kutumika kombe la dunia badala ya vibendera

0

Waamuzi wasaidizi katika fainali za 21 za kombe la FIFA la dunia wametakiwa kutonyanyua vibendera vyao endapo kutatokea utata wa kutambua kama kuna tukio la kuotea yaani offside na badala yake wasubiri msaada wa teknolojia ya Video -VAR ufanye kazi.

Shirikisho la soka duniani -FIFA linaamini kwamba teknolojia hiyo ya video ina msaada mkubwa katika kuwasaidia waamuzi kuamua matukio yenye utata na hii itakuwa mara ya kwanza kwa teknolojia hiyo kutumika katika fainali za kombe la FIFA la dunia.

Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi Pierluigi Collina amesema endapo mwamuzi Msaidizi hatanyanyua kibendera ifahamike kuwa atakuwa hajafanya makosa na badala yake atakuwa anaheshimu maamuzi hayo na kusubiri teknolojia ya VAR ifanye kazi yake.

Mwamuzi huyo nguli kutoka nchini Italia amesema waamuzi hao wasaidizi wametakiwa kufanya hivyo kwasababu inawezekana kutokea shambulizi la nguvu katika lango la timu mojawapo au nafasi ya kupatikana bao na endapo mwamuzi msaidizi atanyanyua kibendera basi kila kitu kitakuwa kimemalizika.

Colina amefafanua zaidi na kusema endapo mwamuzi msaidizi hatonyanyua kibendera na mchezo ukaendelea hadi bao likafungwa watatumia teknolojia ya video kupitia tukio hilo ili kujiridhisha.

Katika  michuano ya mwaka huu kutakuwa na televisheni kubwa kwenye viwanja vyote ambayo itatoa fursa kwa mashabiki kutazama namna matukio mbalimbali yanavyoamualiwa na teknolojia hiyo ikiwemo yale ya penati na kadi nyekundu.

Watumishi sita wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu – HESLB waachishwa kazi.

0

Wakurugenzi watano na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu – HESLB wameachishwa kazi baada ya kubainika kuhusika na makosa mbalimbali ikiwemo kushindwa kutekeleza majukumu yao na uzembe hali iliyoisababishia serikali hasara.

Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul –Razaq Badru amesema maamuzi hayo yamefikiwa na Bodi ya wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo.

Walioachishwa kazi ni Juma Chagonja aliyekuwa Mkurugenzi wa Urejeshaji wa Mikopo, Onesmus Laizer aliyekuwa Mkurugenzi wa Upangaji na Ugawaji Mikopo, John Elias aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Ugawaji Mikopo, Robert Kibona aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo, Heri Sago aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu na Chikira Jahari aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Upangaji Mikopo.

Mwaka 2016 na 2017 Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya mikopo ya Elimu ya Juu iliwasimamisha kazi Wakurugenzi WATANO na Mkaguzi Mkuu wa ndani wa hesabu wa bodi hiyo ya mikopo.

Mapema mwaka huu HESLB iliunda kamati kuwachunguza watumishi hao na matokeo ya kamati hiyo yamewatia hatiani.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Bodi hiyo Abdul Mtibora amesema rufaa iko wazi endapo hawajaridhika na uamuzi wa bodi ya wakurugenzi.

 

Ngarayai Kimosa

13 Juni 2018

Wafanyabiashara waachwa nyuma kasi ya Magufuli uchumi wa viwanda

0
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF Godfrey Simbeye

Taasisi ya sekta binafsi nchini TPSF imesema kuna umuhimu kwa wafanyabiashara kwenda na kasi ya serikali katika utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda ili sera hiyo iweze kuwa na tija kwa taifa.

Akizungumza katika kikao cha sekta binafsi jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF Godfrey Simbeye amesema serikali inakwenda haraka kuliko sekta binafsi jambo ambalo halitakiwi.

Baadhi ya washiriki wa taasisi za sekta binafsi zinazosimamia wafanyabiashara wamesema vikao kama hivyo vinawapa nguvu ya kuwa na sauti moja wanapokabiliana na serikali kwa maslahi ya wafanyabiashara.

 

MCB yaanzisha huduma ya mikopo ya dharura

0
Mkuu wa kitengo cha ukuzaji biashara na masoko wa benki ya MCB Valence Luteganya (wa tatu kushoto) akiongea na waandishi wa habari katika uzinduzi wa huduma mpya ya benki hiyo ya Mikopo ya dharula.

Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB) imeanzisha huduma ya mikopo ya dharura ambayo rejesho lake hukatwa kwenye mshahara wa mteja (Salary advance) kwa lengo la kumwezesha mteja kuyakabili mahitaji muhimu yanayojitokeza wakati wowote.

Mkuu wa kitengo cha ukuzaji biashara na masoko wa benki hiyo Valence Luteganya amesema huduma ya ‘Salary Advance’ inawahusu wateja wafanyakazi wanaopitisha mishahara yao katika benki ya mwalimu ambao wataweza kupata mkopo wa hadi asilimia 50 ya mishahara yao.

Wajasiriamali kupatiwa mikopo yenye masharti nafuu

0

Serikali imesema itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kina mama na vijana. Akizungumza mjini Arusha katika hafla ya kukabidhi mikopo isiyokuwa na riba kwa kina mama wajasiliamali Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema serikali itaendelea kuwasaidia wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Pia ameahidi kuwasaidia wanawake kuanzisha umoja wenye nguvu utakaowasaidia kujikomboa kutoka katika umasikini.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amewaagiza viongozi wa ngazi ya chini katika mkoa huo kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili wananchi hao na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Zaidi ya Kinamama 600 wa mkoa wa Arusha wanatarajiwa kupewa mikopo isiyokuwa na riba yenye thamani ya shilingi milioni miamoja na ishirini.

Trump na Kim wazungumza

0

Rais wa Marekani Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un wamekutana katika mazungumzo ya kihistoria, ambapo ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa serikali ya Marekani na wa Korea Kaskazini walioko madarakani kukutana uso kwa uso.

Majaliwa ataka taasisi za serikali ziache kutumia mkaa

0

Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara, mashirika na taasisi zote za Serikali na binafsi zianze kutumia nishati mbadala ili kuondoa kabisa matumizi ya kuni na mkaa.

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Mei 31, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mkaa ni Gharama: Tumia Nishati Mbadala.”

Amesema teknolojia bora ya uzalishaji wa mkaa mbadala ambayo ameiona kwenye maonesho hayo, ikuzwe na kusambazwa kote nchini ili kuwawezesha wananchi walio wengi waachane na matumizi ya mkaa wa kawaida na badala yake watumie mkaa-mbadala kwa lengo la kuhifadhi misitu na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Waziri Mkuu ameagiza pia kuwa vibali vya ujenzi wa majengo makubwa na taasisi kama shule, vyuo, hospitali navyo pia vianze kutolewa kwa kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia ili kurahisisha upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala katika taasisi na majengo makubwa.

“Wahandisi na wachoraji ramani za majengo waweke njia za kupitisha gesi kwenye michoro yao ili ujenzi wa nyumba na majengo haya ukikamilika, watumiaji waweze kutumia teknolojia hiyo,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni lazima ubadilike na uachane na matumizi ya mkaa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo unatumia tani 500,000 za mkaa kwa mwaka.

“Viongozi wa mkoa na wilaya ondokeni hapa na hili kama ajenda ya mkoa wa Dar es Salaam, mkaifanyie kazi na Wizara pia ifuatilie mmetekeleza kwa kiasi gani. Jitihada zilizofanywa na Jiji la Dar es Salaam kupitia kwa Mstahiki Meya, za kuanza kuwapa mtaji wajasiriamali hawa wanaotengeneza teknolojia mpya ni lazima ziigwe na nyie kwenye Manispaa zenu.”

Moto wazuka katika jengo moja Kariakoo

0

Sehemu ya jengo la ghorofa moja imeteketea kwa moto katika mtaa wa Aggrey na Livingstone eneo la Kariakoo jijini Dar Es Salaam mapema leo.

Taarifa za awali zinasema moto huo umeteketeza baadhi ya mali zilizokuwemo  katika jengo hilo.Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika.

Hakuna watu waliodhurika kutokana na moto huo.

Gloria Michael

13 Juni 2018