Zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kuanza kwa fainali za kombe la FIFA la dunia, Rais wa shirikisho la vyama vya mpira wa miguu duniani FIFA, Giovanni Infantino ametangaza kuondolewa kwa mjadala wa ushiriki wa mataifa 48 katika fainali za kombe la FIFA la dunia zitakazofanyika nchini Qatar mwaka 2022 kwenye mkutano mkuu wa 68 wa FIFA utakaofanyika Juni 13 mjini Moscow nchini Russia.
Infantino amesema agenda hiyo haitojadiliwa kutokana na changamoto ya miundombinu hasa viwanja vya kufanikisha michuano hiyo nchini Qatar ingawa mazungumzo na Qatar bado yanaendelea kuona kama wataweza kumudu kuandaa mashindano kwa mataifa 48 au la.
Rais huyo wa FIFA alikuwa na matumaini ya kuongezeka idadi ya mataifa shiriki katika fainali za kombe la FIFA la dunia kutoka mataifa 32 ya sasa hadi 48, matumaini ambayo yalichagizwa kwa kiasi kikubwa na mataifa kutoka bara la Amerika ambayo yanaamini ongezeko la mataifa shiriki litaongeza msisimko zaidi kwenye fainali hizo.
Katika hatua nyingine Rais huyo wa FIFA amesema hana hofu yoyote juu ya matumizi ya msaada wa video katika kufanya maamuzi yaani Video Assistant Referee (VAR) kwasababu anaamini kuna wakati matumizi ya teknolojia hiyo yatasaidia kuondoa utata katika baadhi ya matukio wakati wa mchezo.
Oscar Urassa
11 Juni 2018