Maabara mpya ya kupima madini yazinduliwa Dar

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea maelezo kutoka kwa mtaalam wa maabara ya kupima madini iliyozinduliwa leo Ijumaa Dar es salaam

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua maabara ya kisasa yenye uwezo wa kupima na kutambua aina mbalimbali za madini.

Maabara hiyo iliyofunguliwa leo Ijumaa, katika Kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika (AMGC) kilichopo Kunduchi jijini Dar es Salaam, itasaidia kupunguza migogoro ya umiliki wa madini na kudhibiti utoroshwaji wa madini mbalimbali kati ya nchi moja na nyingine.

“Maabara hii litatuweza kulinda madini yetu na kufanya biashara ya madini vizuri. Pia hii ni fursa nzuri kwa nchi za Afrika kutumia maabara hii kupima madini yao na kubaini yalikotoka,” Waziri Mkuu amesema.

Waziri Mkuu pia amewataka viongozi wa kituo hicho kuhakikisha wanaziwesha nchi wanachama kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya madini pindi zinapohitaji.

Ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kusaidia katika ununuzi wa vifaa vya maabara hiyo pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu watakaoiendesha.Waziri Mkuu, pia ameiomba Serikali hiyo kutoa mafunzo hayo kwa Watanzania wengi zaidi ili kuongeza idadi ya wataalamu wa kuendesha maabara hiyo.

Pia, Waziri Mkuu amefungua Mkutano 38 wa Mawaziri wa Madini kutoka nchi Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu unaofanyika katika kituo cha AMGC.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ikiwa ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama zilizosheheni wanyama wa aina mbalimbali pamoja na fukwe za bahari.

Macron ampa uraia mhamiaji aliyemuokoa mtoto aliyekuwa akining’inia ghorofani

0

Mtoto wa miaka minne akining’inia kutoka ghorofa ya nne kabla hajaokolewa na mhamiaji kutoka nchi ya Mali Mamoudou Gassama (22). Picha ya pili Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akizungumza na Gassama leo Jumatatu Mei 28. .

Mhamiaji kutoka Mali aliyekuwa ‘akibangaiza’ maisha huko Ufaransa, Mamoudou Gassama ghafla amejikuta mambo yake yakinyooka, baada ya Rais Emmanuel Macron kuagiza apewe uraia wa Ufaransa kwa kitendo cha kishujaa alichofanya mwishoni mwa wiki iliyopita, cha kukwea ghorofa kutokea nje hadi kufanikiwa kumuokoa mtoto aliyekuwa akininginia nusura aanguke, kutoka ghorofa ya nne.

Gassama amepata umaarufu mkubwa katika vyombo vya habari vya Ufaransa na duniani kuanzia Jumamosi iliyopita siku ambayo tukio hilo limetokea, kiasi kwamba Rais Macron amemuita Ikulu leo Jumatatu ambapo baada ya kuzungumza naye, Rais huyo akatangaza kuwa atapatiwa uraia wa Ufaransa.

Picha za video zilizochukuliwa na baadhi ya mashuhuda zimeonyesha jinsi Gassama ambaye alikuwa ni mpita njia, alivyopanda kwa kasi ghorofa hadi ghorofa kutokea nje ya jengo hilo huku akishangiliwa na mashuhuda wengine, hadi kumfikia mtoto huyo mwenye umri wa miaka minne na kufanikiwa kumweka mikononi mwake akiwa salama.

Gassama amesema wakati akipita njia katika eneo hilo kaskazini mwa jiji la Paris, aliona umati wa watu waliokusanyika mbele ya jengo hilo na kuongeza kuwa alihisi maumivu makali kumuona mtoto yule katika hali ile ndipo akachukua ujasiri wa kwenda kumuokoa.

“NIlipofanikiwa kumuweka kwenye mikono yangu nilizungumza naye na kumuuliza kwa nini umefanya hivi lakini hakunijibu” amesema Gassama.

Maofisa wa kikosi cha zimamoto cha Paris wamesema askari wao walipofika katika jengo hilo walikuta mtoto huyo alishaokolewa.

“Kwa bahati palikuwa na mtu ambaye ni mkakamavu kimaumbile na aliyekuwa na ujasiri wa kwenda kumuokoa mtoto huyo” msemaji wa zimamoto aliwaambia waandishi wa shirika la habari la AFP.

Viongozi wa mtaa tukio hilo lilipotokea wamenukuliwa wakisema kuwa wakati tukio hilo linatokea wazazi wa mtoto huyo hawakuwepo nyumbani.

Polisi wanamshikilia baba wa mtoto huyo kwa tuhuma za kumuacha mtoto bila uangalizi, ambapo inasemekana kuwa mama wa mtoto huyo alikuwa nje ya jiji la Paris wakati tukio linatokea.

Meya wa jiji la Paris Anne Hidalgo alikuwa ni mmoja wa watu waliompongeza Gassama(22) kwa kumpigia simu yeye binafsi na baadae kuongea na waandishi wa habari huku akimpachika jina la ‘spiderman’ akimaanisha mtu mwenye uwezo mkubwa wa kukwea majengo marefu.

Rais Macron amemshukuru Gassama na kumpa medali kwa ujasiri, lakini pia amesema Ufaransa itampa ajira ya uaskari shujaa huyo, katika kikosi cha zimamoto.

Volkano yalipuka tena Guatemala

0

Kwa mara nyingine serikali ya Guatemala imewahamisha watu wanaokaa karibu na mlima wenye volkano hai wa Fuego nchini humo baada ya mlima huo kulipuka tena kwa mara ya pili wiki hii.

Hadi sasa watu 75 wamethibitika kufa na wengine mia mbili hawajulikani walipo baada ya mlipuko wa kwanza kutokea katika mlima huo na kusababisha mawe, matope ya moto na majivu kurushwa umbali mrefu kutoka kwenye mlima huo.

Habari zinasema lava na majivu yameanza tena kumwagika katika eneo linalozunguka mlima huo na zoezi la uokoaji wakati mwingine likikwamishwa na majivu pamoja na moshi unaoendelea kufuka.

Korea Kaskazini yamuita makamu wa Trump ‘mpumbavu’, mkutano Juni 12 bado njiapanda

0

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence (Picha na REUTERS)

Vita ya maneno inaendelea kati ya maofisa wa Korea Kaskazini na Marekani ambapo katika hatua ya hivi karibuni ofisa mmoja wa ngazi za juu katika serikali ya Korea Kaskazini Choe Son-hui amemuita Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence kuwa ni ‘mpumbavu’ kwa kuilinganisha nchi hiyo na Libya.

Ofisa huyo pia ametishia kuwepo tayari kwa Korea Kaskazini kwa vita ya nuklia iwapo diplomasia itashindwa, akisema kuwa nchi hiyo haiwezi kamwe kuibembeleza Marekani kumaliza mgogoro huo kidiplomasia na wala kujaribu kuishawishi ihudhurie mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Juni 12 mwaka huu nchini Singapore.

Katika siku za karibuni pande zote mbili zimekuwa zikionya kwamba kuna hatari mazungumzo hayo ya Juni 12 yakasogezwa mbele au kufutwa kabisa, ambapo Pyongyang imesema haitahudhuria kama Marekani itasisitiza kuwa nchi hiyo iachane na nuklia huku Trump akisema juzi kuwa ni Korea Kaskazini inayopaswa kutimiza masharti ili mazungumzo hayo yaweze kufanyika kama ilivyopangwa.

Choe Son-hui, mwanamama ambaye katika muongo mmoja uliopita ameshiriki katika harakati mbali mbali za kidiplomasia na Marekani, amesema Pence ametoa kauli zisizoonyesha heshima kwa Korea Kaskazini, ikiwa ni pamoja na kusema kwamba nchi hiyo inaweza kuishia kama Libya.

Katika makala iIiyotangazwa na Shirika la Habari la Serikali ya Korea Kaskazini (KCNA), Choe Son-hui amesema Pence ni mjinga na mwanasiasa uchwara, kwa kuilinganisha nchi ya nuklia ya Korea Kaskazini na Libya ambayo ilikuwa na vifaa vichache tu tena ambavyo ‘ilivichezea’.

“Kama mtu niliyeshiriki sana mambo ya Marekani, siwezi kuficha mshangao wangu kuhusu kauli za kijinga na kipumbavu kutoka kwenye mdomo wa Makamu wa Rais wa Marekani” amesema Choe na kuongeza “Kama Marekani itakutana nasi katika chumba cha mkutano au katika uwanja wa vita vya nuklia, ni suala linalotegema kwa asilimia 100 katika uamuzi na mwenendo wa Marekani”.

Hivi karibuni mshauri wa usalama wa Marekani John Bolton pia aliiudhi Korea Kaskazini hadi ikatishia kujitoa katika mazungumzo yanayotarajiwa, baada ya kusema Korea Kaskazini inaweza kufuata mtindo uliotumika Libya kuiondolea uwezo wa kinuklia.

Wachambuzi wanasema kwa vile Choe Son-hui ni mtu mwenye nguvu katika siasa za Korea Kaskazini na mmoja wa wasaidizi wakuu wa Rais Kim jong-un, bila shaka kauli alizotoa zina baraka zote za Rais Kim mwenyewe.

Kwamba hadi sasa Pyongyang haijamrushia matusi Donald Trump ambaye kwa kiasi fulani juzi alitoa kauli zinazokaribia kufanana na za hao wasaidizi wake wa karibu, inaashiria kuwa huenda Korea Kaskazini bado haijachukua uamuzi wa kuyatupila mbali moja kwa moja, mazungumzo hayo.

Wadau wa elimu kupitia TBC kukutana Arusha Juni 17

0

Waziri wa elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako

Mkutano wa wadau wa elimu kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) utafanyika Juni 17 hadi 23, 2018 katika ukumbi wa mahakama ya kimataifa (TANAPA) mjini Arusha.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa TBC imewataka wadau wote kulipa ada ya ushiriki katika mkutano huo ambayo ni kiasi cha Shilingi laki tano (500,000 /=) kwa kila mshiriki, mapema iwezekanavyo.

Taarifa hiyo imeelekeza kuwa malipo yanapaswa kufanyika katika ofisi za TBC makao makuu huko barabara ya Nyerere Dar es Salaam au TBC1 Mikocheni jijini au katika ofisi za Masoko zilizopo mtaa wa Zanaki Dar es Salaaam.

Taarifa hiyo imesema pia kuwa malipo yanaweza kufanyika kupitia akaunti ya benki ya CRDB namba 0IJ 1043002901 jina la akaunti likiwa ni TBC.

Watu walioko mikoani wameshauriwa kufanya malipo kupitia ofisi za kanda za TBC na kwa mawasiliano zaidi wanaweza kupiga simu namba 0738 681066.

Uongozi wa TBC unawataka wadau kuthibitisha ushiriki wao kabla ya Juni 15, 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awahamasisha watanzania kununua Hisa

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akinunua hisa toka kampuni ya Simu ya Vodacom

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amenunua Hisa za thamani ya shilingi milioni 20 za kampuni ya Simu ya Vodacom ili kuwahamasisha watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye masoko ya hisa na mitaji.

Akizungumza wakati akinunua Hisa hizo jijini Dar es salaam Waziri Mkuu amesema hisa za shilingi milioni 10 kati ya hisa hizo ni za kwake na na zinazobakia ni kwa ajili ya Mke wake Mary Majaliwa.

Wakizungumzia uwekezaji huo waziri wa Fedha na mipango Dokta Philip Mpango na katibu mtendaji wa baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi NEEC Beng’i Issa wamewataka wakulima na wafugaji kuwekeza kwenye Hisa ili waweze kunufaika moja kwa moja na ukuwaji Wa uchumi .

Vumilia Mwasha

Mauzo ya hisa yaongezeka DSE

0

Msemaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam Mary Kinabo

Wiki iliyopita ilikuwa yenye mavuno manono kwa soko la hisa la Dar es salaam (DSE)  baada ya mauzo ya hisa kuongezeka karibu mara nne ikilinganishwa na mauzo ya hisa ya wiki iliyoishia Januari 11.

Kwa mujibu wa taarifa ya Soko hilo, mauzo ya hisa yaliongezeka na kufikia shilingi bilioni 1.8 wiki iliyopita kutoka shilingi milioni 371 katika wiki iliyotangulia kutokana na kupanda kwa bei za hisa za kampuni mbalimbali zikiwemo DSE wenyewe na benki ya CRDB.

Msemaji wa soko hilo Mary Kinabo amesema mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko la hisa la Dar es salaam pia umeongezeka kwa shilingi bilioni 16.

Yanga yaomba kujitoa kombe la Kagame

0

Uongozi wa klabu ya Yanga umeliandikia barua shirikisho la soka hapa nchini TFF  kuwaomba kujitoa katika mashindano ya Kagame Cup yanayotarajiwa kuanza June 28 mpaka Julai 13 mwaka huu jijini Dar Es Salaam.

Msemaji wa Yanga, Dismas Ten amesema sababu za msingi zilizofikia Yanga kuandika barua hiyo ni kufanya maandalizi ya michunao ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo watacheza na Gor Mahia FC ya Kenya, Julai 18 jijini Nairobi nchini Kenya.

Kutokana na muingiliano wa ratiba ya Kagame na CAF, Yanga wameona ni vema kuwapatia wachezaji wao mapumziko ili kuwapa fursa ya kujiandaa vizuri kuelekea mechi hiyo ambayo itakuwa ni ya tatu baada ya kucheza na USM Alger pia Rayon Sports ya Rwanda.

Enock Bwigane
08 Juni 2018