Trump asisitiza kutovunja sheria

0

Rais Donald Trump wa Marekani amesisitiza kuwa malipo yanayodaiwa kufanywa kwa siri kwa wanawake wawili wanaodhaniwa kuwa na uhusiano naye hayakuvunja sheria ya fedha za kampeni za uchaguzi mwaka 2016.

Trump amekana tuhuma za kuhusika kwake katika kutumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikutano ya kampeni kuwalipa wanawake hao.

Mapema wiki hii katika kesi iliyosikilizwa kwenye mahakama moja mjini New York , mwanasheria wa zamani wa Rais Trump,- Michael Cohen alidai kuwa Trump alimpa maelekezo ya kutoa fedha kwa lengo la kuwashawishi wanawake hao kukaa kimya wakati wa uchaguzi huo wa Urais wa mwaka 2016.

Ikulu ya Marekani imesisitiza kuwa kuvunja sheria ya fedha za kampeni kwa Cohen hakumaanishi kuwa Rais Trump naye atawajibika,

Hata hivyo Rais Trump mwenyewe katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini Marekani alitolea ufafanuzi suala hilo na kusema kuwa malipo kwa Wanawake hao wawili yalitoka katika fedha zake binafsi na si fedha za kampeni kama inavyodhaniwa na wengi.

Trump amekuwa akimshutumu Cohen kwa kusema mambo yasiyo na ukweli dhidi yake kwa lengo la kupata huruma na kuepuka kifungo.

Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini Marekani, malipo yanayofanywa kwa siri kwa niaba ya mwanasiasa ama mgombea yeyote yanaweza kuchukuliwa kama ukiukwaji wa sheria za kampeni za uchaguzi.

Mapigano ya wakulima na wafugaji yazuka Mkuranga

0

Watu Sita wamejeruhiwa baada ya kutokea kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji katika kijiji cha Kondomwelanzi kilichopo kwenye eneo la mpaka wa wilaya za Mkuranga na Kisarawe mkoani Pwani.

Mkuu wa wilaya ya Mkuranga , -Filberto Sanga amesema kuwa mapigano hayo yamezuka baada ya kundi la wafugaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima na kuharibu mazao.

Amesema kuwa baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Mkuranga kupata taarifa hizo, askari walitumwa katika eneo la tukio kwa lengo la kuwasaka wafugaji waliosababisha mapigano hayo ambao hawajapatikana na jitihada za kuwatafuta zinaendelea.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mkuranga ameongeza kuwa ili kuzuia kutokea kwa matukio kama hayo, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Mkuranga itaenda katika kijiji hicho kwa lengo la kuzungumza na wakazi wake ili kukubaliana namna ya kufanya pindi yanapojitokeza matukio ya aina hiyo na si kuingia katika mapigano.

Sanga amefafanua kuwa mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika kijiji hicho cha Kondomwelanzi yamesababishwa na ongezeko la mifugo hasa ng’ómbe baada ya wafugaji wengi kuondolewa katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya jirani ya Kisarawe.

Bobi Wine afutiwa mashitaka

0

Serikali ya Uganda imemfutia mashitaka yaliyokua yakimkabili Mbunge wa jimbo la Kyadondo – Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Mbunge huyo ambaye aliwahi kuwa mwanamuziki nchini humo leo Agosti 23 alitarajiwa kurudishwa katika mahakama ya kijeshi iliyopo kwenye mji wa Gulu kaskazini mwa Uganda.

Kabla ya kuwepo kwa taarifa za kufutiwa mashitaka kwa Bobi Wine, mawakili wa Mbunge huyo walifahamishwa kuwa kesi yake itasikilizwa katika kambi ya kijeshi ya Makindye mahali anakozuiliwa mjini Kampala.

Vyombo vya dola nchini Uganda vimekua vikimshikilia Bobi Wine kwa madai ya kumiliki silaha kinyume na sheria, hatua iliyozusha maandamano katika maeneo mbalimbali nchini humo na kusababisha uharibifu wa mali huku wengi wa waandamaji hao wakisema kuwa tuhuma hizo zinahusiana na mambo ya kisiasa

Kumekuwa na shinikizo la kimataifa la kutaka kuachiliwa huru kwa Bobi Wine ambaye amekua akishikiliwa kwa takribani wiki moja, ikiwa ni pamoja na shinikizo kutoka kwa baadhi ya Wanamuziki maarufu duniani.

Tanzania Makamu Mwenyekiti mpya wa SADC

0

Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umemalizika rasmi tarehe 18 Agosti katika mji wa Windhoek nchini Namibia kwa kumteua Rais John Magufuli kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha Agosti 2018 mpaka Agosti 2019.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliyemwakilisha Rais Magufuli katika mkutano huo ameishukuru SADC kwa imani kubwa waliyoionesha kwa Tanzania katika jukumu hilo na amewaahidi Wakuu nchi wanachama ushirikiano wa dhati wa serikali ya Tanzania katika kutekeleza majukumu ya Makamu Mwenyekiti kwa kuweka mbele vipaumbele na agenda za Jumuiya hiyo.

Kufuatia uteuzi huo, Rais Magufuli atapewa rasmi jukumu la Uenyekiti wa SADC katika Mkutano Mkuu ujao wa 39 utakaofanyika Tanzania mwezi Agosti mwaka 2019.

Tanzania imeteuliwa kushika nafasi hiyo kufuatia utaratibu wa kawaida wa mzunguko wa uongozi baina ya nchi Wanachama wa SADC ambapo itaongoza kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2018 hadi Agosti 2019.

Viongozi wengine walioteuliwa katika uchaguzi huo ni pamoja na Jamhuri ya Namibia kuwa Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha Agosti 2018 hadi Agosti 2019.

Troika ya SADC kwa kipindi cha Agosti 2018 na Agosti 2019 itaundwa na Namibia, Tanzania na Afrika Kusini.

Rais asema mambo yanaenda vizuri

0

Rais John Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa juhudi za kujenga Tanzania mpya zinakwenda vizuri kutokana na mafanikio makubwa yaliyoanza kupatikana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Agosti 18 aliposalimiana na wananchiwa liokusanyika katika njiapanda ya Bugando jijini Mwanza na Mjini Sengerema akiwa njiani kuelekea Chato mkoani Geita kwa mapumziko.

Amesema kuwa utekelezaji wa ahadi za serikali unakwenda vizuri ambapo katika kipindi kifupi cha miaka miwili na miezi 8 kumekuwa na kasi kubwa ya ujenzi wa viwanda vilivyofikia 73,060, Kampuni ya Ndege Nchini (ATCL) imefufuliwa, miundombinu ya barabara na madaraja inajengwa, watoto wanapata elimu bila malipo na mengine mengi ambayo yamechangia kupanua uwigo wa ajira na kukuza uchumi.

Akiwa Sengerema Rais Magufuli amesikiliza kero za wananchi ambapo amepiga marufuku viongozi wa halmashauri kuwanyang’anya bidhaa zao wafanyabiashara wadogo na badala yake ameagiza viongozi wote nchini kujielekeza kutatua kero zinazowakabili wananchi ikiwemo ukosefu wa soko la mazao yao.

Ametoa agizo hilo baada ya wananchi wa Sengerema kudai kuwa halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa ikiwanyang’anya matunda aina ya nanasi wakulima na wafanyabiashara wanaouza matunda yao mjini.

Rais amemuagiza mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella kufuatilia na kutatua kero hiyo.

Kabla ya kukutana na wananchi wa Mwanza,
Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya uangalizi maalum (ICU) ya hospitali ya Bugando jijini Mwanza akiwemo dada yake Monica Magufuli.

Amewashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuwatibu wagonjwa na amesema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo ili kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.

Kofi Annan afariki dunia

0

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amefariki dunia.

Habari zinasema kuwa Annan amefariki dunia katika hospitali moja nchini Switzerland alipokua akipatiwa matibabu baada ya kuugua gafla.

Amefariki akiwa na umri wa miaka 80.

Annan alikua ni Mwafrika mweusi wa kwanza kutumikia wadhifa huo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na alitumikia nafasi hiyo kwa vipindi viwili kati ya mwaka 1997 na 2006.

Wilaya zatakiwa kufanya tathmini ya mali zake

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya nchini kushirikiana na madiwani katika halmashauri zao kufanya tathmini ya mali zote zinazomilikwa na halmashauri vikiwemo vibanda vya biashara ili kujiridhisha kama viwango vya kodi vinavyotozwa vinalingana na hali halisi ya uchumi kwa sasa.

Amesema kuwa mbali na tathmini hiyo kuwawezesha kufahamu viwango vinavyotozwa, pia itazisaidia halmashauri kubaini watu wa kati ambao wanawatoza wafanyabiashara fedha nyingi na kuilipa halmashauri fedha kidogo, jambo linalochangia kuikosesha serikali mapato.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya mji wa Nzega na wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega pamoja na madiwani, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi wilayani Nzega mkoani Tabora.

Ametoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Nzega Mjini, Husein Bashe kuomba serikali iingilie kati mgogoro uliopo baina ya halmashauri na wafanyabiashara kuhusu mradi wa vibanda vya biashara katika eneo la Soko Kuu la Nzega ambavyo vimejengwa na wafanyabiashara katika ardhi ya halmashauri kwa makubaliano ya kulipa kodi.

Mwili wa Meja Jenerali Mstaafu Lesulie waagwa

0

Rais John Magufuli ameongoza waombolezaji kuuaga mwili wa Meja Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Joseph Anael Lesulie aliyefariki dunia Agosti 14 mwaka huu katika hospitali ya taifa ya muhimbili jijini Dar es salaa alikokuwa akipatiwa matibabu.

Shughuli ya kuuaga mwili wa meja jenerali mstaafu lesulie imefanyika nyumbani kwa marehemu katika eneo la ada estate, kinondoni jijini Dar es salaam.

Meja Jenerali Mstaafu Lesulie anazikwa hii leo katika makaburi ya kinondoni jijini dar es salaam.