Simba Watoto mabingwa Afcon U-17

0

Timu ya Uganda ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 imeungana na wenyeji Tanzania katika kufuzu kwa michuano ya vijana itakayotimua vumbi mwezi Mei mwaka 2019.

Timu hiyo ya Uganda maarufu kama Simba Watoto wamekata tiketi hiyo baada ya kuifunga Ethiopia katika mchezo wa fainali wa mashindano ya kufuzu kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) magoli matatu kwa moja katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Iliwachukua dakika 15 Simba Watoto hao kuandika bao la kuongoza kupitia kwa Samson Kasozi, huku Abdul Wahad Iddi akiwa mwiba mkali kwa timu ya Ethopia baada ya kuiandikia Uganda magoli mawili katika kipindi cha pili, ambapo Waethiopia nao walipata goli la kufutia machozi katika dakika za lala salama kupitia kwa Wondimagegn Bunaro.

Katika mchezo wao wa nusu fainali, Uganda waliifunga timu ya Tanzania ya vijana wa umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys kwa kuwachabanga magoli matatu kwa moja, Ethiopia wao waliwafunga Rwanda katika hatua hiyo.

Serengeti Boys ambao walishafuzu kutokana na Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, wamemaliza michuano ya kufuzu katika nafasi ya tatu baada ya kuifunga Rwanda kwa mikwaju ya penati minne kwa mitatu baada ya dakika 90 kumalizika kwa vijana hao kutoshana nguvu kwa goli mbili kwa mbili.

Katika michuano hiyo Tanzania ilipata tuzo ya timu yenye nidhamu na Kelvin John amechaguliwa kuwa mchezaji bora

Mnangagwa aapishwa

0

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe anayeungwa mkono na jeshi la nchi hiyo ameapishwa kuongoza Taifa hilo baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Julai mwaka huu.

Rais Mnangagwa ameapishwa na Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo Luke Malaba katika sherehe zilizohudhuriwa na idadi kubwa ya raia wa Zimbabwe katika uwanja wa Taifa mjini Harare.

Viongozi kutoka mataifa mbalimbali wamehudhuria sherehe hizo ambapo kwa Tanzania, Rais John Magufuli amewakilishwa na Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Dkt Jakaya Kikwete.

Rais Mnangagwa anakabiliwa na jukumu kubwa la kuijenga upya Zimbabwe inayokabiliwa na matatizo ya kiuchumi pamoja na kuliunganisha taifa hilo.

KKKT yatoa pongezi kwa serikali

0

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limeipongeza serikali kwa kutoa huduma za matibabu ya moyo na figo nchini na hivyo kuwawezesha Watanzania wengi kumudu gharama za matibabu ya magonjwa hayo ndani ya nchi.

Pongezi hizo zimetolewa mkoani Kilimanjaro na Mkuu wa KKKT Askofu Fredrick Shoo wakati
wa mkutano mkuu wa 35 wa kanisa hilo.

Askofu Shoo ameiomba serikali kuongeza idadi ya madaktari pamoja na vitendea kazi ili kuwezesha Watanzania wengi zaidi kupatiwa matibabu hayo ya moyo na figo.

Akifungua mkutano huo, Mkuu huyo wa KKKT pia ameiomba serikali kuangalia namna ya kuondoa kodi ya ardhi kwa taasisi za kidini.

Akitoa salamu za serikali wakati wa mkutano huo mkuu wa 35 wa KKKT, Kaimu mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro – Kippi Warioba amesema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na kanisa hilo katika kuwaletea maendeleo Watanzania.

Walalamikia Bwawa kutotoa maji

0

Zaidi ya wakulima Elfu 25 wa kata tatu za Igurusi, Ruhanga na Itamboleo wilayani Mbarali mkoani Mbeya wameiomba serikali kuingilia kati mradi wa bwawa la umwagiliaji maji la Rwanyo ambalo tangu kukamilika kwake mwaka 2013 halijawahi kutoa maji.

Wakizungumza na Mwandishi wa TBC mkoani Mbeya, wakulima hao wamedai kuwa pamoja na kwamba ujenzi wa bwawa hilo umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 4.9 hadi kukamilika kwake, bado uwepo wa bwawa hilo haujawanufaisha.

Wakulima wa kata hizo tatu za Igurusi, Ruhanga na Itamboleo wilayani Mbarali mkoani Mbeya wameongeza kuwa matumaini yao ni kuona bwawa hilo linawasaidia katika kuinua sekta ya kilimo, lakini kutokana na kushindwa kutoa maji matumaini hayo hayapo kwa sasa.

Naye msimamizi wa mradi huo wa bwawa la umwagiliaji maji la Rwanyo,- Pius Mwaigonjola amekiri ujenzi wa mradi huo kufanyika chini ya kiwango na hivyo kutokua na uwezo wa kutoa maji

Scott Morrison Waziri Mkuu mpya Australia

0

Chama cha Liberal nchini Australia kimemteua Scott Morrison kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo kuchukua nafasi ya Malcolm Turnbull ambaye ameondolewa kwa lazima na chama chake.

Kutokana na mzozo wa uongozi ndani ya chama cha Liberal, viongozi wa chama hicho waliamua kuitisha uchaguzi na kumchagua Morrison ambaye ni Mweka hazina wa chama hicho kwa kura 45 huku mpinzani wake Peter Dutton akipata kura 40.

Morrison anakuwa Waziri Mkuu wa 30 wa Australia, nchi ambayo imeendelea kushuhudia mgogoro wa uongozi ndani ya kipindi cha miaka 10.

Turnbull mwenyewe hakuwania tena nafasi hiyo na mara nyingi amekua akipuuzia wito wa kumtaka ajiuzulu kutokana na mgogoro huo wa uongozi ndani ya chama cha Liberal, mgogoro unaoelezwa kuwa unadhoofisha hata utendaji kazi wa serikali.

Samatta aendelea kufanya vizuri Genk

0

Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Mbwana Samatta amefunga mabao matatu – Hat Trick katika mchezo ambao timu yake ya KRC Genk imeibuka na ushindi wa mabao matano kwa mawili dhidi ya Brondby IF ya Denmark katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya michuano ya Europa.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye dimba la Luminus mjini Genk, Samatta amefunga mabao yake katika dakika za 37, 55 na 70 wakati mabao mengine ya Genk yamefungwa na mshambuliaji Mbelgiji, Leandro Trossard kwa penalti dakika ya 45 na Ushei aliyefunga la mwisho katika dakika ya 90.

Genk sasa watatakiwa kwenda kuulinda ushindi wao katika mchezo wa marudiano ugenini, agosti 30 kwenye uwanja wa Brondby na endapo watapata ushindi wa jumla watatinga moja kwa moja hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Tanzania na Uganda zanufaika na ushirikiano

0

Tanzania na Uganda zimepata mafanikio makubwa kupitia mikutano ya Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) iliyofanyika jijini Arusha mwezi Aprili mwaka huu na ule uliofanyika mjini Kampala nchini Uganda na kumalizika Agosti 23 mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Balozi Augustine Mahiga na mwenzake wa Uganda, -Sam Kutesa wakati wa ufunguzi wa mkutano uliofanyika mjini Kampala.

Wametaja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kusainiwa kwa Mikataba ya Makubaliano tisa ikiwemo Mikataba ya kushirikiana katika uendelezaji wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar es salaam hadi Uganda na ile ya ushirikiano katika masuala ya elimu na mafunzo.

Mikataba hiyo inalenga kurahisisha ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili ili kutimiza azma ya viongozi wa nchi hizo John Magufuli na Yoweri Museveni wa Uganda ya kukuza biashara kati ya nchi hizo.

Kufuatia mikataba hiyo miradi mbalimbali ipo katika hatua tofauti za utekelezaji ikiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Kikagati – Murongo uliopangwa kukamilika mwaka 2020.

Pia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) litaanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es salaam hadi Entebbe mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa masuala ya anga katika mkutano uliofanyika jijini Arusha.

Magari ya kubeba wanafunzi yagongana

0

Mtu mmoja amekufa na wengine Kumi wamejeruhiwa wakiwemo wanafunzi Wanane baada ya magari mawili yaliyobeba wanafunzi wa shule za msingi Kivulini na Nyamuge kugongana uso kwa uso katika barabara kuu ya Mwanza – Simiyu eneo la Nyamhongolo jijini Mwanza.

Jeshi la polisi mkoani Mwanza limethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa imesababishwa na uzembe wa dereva wa gari la shule ya msingi Kivulini, – Kulwa Charles ambaye alihama upande wake na kwenda kuligonga gari la shule ya msingi Nyamuge lililokua kikiendeshwa na Albert Joram ambaye amefariki dunia.

Majeruhi wanane wa ajali hiyo wameruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu katika kituo cha afya cha Buzuluga na katika hospitali ya Sekou-Toure .

Majeruhi wawili ambao ni mwanafunzi Devotha Beni na dereva wa gari la shule ya msingi Kivulini, – Kulwa wamehamishiwa kwenye hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.