Waziri Mkuu akutana na Rais wa CAF

0

Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) Ahmad Ahmad ameelezea kuridhishwa na maandalizi ya michuano ya Afrika ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.

Michuano hiyo ya mpira wa miguu kwa Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 inatarajiwa kufanyika mwaka 2019 nchini Tanzania.

Akizungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam, Ahmad ameihakikishia serikali kuwa hakuna mabadiliyo yoyote ya ratiba yatakayofanyika kuhusu wenyeji wa michuano hiyo na kwamba CAF itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha michuano hiyo.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa mechi zote za michuano ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitafanyika jijini Dar es Salaam.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa nchi kushiriki katika mashindano makubwa kama hayo kwa kuwa yanasaidia kwenye ukuzaji wa vipaji kwa vijana ambao wengi wao ni wanafunzi.

Rais huyo wa CAF Ahmad Ahmad yupo nchini kwa ajili ya kuongoza mkutano maalum wa mabadiliko ya katiba ya Baraza la Vyama vya Soka katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam unahudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi wanachama wote 12 wa CECAFA.

TRA yatakiwa kupiga mnada makontena ya samani

0

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango amemuagiza Kamishna wa forodha wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kufuata hatua stahiki na kuyapiga mnada makontena Ishirini ya samani yaliyoagizwa na kuingizwa nchini na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, – Paul Makonda ambayo hayajalipiwa kodi.

Waziri Mpango ametoa agizo hilo bandarini jijini Dar es salaam ambapo amefanya ziara ya kushtukiza na kutoa wito kwa watanzania kununua samani hizo pindi zitakapopigwa mnada kwa mara nyingine.

Ziara hiyo ya Waziri Mpango ilikua na lengo kupata taarifa ya makontena hayo Ishirini ambayo yaliingia katika bandari ya Dar es salaam kwa awamu mbili tofauti tangu mwezi Januari mwaka huu na kutakiwa kulipiwa kodi ya zaidi ya Shilingi Bilioni Moja.

Makontena hayo Ishirini ya samani yanatarajiwa kupigwa mnada na TRA na endapo yatakosa mteja yatatolewa msaada kwa shule na ofisi mbalimbali nchini.

Wasimamizi wa uchaguzi mdogo watakiwa kuzingatia sheria

0

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani utakaofanyika Septemba 16 mwaka huu katika majimbo ya Ukonga mkoani Dar es salaam na Monduli mkoani Arusha na kwenye kata 13 za Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya katiba, sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa kata na majimbo hayo.

Jaji Kaijage amewataka wasimamizi hao kuzingatia weledi na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ili wapunguze na kuondoa malalamiko yanayojitokeza wakati wa uchaguzi.

Amesema kuwa uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa na kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko au vurugu.

Katika uchaguzi huo mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Septemba 16 mwaka huu mgombea Ubunge katika Jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga amepita bila kupingwa na wagombea 10 wa udiwani katika kata 10 nao wamepita bila kupingwa, hivyo jumla ya kata zilizobaki zitakazoingia kwenye uchaguzi mdogo ni 13 na majimbo mawili ambayo ni Monduli na Ukonga.

TIC kutumia mfumo wa kielektroniki kutoa vibali

0

Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kinatarajia kuanza kutumia mfumo wa ndani wa kielektroniki kutoa vibali vya kazi kwa wawekezaji, lengo likiwa ni kuwawezesha wawekezaji hao kuomba vibali hivyo kabla ya kufika nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, – Geoffrey Mwambe amesema kuwa hatua hiyo itawezesha maombi hayo kufanyiwa kazi mapema na kuondoa usumbufu kwa wawekezaji hao pindi wanapofika nchini.

Kwa mujibu wa Mwambe, mfumo huo utaanza kutumika Septemba Tatu mwaka huu.

Mwambe pia amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo baadhi ya wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na mawaziri kuacha kutoa matamko na maagizo kwa wawekezaji nchini.

Amesema kuwa ni vema kila mamlaka ikatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kufafanua kuwa iwapo kuna tatizo lolote linalohusu kodi, vibali au ubora wa bidhaa kwa Mwekezaji kuna haja ya kufuata taratibu kutafuta ufumbuzi kupitia mamlaka husika badala ya kutoa maagizo ambayo hayazingatii sheria.

AfDB kuangalia miradi zaidi ya kuwekeza Tanzania

0

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Phillip Mpango amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Wanachama wa Benki ya Maendeleo ya Afrika(AfDB) zinazonufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na benki hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Dkt Mpango amesema kuwa katika kuelekea uchumi wa viwanda, miradi kadhaa ya maendeleo inafadhiliwa na benki hiyo kwa gharama ya zaidi ya shilingi trilioni Nne.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari Dkt Mpango alifuatana na Mwakilishi wa Marekani katika Benki ya Maendeleo ya Afrika, – Steven Dowd ambaye yupo nchini kwa lengo la kuangalia na kufanya tathmini ya aina ya miradi itakayoweza kutekelezwa benki hiyo.

Akiwa hapa nchini, pamoja na mambo mengine Dowd atatembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

Mashindano ya Gofu Afrika kufanyikia Accra

0

Timu ya Taifa ya mchezo wa gofu imeelekea nchini Ghana kushiriki mashindano ya Afrika kwa mchezo huo huku ikisema kuwa ipo tayari kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Akikabidhi bendera ya taifa kwa timu hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) – Alex Mkenyenge ameitaka timu hiyo kuwa na uzalendo.

Naye Rais wa Chama cha Gofu Tanzania kwa wanawake – Sophia Viggo pamoja na nahodha wa timu hiyo Madina Idd wamewashukuru wadau mbalimbali wa mchezo wa gofu kwa kuiunga mkono timu hiyo wakati wote wa maandalizi.

Mashindano ya Afrika kwa mchezo wa gofu yanafanyikia mjini Accra nchini Ghana kuanzia Agosti 29 hadi Septemba Nne mwaka huu na yanashirikisha timu kutoka mataifa 26.

Mbao FC wapanda kileleni mwa Ligi Kuu

0

Wabishi wa Mwanza, Mbao FC wamepanda kileleni mwa ligi kuu Tanzania Bara baada ya kupata ushindi wa ugegeni wa bao mbili kwa moja dhidi ya Stand United – Chama la Wana ya Shinyanga.

Pamoja na Stand United kutangulia kupata goli kwenye dakika ya 31 kupitia kwa Sixtus Sabela lakini walishindwa kulinda goli hilo na Mbao FC kufunga magoli hayo mawili kupitia kwa Said Hamis kwenye dakika ya 54 na Pastory Athanas akapigilia goli la ushindi kwenye dakika ya 59.

Huo ni ushindi wa pili wa Mbao FC tangu kuanza kwa msimu wa ligi kuu baada ya kupata ushindi wa bao moja kwa bila kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya wapinzani wao wa mji mmoja Alliance FC .

Nao mabingwa wa kombe la Shirikisho Mtibwa Sugar wamepata ushindi wao wa kwanza kwenye ligi kuu msimu huu baada ya kuifunga timu ngumu ya Tanzania Prisons bao moja kwa bila, bao lililofungwa kwenye dakika ya 37 na mshambuliaji wa kati Stamili Mbonde.

Katika michezo mingine Ruvu Shooting, – wazee wa kupapasa wamebanwa mbavu na kutoka sare ya bao moja kwa moja na timu mpya ya KMC, huku Wanapaluhengo Lipuli FC wakiendeleza sare baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja na JKT Tanzania.

Wakili wa Bobi Wine azuiliwa kuingia Uganda

0

Wakili wa kimataifa aliyepewa kazi ya kumwakilisha Mbunge wa Kyadondo Mashariki nchini Uganda, – Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine amezuiwa kuingia nchini humo.

Robert Amsterdam ambaye ni raia wa Canada ameorodheshwa kama mtu asiyetakiwa na serikali ya Uganda.

Amsterdam ni miongoni mwa mawakili walioorodheshwa kumtetea Bobi Wine katika kesi yake ambapo ameshtakiwa kwa uhaini.

Jukumu la Amsterdam ambaye huendesha shughuli zake kupitia kampuni ya Amsterdam and Partners iliyo na ofisi katika miji wa Washington nchini Marekani na London nchini Uingereza limetajwa kuwa ni kufanya masuala ya kiufundi, kutoa ushauri na kusaidia katika utafiti.

Bobi Wine amekuwa akizuiliwa rumande katika gereza la Gulu akiwa pamoja na watuhumiwa wengine 33 kwa madai ya kuurushia mawe msafara wa Rais Yoweri Museveni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arua.