SGR yakamilikiwa kwa asilimia 22

0

Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – Standard Gauge awamu ya kwanza kutoka jijini Dar Es Salaam hadi Morogoro, umekamilika kwa asilimia 22 huku katika baadhi ya maeneo shughuli za ujenzi ukiwa umepiga hatua.

Licha ya kuwepo kwa changamoto katika mradi huo, shughuli za ujenzi wa mradi huo zinafanyika usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.

Katika kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa maarufu kama Standard Gauge, bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania –TRC wamefanya ukaguzi katika mradi huo kuanzia jijini Dar Es Salaam hadi Kilosa mkoani Morogoro.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa, amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo kutoka jijini Dar Es Salaam hadi Morogoro inafanyika kwa saa 24 ili kuhakikisha mradi huo unajengwa na kukamilika kwa wakati.

TBC imeshuhudia baadhi ya madaraja yakiwa yamekamilia kwa zaidi ya asilimia 70 likiwemo daraja ambalo litawezesha njia ya reli kupita juu na sehemu ya chini ya daraja hilo itatumika kama barabara kwa ajili ya magari.

Watoto washinikiza uchunguzi kifo cha mwenzao

0

Watoto wa shule ya msingi Kibeta katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wamegoma kuingia darasani wakishiniza uchunguzi ufanyike kubaini chanzo cha kifo cha mwanafunzi mwenzao wa darasa la tano Spelius Eradius aliyefariki dunia muda mfupi baada ya kupewa adhabu ya viboko.

Mtoto huyo alipewa adhabu na mmoja wa walimu shuleni hapo akituhumiwa kuiba pochi ya mwalimu.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Augustino Ollomi amesema mwalimu anayedaiwa kumchapa mtoto huyo anashikiliwa na polisi kwa sababu za kiusalama na uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

Kamanda Ollomi alifika katika shule ya msingi Kibeta na kuwatuliza wazazi na watoto ambao hatimaye walikubali kuendelea na masomo.

Marekani na Kenya kukuza biashara

0

Rais Donald Trump wa Marekani amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya mjini Washington na kugusia zaidi masuala ya biashara na usalama.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani imesema kuwa akiwa katika ziara yake ya siku nne nchini Marekani, Rais Kenyatta na Rais Trump wamekubaliana na kutangaza mikataba ya jumla ya dola milioni 900 za Kimarekani.

Rais Kenyatta ni kiongozi wa tatu kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara kukaribishwa Ikulu ya Marekani na kufanya mazungumzo na Rais Trump.

Akizungmza mara baada ya mazunguzo yake na Rais Trump, Rais Kenyatta amesema kuwa Kenya imekuwa na ushirikiano mzuri na wa kipekee na Marekani katika masuala ya ulinzi na usalama hasa katika vita dhidi ya ugaidi na kinachofanyika hivi sasa ni kuimarisha uhusiano katika masuala ya biashara pamoja na uwekezaji.

Kwa upande wake Rais Trump ameelezea kufurahishwa na pendekezo lililowasilishwa na kampuni ya ujenzi kutoka nchini Marekani, – Bechtel Corporation la kutaka kupewa kandarasi ya ujenzi wa barabara ya kisasa ya kutoka Nairobi kwenda Mombasa nchini Kenya ambapo mataifa hayo mawili yamekubaliana kuendelea na majadiliano zaidi ili kuafikiana kuhusu ufadhili wa ujenzi huo.

Iran yapingana na Marekani kuhusu vikwazo

0

Marekani imesema kuwa mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu wa kivita haina uwezo wa kusikiliza kesi ya madai ya kuzuia vikwazo ambavyo nchi hiyo imeiwekea Iran.

Iran inataka kuwasilisha madai yake kwenye mahakama hiyo ili kuizuia Marekani kuiwekea vikwazo vipya vya kiuchumi.

Vikwazo hivyo vipya viliwekwa na Marekani dhidi ya Iran wiki mbili zilizopita baada ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kutupilia mbali makubaliano ya mpango wa nyuklia yaliyofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa mwaka 2015.

Mourinho ataka vyombo vya habari kumuheshimu

0

Meneja wa Manchester United, – Jose Mourinho amevitaka vyombo vya habari vya England kumpa heshima kutokana na mafanikio yake kwenye soka la nchi hiyo.

Mourinho ameyasema hayo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mchezo dhidi ya Tottenham Hot Spurs uliomalizika kwa kichapo cha mabao matatu kwa nunge ambapo amebainisha kuwa kichapo hicho si kitu kwani ana mafanikio makubwa kuliko kipigo ilichokipata timu yake hivyo aheshimiwe.

Mourinho amesema kuwa vyombo vya habari vimekuwa vikimsakama haijalishi awe ameshinda ama amefungwa kwani akishinda vinamripoti kuwa ameshinda lakini timu yake imecheza vibaya.

Mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Mourinho alienda moja kwa moja kwenye jukwaa la mashabiki wa Manchester United ambao walisalia uwanjani kwa dakika kadhaa baada ya kuisha kwa mchezo ambao walimpigia makofi wakionyesha kumuunga mkono.

Kwenye mchezo huo uliochezwa katika dimba la Old Trafford, mabao ya Man United yalifungwa na Harry Kane na Lucas Moura.

Kichapo hicho kimeipeleka Man United kwenye nafasi ya 13 ya msimamo wa ligi kuu ya England ikiwa na alama tatu baada ya michezo mitatu huku Tottenham ikikwea hadi nafasi ya pili nyuma ya vinara Liverpool.

Salah aingia kwenye mgogoro na EFA

0

Nyota wa timu ya Misri na klabu ya Liverpool, -Mohamed Salah ameingia kwenye mgogoro na chama soka nchini Misri (EFA) baada ya chama hicho kupuuza malalamiko yake yanayohusu kukiukwa kwa haki za matangazo.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amekishutumu chama hicho kwa kumuingiza kwenye sintofahamu na wadhamini wake ambao ni kampuni ya mawasiliano ya Vodafone baada ya EFA kutumia picha ya Salah kuitangaza kampuni ya WE ambayo ni kampuni pinzani ya Vodafone.

Akitumia mtandao wake wa kijamii wa Twitter, – Salah amesema kuwa alituma barua kadhaa kwa EFA lakini chama hicho kimezipuuza na kusema haelewi kwanini hajibiwi.

Hatua hiyo imezua tafrani nchini Misri ambapo taarifa za ndani zimeeleza kuwa mchezaji huyo anapanga kuisusia timu ya taifa ambayo mwezi Septemba mwaka huu itacheza na Niger kwenye mchezo wa kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika.

Hata hivyo EFA imekanusha suala la Salah kugomea mchezo huo kwa kusema kuwa habari hizo sio sahihi kwani Salah hajawasilisha ombi hilo.

Wawrinka ambwaga Dimitrov

0

Nyota wa mchezo wa tenisi Stan Wawrinka amembwaga Grigor Dimitrov katika mzunguko wa kwanza wa mashindano ya wazi ya Marekani kwenye uwanja wa Flushing Meadows jijini New York.

Hii ni mara ya pili mfululizo ambapo Wawrinka anamtoa Dimitrov kwenye michuano mikubwa katika hatua za awali ambapo katika mzunguko huo amemfunga seti tatu kwa bila za 6-3, 6-2 na 7-5.

Nyota huyo raia wa Switzerland alikosa michuano ya mwaka 2017 kutokana na kuuguza majeraha ya goti alilofanyiwa upasuaji mara mbili na kumfanya ashindwe kutetea taji alilotwaa mwaka 2016.

Katika matokeo mengine Andy Murray ameanza vyema mashindano hayo mara baada ya kumfunga James Duckworth wa Australia seti tatu kwa moja za 5-7, 6-3, 7-5 na 6-3 kwenye uwanja wa Louis Armstrong.

Murray atakutana na mkongwe Fernando Verdasco wa Hispania katika mchezo wa hatua ya pili.

Ashikiliwa kwa mauaji Singida

0

Jeshi la polisi mkoani Singida linamshikilia Naligwa John mwenye umri wa miaka 23 mkazi wa kijiji cha Mgundu wilayani Iramba kwa tuhuma za kumdhalilisha na kumkaba shingo hadi kufa mtoto mwenye umri wa miaka 12 mwanafunzi wa darasa la Nne katika shule ya msingi Mgundu.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Singida, – Sweetbert Njewike amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya mauaji hayo mbele ya mdogo wa marehemu mwenye umri wa miaka Tisa wakiwa wanachunga mifugo.

Akizungumza na Waandishi wa habari mjini Singida, Kamanda Njewike amesema kuwa baada taarifa za tukio hilo kumfikia mama mzazi wa marehemu, mama huyo alipiga kelele kuomba msaada kwa wananchi ambao walijitokeza na kuanza kumtafuta mtuhumiwa huyo na hatimaye kumkamata akiwa katika harakati za kutoroka.

Kufutia tukio hilo, Kamanda huyo wa polisi wa mkoa wa Singida ametoa angalizo kwa wazazi wa jamii ya wafugaji kuhakikisha usalama wa watoto wao wanapokua kwenye kazi ya kuchunga mifugo.

Jeshi la polisi mkoani Singida linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na pindi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.