Wachezaji wa Real Madrid wazoa tuzo

0

Timu ya Real Madrid ya nchini Hispania ambayo ni mabingwa mara tatu mfululizo wa taji la ligi ya mabingwa Barani Ulaya baada ya kuinyuka Liverpool mabao Matatu kwa Moja katika fainali ya msimu uliopita, imefanya vizuri katika tuzo zote ambazo wachezaji wake waliwania.

Mlinda mlango wa timu hiyo Keylor Navas ameshinda tuzo ya kipa bora wa msimu, Sergio Ramos ametwaa tuzo ya beki bora huku Cristiano Ronaldo aliyehamia Juventus akishinda tuzo ya mshambuliaji bora wa msimu.

Katika tuzo hizo, nyota wa kimataifa wa Croatia, -Luka Modric ameshinda tuzo ya kiungo bora wa msimu pamoja na tuzo ya jumla ya mchezaji bora wa ulaya wa UEFA kwa msimu wa 2017/2018 baada ya kuwabwaga Cristiano Ronaldo na Mohamed Salah.

Modric mbali na kushinda taji la ligi ya mabingwa Barani Ulaya na kikosi cha Real Madrid, aliisadia nchi yake ya Croatia kutinga fainali ya kombe la FIFA la dunia ambapo walipoteza mbele ya Ufaransa.

Nyota huyo amesema kuwa anajisikia furaha kushinda tuzo hizo na kwamba huu ni mwaka bora katika maisha yake ya soka kwa kuwa ndoto aliyoiota kwa muda mrefu tangu aanze kuichezea timu ya taifa imetimia.

Raia wanane wa kigeni washikiliwa na polisi Mara

0

Polisi mkoani Mara inawashikilia wafanyakazi wanane raia wa Russia na Armenia kwa tuhuma za kufanya kazi nchini bila ya vibali huku kampuni inayomiliki mgodi wa MMG Musoma Vijijini ikituhumiwa kunyayasa wafanyakazi.

Tukio hilo limejiri kufuatia ziara ya ghafla ya Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko katika mgodi huo.

Katika tukio hilo raia hao wa kigeni wasiokuwa na vibali wamekutwa wamefungiwa vyumbani huku baadhi ya wafanyakazi wakiwa wamefungiwa vyooni.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko amekagua maeneo mbalimbali ya mgodi huo na kuzungumza na wafanyakazi ambapo amebaini ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uwekezaji.

Kampuni hiyo ya MMG iliwafungia vyumbani wafanyakazi wa kigeni wasiokuwa na vibali vya kufanyakazi na vibarua waliokuwa hawana vifaa vya kufanyia kazi walifungiwa chooni.

Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko ameiagiza kampuni hiyo ya MMG kuhakikisha inawapatia wafanyakazi wake mikataba ya ajira ndani ya siku saba.

Vijana wanaoishi kambi ya Nunge watakiwa kuondoka

0

Vijana wanaoishi katika kambi ya kulea wazee wasiojiweza ya Nunge wilayani Kigamboni jijini Dar Es Salaam wametakiwa kuondoka kwenye kambi hiyo ifikapo kesho kwa kutokuwa na sifa ya kuendelea kuishi hapo.

Akizungumza kambini hapo Mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Sara Msafiri amesema wameamua kuwaondoa kutokana na agizo la serikali lililowataka kuondoka tangu mwezi Januari mwaka 2016 lakini hadi sasa vijana hao bado wanaendelea kuishi kambini hapo.

Vijana wapato 34 ambao ni yatima waliokuwa wanaishi kambini hapo walichukuliwa kutoka kwenye makao ya taifa ya watoto Kurasini baada ya kupilitiza umri wa utoto.

Rais Magufuli awataka viongozi kuzingatia sheria

0

Rais John Magufuli amewataka viongozi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria pamoja na kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita wakati akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa wilaya hiyo.

Amesisitiza kuwa viongozi wote wajenge utaratibu wa kusoma sheria na kujiepusha kutumiwa kwa maslahi ya watu binafsi.

Rais Magufuli ametolea mfano mgogoro wa makontena yanayodaiwa kuwa na samani za shule na yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) katika bandari ya Dar es salaam na kusema kuwa makontena hayo yanapaswa kulipiwa kodi kwa mujibu wa sheria.

Amesisitiza kuwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango ndiye mwenye dhamana ya kupokea misaada kwa niaba ya serikali na sio mkuu wa mkoa.

“Kwa mujibu wa sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada Namba 30 ya mwaka 1974 (kama ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya mwaka 2003) kifungu cha 3, 6, 13 na 15, Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye mamlaka ya kukopa nje na ndani, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali.

“Kwa msingi huo, hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kukopa, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya serikali bila mtu huyo kukasimiwa mamlaka hayo na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria hiyo” amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Madiwani wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu matumizi ya fedha za bajeti ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa katika miradi na huduma zenye kujibu kero na kuboresha maisha ya wananchi badala ya kuacha zikitumiwa kulipana posho za vikao na safari zisizo na tija.

“Nafahamu kuwa hata nyie Madiwani huwa mnakaa kikao siku moja na mnataka kulipwa posho ya siku mbili au tatu, au mtumishi wa halmashauri anasafiri kwa siku mbili lakini anaandikiwa posho za siku nne, nataka mchezo huu ukome, elekezeni fedha kwenye mahitaji muhimu ya wananchi, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya simamieni hilo” amesema Rais Magufuli.

Katika mkutano huo ambapo alianza kwa kupokea maswali, kero na maoni ya wafanyakazi na viongozi, Rais Magufuli amewahakikishia kuwa serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa kujitegemea na kutatua kero za wananchi wakiwemo wafanyakazi wote bila kubagua na amewataka viongozi wa Wilaya ya Chato kuwa wabunifu wa namna ya kuharakisha maendeleo ya wananchi badala ya kubweteka kwa kutegemea kupendelewa naye kwa kigezo cha kuwa mwananchi wa Chato.

Wanasheria wa serikali wakutana Dodoma

0

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amewataka wanasheria wa serikali kuhakikisha sheria wanazozisimamia zinakidhi matarajio ya maendeleo na ustawi wa wananchi maskini.

Jaji Mkuu ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wanasheria walio katika utumishi wa umma unaofanyika jijini Dodoma, mkutano unaowakutanisha wanasheria 900 kutoka wizara mbalimbali, idara , taasisi za serikali na mamlaka za serikali za mitaa.

Akitilia mkazo sheria zinazolenga kuwasaidia wananchi maskini, Jaji Mkuu amesema kuwa sheria hizo ni lazima ziwasaidie kunufaika na Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo ni pamoja na Watanzania kuishi maisha yanayolingana na uchumi wa kati na kujenga utawala bora.

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma pia amewataka wanasheria hao wa serikali kuhakikisha kuwa ubora wa huduma za kisheria wanazozitoa zinakidhi mahitaji ya uchumi wa kati na kutumia ujuzi, weledi na uadilifu wao katika kutoa ushauri kwa maslahi ya Taifa.

Ametahadharisha kuwa ikiwa wanasheria hao watashindwa kutumia ujuzi wao, weledi na uadilifu katika kutoa ushauri wa kisheria wanaweza kusababisha mkanganyiko miongoni mwa jamii ya Watanzania.
Baadhi ya mada zitakazowasilishwa katika mkutano huo ni nafasi na majukmu ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itayotolewa na Mwanasheria Mkuu wa serikali Dkt Adelardus Kilangi, nafasi na majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na nafasi na majukumu ya ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Meli za uvuvi za Uingereza na Ufaransa zagongana

0

Meli moja ya uvuvi ya nchini Uingereza imegongana na meli nyingine ya uvuvi kutoka nchini Ufaransa huku wavuvi waliokuwa ndani ya vyombo hivyo vya majini wakitupiana maneno makali na kukaribia kupigana.

Wavuvi hao wamekuwa wakigombea eneo la kuvulia samaki ambalo wavuvi kutoka nchini Ufaransa wanaona kama wenzao kutoka Uingereza wamevamia eneo la nchi yao la bahari na hivyo kuwafanya wakose samaki.

Wavuvi wa Ufaransa wanakasirika kuwa wenzao Waingereza wamekuwa na tabia ya kuiba samaki wao kwa kuvua na kurejea makwao kwa amani huku nchini mwao wakipewa sheria kali kuhusiana na eneo hilo la baharini.

Hata hivyo wavuvi kutoka nchini Uingereza wanasema eneo hilo ni huru na wako radhi kuvua bila kufungwa na sheria yoyote.

Miili ya waliouawa yarudishwa Namibia

0

Serikali ya Ujerumani imerudisha mabaki ya miili ya watu wa kabila la Horero kutoka nchini Namibia waliouwa na wakoloni wa Kijerumani katika harakati za kugombea haki nchini mwao wakati wa utawala wa kikoloni.

Wanaharakati nchini Namibia wamekuwa wakiitaka Ujerumani kuliomba kabila hilo radhi na kurejesha miili ya watu wao ambayo ilichukuliwa baada ya kuuawa kikatili na wengine kunyongwa katika ardhi ya mababu zao.

Takribani watu Elfu 75 kutoka kabila la Herero na kabila lingine nchini Namibia waliuawa na Wajerumani zaidi ya miaka 100 iliyopita baada ya majeshi ya Ujerumani kuivamia nchi hiyo ikitafuta makoloni Barani Afrika.

Waliosombwa na maji Myanmar waendelea kuokolewa

0

Waokoaji nchini Myanmar wanaendelea na zoezi la kuwaokoa watu waliosombwa na maji baada ya bwawa moja kubwa nchini humo kupasuka na maji yake kusambaa hovyo hadi katika makazi ya watu.

Zaidi ya watu Sitini Elfu wamelazimika kuyahama makazi yao huku vijiji vipatavyo mia moja vikiwa vimefunikwa na maji.
Habari kutoka nchini Myanmar zinasema kuwa watu wawili hawajulikani walipo baada ya kusombwa na maji hayo.

Nchi ya Myanmar katika siku za hivi karibuni imekuwa ikishuhudia mvua kubwa iliyosababisha mafuriko na kufanya kingo za mito mingi kupasuka.
Idara ya hali ya hewa nchini Myanmar imetoa taarifa inayosema kuwa mvua hizo ambazo ni za msimu zitaendelea kunyesha kwa siku kadhaa.