Ajali yaua Sita Arusha

0

Watu Sita wamekufa katika ajali ya barabarani iliyotokea kwenye eneo la Naja Mti Mmoja wilayani Monduli mkoani Arusha.

Ajali hiyo imehusisha roli lililokua lilkitoka katika kambi za wakimbizi mkoani Kigoma ambalo limegongana na gari dogo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Arusha ambaye pia ni Mkuu wa mkoa huo Mrisho Gambo amesema kuwa miili ya watu waliokufa katika ajali hiyo imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Arusha, – Mount Meru.

Majeruhi wawili wa ajali hiyo wamelazwa katika hospitali ya Seliani ambapo Gambo amewajulia hali.

Kaimu Mganga mkuu wa mkoa wa Arusha, – Omari Chande amesema kuwa amepokea miili ya watu Watano, minne ikiwa ni ya raia wa kigeni huku mmoja ukiwa ni wa Mtanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya dharura katika hospitali ya Seliani Dkt Peter Mabula amesema kuwa amepokea majeruhi wawili wa ajali hiyo pamoja na mtu mmoja aliyekuwa na hali mbaya ambaye baadaye alifariki dunia.

Tanzania yaialika China kuwekeza

0

Mkutano wa Wakuu wa nchi na serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaanza Septemba Tatu jijini Beijing nchini China.

Katika mkutano huo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye tayari yuko nchini China anamuwakilisha Rais John Magufuli.

Akizungumza wakati wa mkutano wa wakuu wa kampuni na mashirika mbalimbali ya biashara jijini Beijing ikiwa ni maandalizi ya mkutano huo wa FOCAC, Waziri mkuu Kassim Majaliwa imeialika China kuwekeza katika ujenzi wa jiji la Dodoma hasa miundombinu pamoja na nyumba za watumishi .

Amesema kuwa ni wakati muafaka kwa kampuni kutoka nchini China kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu na sekta ya madini.

Watakiwa kuwatambua wageni

0

Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi nchini Naibu Kamishna Liberatus Sabas amewaomba wakazi wa kijiji cha Masuguru mkoani Mtwara kuwatambua wageni wanaoingia kijijini hapo wakitokea maeneo mbalimbali ya nchi na hata nchi jirani ya Msumbiji.

Naibu Kamishna Sabas amesema kuwa amelazimika kutoa ombi baada ya kubainika kuwa asilimia 90 ya silaha zilizopatikana kufuatia operesheni iliyofanyika mkoani Mtwara kupatikana katika kijiji hicho.

Ametumia mkutano huo kuwaonya watu wote ambao wamekua wakifanya vitendo vya uhalifu na kukimbilia nchi jirani ya Msumbiji ambako huko pia wamekua wakijiunga na vikundi vya uhalifu.

Mkuu huyo wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi Nchini Naibu Kamishna Liberatus Sabas amebainisha kuwa kwa sasa kuna ushirikiano baina ya Tanzania na Msumbiji katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu, hivyo mhalifu anaweza kukamatwa kwa urahisi katika pande hizo mbili.

TADB yasema ina mtaji wa kutosha

0

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Nchini (TADB) Japhet Justine amesema kuwa benki hiyo ina mtaji wa kutosha kwa sasa kwa ajili ya kuwahudumia wakulima.

Justine amesema kuwa kwa mujibu wa upembuzi uliofanywa mwaka 2011 wakati wa mchakato wa kuanzisha TADB, mtaji unaohitajika kwa ajili ya kuiwezesha benki hiyo ifikie malengo yake na kutimiza matarajio ya serikali na wakulima ifikapo mwaka 2035 ilikuwa ni Dola Milioni mia Tano za Kimarekani ambazo ni sawa na Shilingi Bilioni 800.

Amefafanua kuwa tangu kuanza shughuli rasmi za ukopeshaji mwaka 2015, serikali imekuwa ikiendelea kuipatia benki hiyo mtaji.

Hadi kufikia mwisho wa mwezi wa Julai mwaka 2018, Benki ya Kilimo imetoa mikopo ya zaidi shilingi Bilioni 48.6 ikiwa ni ukuaji wa shilingi Bilioni 37.2 katika kipindi cha miezi saba ya mwaka 2018.

Mikopo hiyo imewanufaisha zaidi ya wakulima Laki Tano na Ishirini Elfu.

Marekani yatishia kujiondoa WTO

0

Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kuiondoa nchi yake kwenye Shirika la Biashara Duniani (WTO) iwapo shirika hilo litashindwa kubadilisha utendaji wake kwa nchi hiyo.

Mara nyingi Rais Trump amekuwa akidai kuwa WTO imekua haitendi haki kwenye maamuzi yake dhidi ya Marekani na kwamba imekua ikifanya kazi zenye manufaa kwa nchi mbalimbali isipokua kwa nchi hiyo.

Shirika hilo la Biashara Duniani lilianzishwa kwa ajili ya kusimamia sheria za biashara duniani na kutatua tofauti za kibiashara kati ya nchi na nchi.

Hivi karibuni Marekani ilipinga uchaguzi wa majaji wapya wa WTO ambao kazi yao ni kujadili masuala ya kibiashara ya nchi mbalimbali na hatimaye kuyatolea maamuzi.

Kansela Angela Merkel ziarani Nigeria

0

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameanza ziara yake nchini Nigeria ikiwa ni ziara ya mwisho kwa nchi za Afrika Magharibi.

Kabla ya kuanza ziara yake nchini Nigeria, Kansela Merkel alikua na ziara katika nchi za Senegal na Ghana ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo.

Lengo la ziara hiyo ya Kansela wa Ujerumani nchini Nigeria ni kukuza uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi yake na nchi hiyo pamoja na kuangalia namna ya kupunguza suala la wahamiaji wanaoingia Barani Ulaya.

Wakati wa mazungumzo yake na Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo, Kansela Angela Merkel anatarajiwa kugusia masuala ya ulinzi pamoja na uchaguzi mkuu ujao wa Nigeria.

Bobi Wine azuiliwa kwenda nje ya nchi

0

Mbunge wa upinzani nchini Uganda ambaye pia ni Mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine anayedaiwa kupigwa na kuteswa baada ya kukamatwa mapema mwezi huu, amezuiliwa kuondoka nchini humo kwenda kupatiwa matibabu nje ya nchi.

Mwanasheria wa mbunge huyo Robert Amsterdam amedai kuwa mteja wake Bobi Wine amezuiliwa kuingia katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Uganda na badala yake amechukuliwa na polisi ambao wanadaiwa kumpeleka katika hospitali ya serikali.

Amsterdam amesisitiza kuwa kipaumbele cha Bobi Wine kwa sasa ni kupata matibabu nje ya nchi na si kutoroka nchini humo.

Kabla ya kuzuiliwa kwa Bobi Wine katika uwanja huo wa ndege wa Kimataifa wa Uganda, mbunge mwingine wa upinzani Francis Zake pia alizuiliwa kwenye uwanja huo kwenda kupatiwa matibabu nje ya nchi.

Bobi Wine anakabiliwa na makosa ya uhaini, kufuatia tukio la kushambuliwa kwa mawe gari la Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni na aliachiliwa siku ya Jumatatu kwa dhamana kutoka kizuizini alikokuwa akishikiliwa huku ikielezwa kuwa yuko katika hali mbaya.

Venus na Serena Williams kukutana US OPEN

0

Ikiwa ni miaka Ishirini imepita tangu walipokutana kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kuwania taji kubwa la tenisi duniani (Grandslum), wanadada ndugu Venus na Serena Williams watakutana katika hatua ya 16 bora ya mashindano makubwa ya tenisi ya wazi ya Marekani (US OPEN) baada ya kushinda michezo yao ya hatua ya tatu.

Mchezo huo unachezwa usiku wa kuamkia Septemba Mosi mwaka huu kwenye dimba la Arthur Ashe na itakuwa ni mara ya 30 kwa wanadada hao ndugu kukutana ambapo kwa mara ya mwisho walikutana katika mashindano ya Indian Wells mwezi Machi mwaka huu na Venus kuibuka mshindi.

Akizungumzia mchezo huo Venus ambaye ni mkubwa kwa Serena kwa tofauti ya miaka Miwili amesema kuwa angalau kutakuwa na usawa katika mchezo huo akirejea fainali ya mashindano ya wazi ya Australia walipokutana mapema mwaka 2017 ambapo Serena alikuwa na ujauzito wa mwanaye wa kike aitwaye Olympia.

Miongoni mwa michezo yao ya kukumbukwa ni pamoja na ule wa mwaka 1998 katika mashindano ya wazi ya Australia kwenye hatua ya pili ambapo Venus alikua na umri wa miaka 17 huku akishika nafasi ya 16 kwenye viwango vya ubora, aliibuka na ushindi wa seti mbili kwa bila za 7-6 na 6-1 dhidi ya mdogo wake Serena ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 15 na alikua katika nafasi ya 53 kwenye viwango vya ubora.

Mwaka 2003 kwenye fainali za Australian Open, Serena alishinda taji lake la kwanza la mashindano hayo na kuwa mwanamke wa kwanza baada ya Steffi Graf mwaka 1994 kushinda mataji manne ya Grandslum ndani ya mwaka mmoja lakini ukawa mchezo wa nne kwa dada yake Venus kupoteza mfululizo kwa Serena.

Mwaka 2009 kwenye fainali za mashindano ya Wimbledon, – Serena alimzuia dada yake Venus kushinda taji la Tatu mfululizo la mashindano hayo baada ya kumnyuka katika mchezo huo na kutwaa taji la Tisa katika kipindi cha miaka Sita.

Mwaka 2017 kwenye fainali za Australian Open ambazo zilikuwa ni mara yao ya mwisho kukutana katika mashindano makubwa, Serena aliweka rekodi ya kushinda taji lake la 23 lenye hadhi ya grandslum na kutangaza kuwa wakati huo alikuwa na ujauzito wa miezi Mitatu.

Wanandugu hao kwa pamoja wamekusanya mataji 30 ya Grandslum katika mchezo wa tenisi tangu Venus aliposhinda mchezo wa hatua ya pili ya mashindano ya wazi ya Australia mwaka 1998.