Nyota wa Taifa stars wanaocheza nje wawasili nchini

0

Nyota wanne wa timu ya Taifa ya soka ya Tanzania (Taifa stars) wanaocheza soka nje ya nchi wamewasili nchini na kuanza kufanya mazoezi na wenzao tayari kwa mchezo dhidi ya Uganda utakaochezwa mwishoni mwa juma nchini Uganda.

Nyota hao ni nahodha Mbwana Samatta, Ramadhan Kessy, Rashid Mandawa na Thomas Ulimwengu.

Nyota wengine waliotarajiwa kuwasili ni mlinzi Abdi Banda, Simon Msuva, Shabaan Idd Chilunda, Farid Mussa na nahodha msaidizi Himid Mau.

Kikosi hicho cha kocha Emmanuel Amonike kilianza mazoezi wiki moja iliyopita kwa ajili ya kujianda na mchezo huo wa kufuzu kwa mataifa ya Afrika dhidi ya Uganda ambapo wachezaji alioanza nao mazoezi walikuwa wanacheza soka hapa nyumbani.

Huo ni mchezo wa pili kwa Taifa Stars baada ya kutoka sare katika mchezo wa kwanza dhidi ya Lesotho mwaka mmoja uliopita na hivyo wanahitaji kushinda ili kuweka hai matumaini yao ya kufuzu kwa michuano hiyo mikubwa Barani Afrika.

Tanzania yahitaji wawekezaji kutoka China

0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania inahitaji wawekezaji wakubwa kutoka China ambao watawekeza kwenye viwanda vya mazao ya kilimo, samaki na mifugo.

Akizungumza jijini Beijing na Waziri wa Kilimo wa China,- Han Changfu, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Tanzania imeamua kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda hivyo China ni nchi sahihi kushirikiana nayo kwa sababu ina wawekezaji wa kutosha wenye ujuzi mkubwa katika sekta hizo.

Aidha Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Tanzania inahitaji kupata soko la mbaazi na soya nchini China ili kuwawezesha wakulima kuwa na soko la uhakika la mazao hayo.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo wa China, Han Changfu amesema kuwa nchi yake iko tayari kutoa elimu na mafunzo kwa Watanzania hasa maafisa ili wafanye kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Mkutano wa kujadili viumbe vamizi wafunguliwa Arusha

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba amefungua mkutano wa wadau wa mazingira unaojadili hali halisi,changamoto na mikakati ya kukabiliana na viumbe vamizi nchini.

Mkutano huo unafanyika mkoani Arusha ikiwa ni matokeo ya ziara ya Waziri Makamba aliyoifanya mwezi Machi mwaka 2017 katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na kubaini kuwa hifadhi hiyo inakabiliwa na tatizo la viumbe vamizi.

Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ni watafiti kutoka Chuo Kikuu  cha Nelson Mandela cha mkoani Arusha,Wabunge, Wenyeviti na Kaimu wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali.

 

Mkutano wa 12 wa Bunge waanza

0

Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano umeanza kwa Spika wa Bunge Job Ndugai kumuapisha Mhandisi Christopher Chizza ambaye ni Mbunge wa jimbo la Buyungu mkoani Kigoma aliyechaguliwa katika uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika Agosti 12 mwaka 2018.

Shughuli nyingine itakayofanyika kwenye mkutano huo utakaomalizika Septemba 14 ni kupitisha kwa hatua zilizobaki miswada Mitano ya sheria ambayo ilisomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Kumi na Moja Bunge.

Maswali 125 ya kawaida yataulizwa na mengine 16 ya papo kwa papo yataulizwa kwa Waziri Mkuu wakati wa mkutano huo wa 12 wa Bunge.

Rais Magufuli afanya uteuzi

0

Rais John Magufuli amemteua Dkt John Jingu kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kabla ya uteuzi huo Dkt Jingu alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Ikulu imesema kuwa Dkt Jingu anachukua nafasi ya Sihaba Nkinga ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Wakati huohuo Rais Magufuli amemteua Gabriel Malata kuwa Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Kabla ya uteuzi huo Malata alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Kesi za Madai, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Malata anachukua nafasi ya Hilda Kabisa ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Mkutano wa 12 Bunge kuanza kesho

0

Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajiwa kuanza Septemba Nne na kumalizika Septemba 14 mwaka huu kwa kufanya shughuli mbalimbali.

Shughuli hizo ni pamoja na kupitisha kwa hatua zilizobaki miswada Mitano ya sheria ambayo ilisomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Kumi na Moja.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dodoma na Kitengo cha Habari, Elimu kwa Umma na Mawasiliano cha Ofisi ya Bunge imesema kuwa shughuli nyingine itakayofanyika ni kula kiapo cha uaminifu kwa Mhandisi Christopher Chizza ambaye ni Mbunge wa jimbo la Buyungu mkoani Kigoma aliyechaguliwa katika uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika Agosti 12 mwaka 2018.

Maswali 125 ya kawaida yataulizwa na mengine 16 ya papo kwa papo yataulizwa kwa Waziri Mkuu wakati wa mkutano huo wa 12 wa Bunge.

Ajali yasababisha vifo vya watu watatu

0

Watu Watatu wamekufa papo hapo na mmoja kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha magari mawili katika eneo la Hedaru – Kadama wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kilimanjaro Hamis Issah amewataja watu waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Simon mbaga ambaye ni dereva wa gari aina ya scania, Ramadhan Jumanne dereva wa gari aina ya Kenta na mwingine ambaye ametambulika kwa jina moja la Mbongo.

Majeruhi katika ajali hiyo ni Said Tumaini ambaye amepatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Same na kuruhusiwa

IITA yasisitiza uzalishaji wa dawa ya Aflasafe

0

 

Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) imeanza kuwasisitiza wawekezaji wa Tanzania kuanzisha viwanda vya uzalishaji wa dawa ya kupambana na Sumukuvu ijulikanayo kama Aflasafe ili kunusuru uharibifu wa mahindi na karanga.

 

Akizungumza  jijini Dar es salaam wakati wa mdahalo wa wawekezaji,  mtaalam aliyefanya utafiti wa kupatikana kwa dawa hiyo Steve Kisakye amesema kuwa  dawa ya Aflasafe ipo katika mchakato wa kusajiliwa na Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPRI)  na imeshafanyiwa majaribio katika mikoa mbalimbali nchini.

 

Kwa upande wake afisa Kilimo Mkuu kutoka wizara ya kilimo Beatrice Pallangyo amewashauri wakulima nchini kutumia dawa hiyo ili kuepusha Sumukuvu inayoingia katika mazao hayo ya mahindi na karanga wakati wa mavuno na kuathiri afya za walaji.