Walia na sheria ya bao la ugenini

0

Makocha wa vilabu vikubwa Barani Ulaya wamelitaka Shirikisho la soka barani humo (UEFA) kuangalia uwezekano wa kupitia upya sheria ya bao la ugenini katika mashindano ya bara hilo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa UEFA ulioshirikisha makocha hao nchini Uswiss, Kaimu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Giorgio Marchetti amesema  wao wanafikiri kuwa katika wakati huu kufunga bao ugenini imekuwa jambo rahisi tofauti na miaka iliyopita,  hivyo sheria hiyo ni vema ifanyiwe mabadiliko.

Mkutano huo ambao ni wa mwaka umehudhuriwa na makocha wa vilabu vikubwa Barani Ulaya akiwemo kocha wa Manchester United,  – Jose Mourinho,  kocha wa Arsenal, – Unai Emery na mtangulizi wake Arsene Wenger, Massimiliano Allegri wa Juventus, Julen Lopetegui wa Real Madrid, kocha wa Napoli,- Carlo Ancelotti na Thomas Tuchel  kutoka Paris St-Germain.

Sheria hiyo ya bao la ugenini kwa mara ya kwanza ilianzishwa mwaka 1965 kwenye michuano ya kombe la washindi Barani Ulaya kama njia mbadala ya kupata mshindi tofauti na urushaji wa shilingi au kutumia uwanja wa ugenini kwa timu zote mbili (neutral ground) ili kuepuka baadhi ya gharama ikiwemo usafiri.

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UEFA Giorgio Marchetti amesema  kuwa makocha hao wa vilabu vikubwa Barani Ulaya wanaamini kuwa  sheria ya bao la ugenini inadumaza soka kwa kuwa inahamasisha timu ngeni katika mchezo kushambulia muda wote huku wenyeji wakijilinda kuhofia kuruhusu bao la nyumbani na  hivyo kupoteza ladha ya mchezo.

 

Waliokwamisha mradi wa maji kukiona

0

Rais John Magufuli ameagiza kuchukuliwa hatua watu wote  waliohusika kukwamisha kukamilika kwa mradi wa maji katika wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya Wakazi wa wilaya hiyo kumueleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kukosekana kwa maji safi na salama huku wilaya hiyo ikiwa na mradi mkubwa wa maji ambao haujawafaidisha.

Amesema kuwa serikali haiwezi kuvumilia kuona mkandarasi aliyekua akitekeleza mradi huo kushindwa kuukamilisha kwa muda wa miaka Minane wakati amekwishalipwa fedha.

Kufuatia hali hiyo, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Maji na  Umwagiliaji Profesa Makame Mbarawa  pamoja na  Katibu  Mkuu wa wizara hiyo Profesa Kitila Mkumbo kwenda wilayani Bunda ndani ya kipindi cha wiki moja ili kubaini chanzo cha kukwama kwa mradi huo.

Rais Magufuli amewahakikishia wakazi hao wa Bunda kuwa ni lazima watapata maji saji na salama kupitia mradi huo kwa kuwa suala hilo atalishughulikia yeye mwenyewe.

 

Wanafunzi wa darasa la Saba waendelea na mitihani yao

0

Wanafunzi wa darasa la Saba katika maeneo mbalimbali nchini wanaendelea na mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi iliyoanza mapema hii leo.

Mitihani hiyo inafanyika kwa muda wa siku mbili ambazo ni leo Septemba Tano na kumalizika siku ya kesho ambayo ni Septemba Sita.

Jumla ya watahiniwa 960,202 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo, watahiniwa wanaotoka katika shule 16,845.

Waandishi wa habari wa  TBC katika maeneo mbalimbali nchini wamesema kuwa ulinzi umeimarishwa katika maeneo ya shule, na wanafunzi wanafanya mitihani hiyo katika mazingira ya utulivu.

Rais Magufuli akutana na Mzee Msekwa

0

Rais John Magufuli amekutana na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Pius Msekwa na Mkewe Mama Anna Abdallah katika Ikulu Ndogo ya Nansio – Ukerewe mkoani Mwanza.

Baada ya mazungumzo yao, Mzee Msekwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kufanya ziara yake ya kwanza katika kisiwa cha Ukerewe tangu achaguliwe kuwa Rais, na kwa serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kisiwani humo ikiwa ni pamoja na ile ya maji, ujenzi wa barabara na ununuzi wa meli mpya katika ziwa Viktoria.

Mzee Msekwa pia amezungumzia utendaji kazi wa Rais Magufuli na serikali ya awamu ya Tano, ambapo amesema kuwa mageuzi makubwa yanayofanywa yanaandika historia kama alivyofanya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Kwa Nyerere tulisema kama sio juhudi zako Nyerere, maendeleo tungepata wapi, na huyu Rais Magufuli naye tutasema kama sio juhudi zako meli, Dreamliner, reli na mengine mengi tungepata wapi?” amesisitiza Mzee Msekwa.

Kwa upande wake Mama Anna Abdallah ambaye ni Waziri Mstaafu amemshukuru Rais Magufuli kwa kazi kubwa ya kujenga uchumi na kuwapa nafasi za uongozi wanawake wengi na ametoa wito kwa wanawake wote waliopata nafasi za uongozi kuonesha mfano mzuri kwa kuchapa kazi kwa juhudi, uadilifu mkubwa na kujiamini ili wengine wengi zaidi waendelee kupata nafasi.

“Nafurahishwa sana na kazi zinazofanywa na Mhe. Rais Magufuli, kwa hakika anatutendea mazuri mengi sana sisi Watanzania na sisi wanawake” amesema Mama Anna Abdallah.

Rais Magufuli amekutana na Mzee Msekwa na Mama Anna Abdallah kando ya ziara yake katika kanda ya ziwa ambayo inaendelea mkoani Mara.

Keita aapishwa kuiongoza Mali

0

Rais mpya wa Mali Ibrahim Boubcar Keita ameapishwa baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 12 mwaka huu.

Sherehe za kuapishwa kwa Keita zimefanyika katika viwanja vya Kouluba chini ya ulinzi mkali.

Agosti 20 mwaka huu mahakama ya kikatiba nchini Mali ilimthibitisha Keita kuwa mshindi wa kiti cha Urais na kutupilia mbali mashitaka yaliyofunguliwa na mpinzani wake Soumaila Sisse’s kwa madai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na vitendo vya rushwa.

Rais Magufuli aendelea kuunguruma Mwanza

0

Rais John Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa mkandarasi Nyanza Road Works anayejenga barabara ya Bulamba-Kisorya iliyopo mkoani Mara.

Rais Magufuli ameyasema hayo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo na kuiagiza wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha mkandarasi huyo anafanya kila linalowezekana ili ujenzi wa barabara hiyo ukamilike katika muda wa nyongeza ambao ni miezi 35.

Barabara hiyo ya Bulamba – Kisorya ina urefu wa Kilomita 51 na imeanza kujengwa mwaka 2014 kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni hamsini.

Kabla ya Rais Magufuli kuweka jiwe hilo la msingi la ujenzi wa barabara hiyo ya Bulamba – Kisorya iliyoko mkoani Mara, alizindua kiwanda cha Lakairo Industries Group Limited kilichopo wilayani Magu.

Akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho pamoja na wananchi waliojitokeza kumlaki, Rais Magufuli ameiagiza wizara za Fedha na Mipango na ile ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuwawezesha wawekezaji wazawa ili washiriki vizuri katika kuimarisha uchumi wa nchi.

Rais Magufuli pia alielekea wilayani Ukerewe ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Mwanza, ambapo amezindua mradi wa upanuzi wa chuo cha ualimu cha Murutunguru na mradi wa maji katika kijiji cha Nebuye wilayani humo.

Kamati za mitihani zatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu

0

Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limeziagiza kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zote nchini kuhakikisha taratibu zote za uendeshaji wa mitihani ya taifa ya darasa la saba zinazingatiwa.

Agizo hilo limetolewa jijini Dar es salaam na Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt Charles Msonde na kuhimiza mazingira yote ya vituo vya kufanyia mitihani kuwa salama na kuzuia aina yoyote ya udanganyifu.

Dkt Msonde pia amewataka wamiliki wa shule kutoingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha mitihani.

Mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi utafanyika Septemba Tano na Sita mwaka huu ambapo watahiniwa waliosajiliwa ni zaidi ya Laki Tisa na Sitini Elfu katika shule 16,845.

Sharapova na Federer waondolewa US Open

0

Nguli wawili wa mchezo wa Tenisi Maria Sharapova na Roger Federer usiku wa kuamkia Septemba Nne mwaka huu wameondoshwa kwenye mashindano ya US Open baada ya kupoteza michezo yao ya hatua ya Kumi na Sita bora.

Roger Federer alifungwa na John Millman wa Australia ambaye yupo nafasi ya 55 kwenye ubora kwa upande wa wanaume.

Millman alitumia saa tatu na dakika 35 kumtandika nguli huyo wa Tenis,-Roger Federer baada ya kumfunga kwa Seti tatu kwa moja kwenye mchezo huo wa hatua ya kumi na Sita bora.
Baada ya kumtoa nguli Roger Federer, sasa Millman atapambana na nguli mwingine ambaye ni bingwa mara mbili wa mashindano hayo ya US Open,- Novak Djokovic ambaye amemtoa Joao Sousa wa Ureno kwenye hatua ya kumi na sita bora.

Kwa upande wa akina dada, nguli Maria Sharapova naye ameaga mashindano hayo ya US Open ya mwaka 2018 baada ya kukubali kipigo cha seti mbili kwa bila toka kwa Carla Suarez Navarro kwenye hatua ya kumi na sita bora.

Bingwa huyo mara tatu wa mataji makubwa ya Tenis (Gland Slam), – Maria Sharapova alipoteza mara tatu kwenye seti ya kwanza ya mchezo huo na kumfanya apoteza kabisa muelekeo kweye mchezo huo.

Sharapova ambaye kwa sasa ni wa 22 kwenye ubora kwa upande wa akina dada bado hajawa kwenye kiwango bora tangu arejee toka kwenye adhabu ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni na hajawahi kuvuka hatua ya robo fainali kwenye mashindano yeyote yale kwa kipindi cha miezi 15.

Baada ya kumtoa Maria Sharapova, sasa Carla Suarez Navarro atapambana na mshindi wa pili wa mwaka 2017 kwenye mashindano hayo Madison Keys kwenye hatua ya robo fainali.